ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, April 17, 2016

Dart kulipiwa kwa simu za mkononi

Rajab alisema hayo juzi usiku wakati wa mazungumzo baina ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na wakuu wa taaasisi, watendaji wakuu na wadau wa mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka wa jijini Dar es Salaam (Dart), ofisini kwake Magogoni.

Rajab alisema Tanzania inakuwa nchi ya kwanza kuanza kutumia mfumo huo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwamba fedha za mteja zitakuwa salama na hata atakapopoteza kadi yake.

“Mtu akinunua kadi yake anapaswa atunze namba ya usajili iliyoko kwenye kadi hiyo kwani itatumika kurudishia fedha zake kupitia namba yake ya simu ya mkononi,” alisema.

Alisema Maxcom Africa ndio wakusanyaji wa nauli kwa kushirikiana na Uda-RT ambapo watatumia mawakala wa Max-Malipo hivyo kila mwananchi atapata fursa ya kununua kadi yake kwa urahisi.

Alisema taarifa za kila mtumiaji zitaunganishwa na simu yake ya mkononi ambapo mhusika ataweza kujua kwa urahisi salio la fedha lililomo kwenye kadi yake.

Majaliwa aliwaambia wadau hao kuwa hawana muda wa kulala wala kupumzika.

Aidha, Majaliwa amewataka watendaji wa Dart wakamilishe haraka vipengele vichache vilivyobakia ili mradi huo uweze kuanza kazi mapema iwezekanavyo.

“Watu wa Dart, Uda-RT hakuna muda wa kulala tena. Nanyi wa eGA, Maxcom, Polisi na Sumatra inabidi mfanye kazi kama timu moja na wenzenu ili maeneo yaliyobakia yaweze kukamilika katika muda mfupi na kikubwa ni kuhakikisha mnatoa elimu ya kutosha,” alisema Majaliwa.

Akielezea utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Dart, Ronald Rwakatare alisema miundombinu ya mradi huo imekamilika na utoaji huduma unatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Alisema wanamalizia ufungaji wa mfumo wa ukusanyaji nauli na uendeshaji wa mabasi hayo.

Aidha, Rwakatare aliwataka wananchi kutunza miundombinu ya mradi huo na kuwa makini na matumizi ya barabara wakati mradi huo ukiwa kwenye majaribio na hatimaye kuanza kazi rasmi.

Rwakatare alisema watakuwa na karakana itakayotumika kwa ajili mabasi ambayo itakuwepo eneo la Jangwani na kwamba ofisi za mradi pia zitakuwa eneo hilo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Uda-RT, Robert Kisena alisema mabasi yote yamelipiwa kodi pamoja na bima.
Uda-RT ni kampuni ya muunganiko wa Uda na wamiliki wa daladala, ya kutoa huduma ya usafiri katika miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (BRT).

Kisena alisema kesho wataanza majaribio ya mradi huo kwa kutumia mabasi 10 na watakuwa wanaongeza mabasi 10 kila siku hadi yafikie 50 hivyo amewataka wananchi kuondoa shaka juu ya mradi huo.

NIPASHE JUMAPILI

No comments: