ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, April 17, 2016

Mwenye mishahara hewa 17 TRA aonja joto ya jiwe

Rais Magufuli alifichua uwapo wa mfanyakazi huyo hivi karibuni akiwa nyumbani kwake katika Kijiji cha Mlimani, Wilaya ya Chato mkoani Geita, alipokuwa akihutubia kwa mara ya kwanza nyumbani kwake tangu aapishwe kuwa Rais Novemba 5, mwaka jana.

“Yupo mfanyakazi mmoja wa TRA ambaye alikuwa akilipwa mishahara ya watu 17 na huyo ni lazima afikishwe mahakamani,” alisema Rais Magufuli akiwa nyumbani kwake wilayani Chato.

Gazeti hili limefuatilia hatua ambazo TRA imechukua tangu Rais amfichue mtumishi huyo na kuambiwa ameanza kushughulikiwa na kila kitu kitawekwa wazi mambo yatakapokamilika.

“Rais akisema vile ni agizo,” kilisema chanzo kimoja kutoka ndani ya Mamlaka hiyo, "hivyo huyo mtu atafikishwa mahakamani.

"Lakini mambo haya hayawezi kuwekwa hadharani yakiwa nusunusu, (Nipashe) subirini hadi suala zima litakapokamilika mtajua tu maana haiwezi kuwa siri."

Nipashe pia ilimtafuta Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma wa Mamlaka hiyo, Richard Kayombo ambaye alikiri kuwa suala la mtumishi huyo linashughulikiwa na mamlaka ziliozo juu yake, lakini wakati huu si mwafaka kuanika kinachoendelea.

“Ni kweli huyo mtu anashughulikiwa na ngazi za juu kiutawala, sasa hatuwezi kuyaweka kwenye vyombo vya habari mambo ambayo bado yanaendelea kufanyiwa kazi,” alisema Kayombo.

Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Imani Nyamangaro (44) juzi alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida akikabiliwa na tuhuma za kujilipa mishahara hewa 57 yenye thamani ya jumla ya Sh. milioni 29.4.
Mwendesha Mashtaka, Wakili wa serikali, Michael Ng’hoboko alidai kwamba kati ya Aprili 29, mwaka 2013 na Machi, 27, mwaka 2014 mshitakiwa kwa makusudi alilipa mishahara ya wafanyakazi hewa ya zaidi ya Sh. milioni 29.4 huku akijua wazi kwamba kitendo hicho ni kinyume na sheria.

Mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, Joyce Minde, Ng’hoboko alidai kwamba mshitakiwa huyo alikuwa akijipatia mishahara hiyo ambayo wahusika waliisha staafu kazi kwa kipindi cha muda mrefu, kupitia akaunti yake iliyopo katika Benki ya NMB, Tawi la Singida.

Mshitakiwa Nyamangaro alikana kutenda makosa hayo yote 57 na kesi yake imeahirishwa hadi Aprili 27, mwaka huu itakapotajwa tena.

Wiki iliyopita serikali ilitangaza kuanza uchunguzi kuwabaini watumishi wote waliokuwa wakijilipa mishahara hewa ili hatimaye wachukuliwe hatua.

Kwa mujibu wa Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi, Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki, watumishi hewa wameisababishia serikali hasara Sh. bilioni 7.6 kati ya Januari-Machi tu mwaka huu.

Chanzo cha uhakika kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kilieleza Nipashe kuwa tayari serikali imeanza uchunguzi wake kuwabaini maofisa utumishi waliokuwa wakitafuna fedha hizo ili wakamatwe na kufikishwa mahakamani.

Mtoa taarifa wetu alisema ukamataji huo utahusisha hazina, waliolipa, wafanyakazi wa wizarani na hata Halmashauri, na kwamba ni suala ambalo linahitaji upelelezi wa kitaalamu kuwabaini wahusika.

"Wale waliokuwa wakitajirika na mishahara hewa siku zao zinahesabika na uchunguzi unaofanyika si wa kawaida," kilisema chanzo chetu ambacho hakikupenda kutajwa jina.

Hivi karibuni, Rais John Magufuli alitengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ana kilango Malecela baada ya kutangaza kwenye vyombo vya habari kuwa mkoa wake hauna watumishi hewa.

Baada ya taarifa hiyo, Ikulu ilifanya uchunguzi wake na kubaini kuwepo kwa wafanyakazi hewa 45 katika awamu ya kwanza na awamu ya pili ya uchunguzi bado inaendelea.

NIPASHE JUMAPILI

No comments: