ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, April 17, 2016

MAMBO SITA KUTIKISA BUNGE LA BAJETI

Wakati Watanzania wakilisubiri kwa hamu Bunge la kwanza la Bajeti ya Serikali ya Awamu ya Tano linalotarajiwa kuanza Jumanne ijayo, wachambuzi wa masuala mbalimbali nchini wamesema litatawaliwa na mvutano wa kisiasa na kuonyeshana umwamba baina ya wabunge kutokana na kuibuka kwa masuala yenye utata tangu Rais John Magufuli aingie madarakani.
Wachambuzi hao wametaja mambo sita yatakayotikisa Bunge hilo kuwa ni sakata la kampuni ya Lugumi inayotuhumiwa kulitapeli Jeshi la Polisi, baadhi ya wabunge kupandishwa kizimbani kwa tuhuma za kuomba rushwa, kupunguzwa kwa Sh6 bilioni katika bajeti ya chombo hicho cha kutunga sheria, uamuzi wa Rais Magufuli kubadilisha matumizi ya fedha na mkakati wa Serikali kubana matumizi na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Wamesema licha ya kuwa Bunge hilo litakuwa na jukumu la kujadili na kupitisha Bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/17 inayoonyesha kutakuwa na makusanyo na matumizi ya Sh29.5 trilioni, mambo yaliyoibuka tangu Rais Magufuli aingie madarakani yasipopatiwa majibu sahihi yataathiri uwasilishwaji wa bajeti hiyo.
Bajeti iliyopita ilikuwa ni Sh22.45 trilioni na kutofautiana na bajeti ya 2016/17 kwa Sh7.1 trilioni na pia katika maeneo mengi, ikiwamo kiwango cha fedha kitakachotengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
Wachambuzi hao wamesema iwapo Serikali itashindwa kuainisha vyanzo vya mapato, itakumbana na hasira za wabunge kutokana na uamuzi wa Serikali ya Marekani kupitia Bodi yake ya Changamoto za Milenia (MCC) kuzuia Sh1 trilioni za misaada yake kwa Tanzania.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Nicolaus Mgaya alisema Serikali lazima ijipange kulitolea ufafanuzi suala la Lugumi kwani litatawala katika Bunge hilo kutokana na mkataba wake kuwa na utata mkubwa huku vigogo Serikali wakitajwa kuhusika.
Kampuni ya Lugumi iliingia mkataba wa Sh37 bilioni na Jeshi la Polisi wa kufunga mashine za kielektroniki za kuchukua alama za vidole nchi nzima lakini badala ya kufunga mashine 106, imefunga 14 tu licha ya kulipwa zaidi ya asilimia 90 ya fedha kwa mujibu wa mkataba.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda alisema kitendo cha wabunge kuhoji uhalali wa kisheria wa Rais Magufuli kuhamisha fedha zilizotengwa kwa ajili ya sherehe mbalimbali na kuzipeleka katika matumizi mengine kitaibuka tena katika Bunge hilo la bajeti.
Aprili 10, wabunge walihoji juu ya jambo hilo katika semina iliyofanyika Dar es Salaam na kuendeshwa na Dk Haji Semboja kutoka UDSM na Harold Sungusia wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
Mbunda alisema hata uamuzi wa Bunge kubana Sh6 bilioni, utazuia maswali na mvutano mkali.
Profesa wa Sheria UDSM, Chris Peter Maina alisema: “Bunge linapaswa kuwa makini kuijadili bajeti hii kwa sababu tayari nchi mbalimbali zimeanza kuonyesha dalili ya kutotaka kuisaidia tena Tanzania.”
Alisema lazima wabunge wajikite kuishauri Serikali kuondokana na utegemezi kwa kutumia uzoefu na utaalamu wao katika masuala mbalimbali.
Kuhusu suala la kubana matumizi, Profesa Maina alisema mjadala wa baadhi ya wabunge kutajwa kuomba rushwa utakitikisa chombo hicho cha kutunga sheria.
Mpaka sasa wabunge watano wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka mbalimbali ya rushwa.
Wabunge hao ni Richard Ndassa (Sumve), Kangi Lugola (Mwibara), Ahmad Saddiq (Mvomero) na Victor Mwambalaswa (Lupa).
“Jambo hili (la wabunge kuhusishwa na rushwa) linaweza kuondoa umakini kwa wabunge wengine katika kujadili bajeti au kuchukua muda mwingi wa mijadala mingine,” alisema.
Katika kubana matumizi, Profesa Maina alisema: “Rais Magufuli ni mtu wa kubana matumizi. Wabunge wanapaswa kujifunza kwake kwa sababu kila Serikali inakuja na mtindo wake wa ufanyaji kazi.”
Kuhusu kubana matumizi, Mhadhiri mwingine wa UDSM Dk, Bashiru Ally alisema; “litakuwa Bunge la mapambano katika upitishaji wa bajeti na mwisho wa siku wengi ndiyo watashinda. Rais amejenga matarajio makubwa kwa wananchi hivyo hapendi kuona yakiyeyuka. Tutarajie kuona siasa zikitawala zaidi. Ni bajeti ya kwanza baada ya Uchaguzi Mkuu. Tunajua kuwa anabana matumizi na anataka kutekeleza ahadi zake. Fedha atazitoa wapi, tusubiri mpango wa ubanaji wa matumizi.”
Mjadala mwingine utakaoliteka Bunge ni Ripoti ya CAG ambayo huwasilishwa kila mwanzo wa Bunge la bajeti na kujadiliwa kwa siku tano.
Ripoti hiyo inatarajiwa kuibua masuala mazito yatakayozua mvutano mkali bungeni huku suala la watumishi hewa na ubadhirifu vikitajwa. Mwaka 2012 Rais mstaafu Jakaya Kikwete alilazimika kufanya mabadiliko ya mawaziri kutokana na kashfa iliyotokana na ripoti ya CAG.

No comments: