ANGALIA LIVE NEWS

Monday, April 18, 2016

MAKONDA AMTEGA RAIS MAGUFULI

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amemtega Rais John Magufuli baada ya kutamka kuwa hamtaki mkurugenzi wa jiji hilo, Wilson Kabwe na wasaidizi wake na kuomba mamlaka zinazohusika kuwawajibisha kwa madai ya kuusababishia mkoa wake hasara ya zaidi ya Sh3 bilioni.
Dk Magufuli, ambaye ndiye mwenye mamlaka ya uteuzi na utenguzi wa mkurugenzi huyo, kama ataufanyia kazi mtego huo huenda Kabwe akajikuta amehamishwa tena kama alivyoondolewa Mwanza baada ya kulalamikiwa bungeni.
Kabwe alipokuwa mkurugenzi wa jiji la Mwanza aling’olewa kwa njia ya kura bungeni ambapo wabunge walimtaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa wakati huo, kumuhamishia jijini Dar es Salaam kwa kile kilichodaiwa kusababisha matatizo kwa wananchi ikiwamo kuendesha mambo kibabe. Tamisemi sasa ipo chini ya Ofisi ya Rais.
Akiomba mwongozo wa Spika katika kikao kilichofanyika Novemba 14, Selasini alihoji kwa nini mkurugenzi huyo amefanya kazi jiji la Mbeya na kuacha matatizo, vivyo hivyo alivyokuwa Mwanza na sasa amehamishiwa jiji la Dar es Salaam, lakini hachukuliwi hatua.
Akijibu mwongozo wa Selasini, Zungu ambaye alikuwa mwenyekiti na pia Mbunge wa Ilala jijini Dar es Salaam hadi sasa, alisema kwamba Serikali ndiyo ya kulaumiwa kwa kuzembea kuwaondoa viongozi wa aina hiyo akisema Kabwe ni tatizo hata Dar es Salaam.
Jana, Kabwe alipotafutwa na Mwananchi alisema suala analolalamikia Makonda halifahamu.
“Hayo ni maoni yake binafsi hakuna utata wowote kwenye mikataba iliyopo kila kitu kipo sahihi,” alisema Kabwe.
Akizungumzia mikataba iliyosababisha hasara hiyo, Makonda alisema jiji hilo limeingia mkataba na Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo (UBT), maegesho ya magari na Tambaza ambayo yote ni tata.
Alisema walifuatilia na kubaini kuwa UBT ina mikataba miwili; wa mwaka 2004 na mwaka 2009 na kisheria unatakiwa utumike wa 2009, lakini jiji hilo linatumia wa 2004 jambo ambalo ni hasara kwa mkoa.
“Kisheria mkataba unaotakiwa kutumiwa ni wa mwaka 2009 na siyo wa mwaka 2004, tumegundua meneja wa kituo cha Ubungo anapokusanya fedha za ushuru zinapofika jiji zinaliwa na watu wachache kwa kisingizio cha kutumia mkataba wa mwaka 2004,” alisema Makonda.
Alisema mabasi yaliyopo katika kituo hicho ni 350 kwa kutumia mkataba wa mwaka 2004, basi moja linalipia ushuru wa Sh 4,000 na kwa mwezi wanakusanya Sh42 milioni.
Mkataba wa mwaka 2009 unaonyesha kila basi moja linalipia ushuru wa Sh 8,000 na kila mwezi inakusanywa Sh84 milioni, hivyo tangu itangazwe sheria mpya wa mkataba huo haujawahi kutumika.
Makonda alisema mkataba wa mwaka 2004 ulisainiwa Januari 31 mwaka 2015 na mkataba wa mwaka 2009 ulisainiwa Januari 30 mwaka 2015, na yote ilisainiwa na mkurugenzi wa jiji hilo na wasaidizi wake.
Alisema makusanyio yanayotokana na kituo hicho cha mabasi Serikali inapoteza Sh504 milioni kila mwaka, ambapo kuanzia mwaka 2009 hadi sasa imeshapoteza zaidi ya Sh3 bilioni.
Alisema alipokea malalamiko kutoka kwa wananchi kutozwa fedha nyingi kwenye vibanda vilivyopo kwenye kituo hicho, hivyo kuyafuatilia na kuanza kuyafanyia kazi.
Makonda alisema alituma watu wake kufuatilia ndipo walibaini kuwa wapo viongozi wanakodi vibanda zaidi ya vitatu kwa kila kimoja Sh 100,000 na baadaye wanawakodisha kwa kila mtu mwingine kwa zaidi ya zaidi ya Sh1 milioni kwa mwezi.
Pia Makonda alisema walipochunguza mkataba wa Tambaza unaohusika na ukamataji wa makosa madogomadogo ya pikipiki, walibaini kuwa faini inayotakiwa kulipwa kwa makosa ni Sh20,000, lakini jiji linawalipisha Sh80,000 jambo ambalo si sawa.
Kuhusu maegesho ya magari, Makonda alisema wamebaini kuwa muda wa mwenye tenda hiyo umeshakwisha lakini huongezewa miezi sita, sita na mara ya mwisho ameongezewa miezi mitatu bila kufuatwa sheria ambayo ni kutangaza tenda inapokwisha.

No comments: