ANGALIA LIVE NEWS

Monday, April 18, 2016

KAMPUNI BINAFSI ZAONGOZA KUAJIRI WAHAMIAJI HARAMU

Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Shinyanga, Anamaria Yondani ameeleza kuwa kipindi cha miezi mitatu wamekamata wahamiaji haramu 283, huku kampuni binafsi zikiongoza kwa kuajiri watu hao kinyume cha utaratibu.

Pia alifafanua kuwa wahamiaji hao 111 walikuwa sio rasmi, 45 walifikishwa mahakamani, saba walifungwa, 103 walifukuzwa nchini, 172 waliachiwa huru na waliomaliza kifungo ni wanne.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mwishoni mwa wiki, Yondani alisema kukamatwa kwa wahamiaji hao kumetokana na kufanya msako mbalimbali na kutoa elimu ya dhana ya uhamiaji shirikishi katika makundi mbalimbali ya kijamii.

Alisema wamewakamata wahamiaji haramu hao 283 wengine wakiwa wameajiriwa kwenye baadhi ya kampuni binafsi kinyume cha sheria na taratibu za nchi, wakiwa wanatoka katika mataifa tofauti tofauti.
“Kipindi cha miezi mitatu tumefanikiwa kukamata wahamiaji haramu 283 huku kampuni binafsi zikiongoza kuwapatia ajira kinyume na taratibu, mimi nilikuwa nawaomba wamiliki wa kampuni hata wanapokuwa na vibali vya kisheria wahamiaji hao basi wawaingize katika ajira kwa kufuata utaratibu na sheria za nchi,” alisema.

Alisema wengi wa hao wana vibali vya kuishi, lakini anaingizwa kwenye ajira kinyume cha taratibu na ndio wengi wao wamekamatwa kwa makosa hayo.

 Wahamiaji hao wanatoka nchi za Kenya, Jamhuri ya Congo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Rwanda, Somalia, Ethiopia na China.

1 comment:

Anonymous said...

Kwanini hizo kampuni binafsi zisitumbuliwe? Kwani kila kitu mpaka tumuachie Rais? Tumezidi kuwa walalamishi bila vitendo. Rais ana kazi .