Sunday, April 24, 2016

MUHIMBILI NI KAMA TANURU LA MOTO KWA WANAOJIFUNGUA

Inaweza kuwa hospitali bora kuliko zote za Serikali nchini ikiwa na kila aina ya wauguzi waliobobea, vifaa tiba na dawa, lakini Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) yaweza kufananishwa na tanuru la moto kwa wajawazito kwenye baadhi ya wodi.
Muhimbili inahudumia wagonjwa wa aina zote, wengi wakiwa waliopewa rufaa kutoka hospitali za jijini Dar es Salaam na mikoa mingine na hupata huduma kwa madaraja kulingana na uwezo wao, lakini wale wa kiwango cha chini ndio ambao hulazimika kustahimili kila aina ya vitendo visivyo na staha kutoka kwa baadhi ya wahudumu.
Baadhi hujiona kama wanazidishiwa magonjwa na wengine au watoto waliowazaa kwa njia ya upasuaji hupoteza maisha kutokana na huduma zisizo na ubora kutoka kwa baadhi ya wahudumu.
Mwandishi wa gazeti hili (jina tunalihifadhi) alishuhudia vitendo hivyo wakati alipokuwa kwenye wodi namba 33 ya MNH ambayo inahudumia wanawake wengi wanaojifungua kwa njia ya upasuaji.
Wakati mwandishi wetu akiandaa simulizi hii alipata habari ya wauguzi wawili wa kijiji cha Uzia mkoani Rukwa waliomtelekeza mjamzito mapema wiki hii na kumpa mumewe glovu ili amzalishe. Kitendo hicho kilisababisha kifo cha mtoto aliyezaliwa.
“Tukio hili lilinifanya nione kuwa hali ni mbaya kwenye wodi nyingine nyingi nchini na nikahamasika kuiambia jamii mambo haya,” alisema mwandishi wetu.

Mshono wa mzazi wafumuka
Miongoni mwa mambo yaliyoshuhudiwa katika wodi hiyo ni pamoja na mshono wa mwanamke mmoja katika wodi hiyo kufumuka, lakini juhudi zake za kuwaita wahudumu wakati damu ikivuja hazikuzaa matunda hadi baada ya saa tano.
Lugha chafu na isiyo na staha dhidi ya wanawake waliokuwa wakilalamika kutokana na maumivu, na ukosefu wa umakini katika kuhudumia watoto wachanga kwenye chumba maalumu ni mambo ambayo mwandishi wetu alishuhudia kwa kipindi chote cha wiki mbili.
Damu yamlowesha mtoto mchana
Ifikapo saa 6:00 usiku, wauguzi hutafuta sehemu za kulala, mwingine huweza kulala kwenye benchi na mwingine kwenye meza iliyopo wodini humo au kutandika chini.
Mwandishi wa Mwananchi alishuhudia mwanamke aliyejifungua kwa upasuaji akiwaita wauguzi hao usiku kucha bila kupata msaada.
Mwanamke alikuwa na mshono uliofumuka na kusababisha damu kuvuja na hivyo kumlowesha mtoto wake mchanga. Kutokana na wauguzi kutostuka, wanawake wengine waliokuwa wamelazwa na ambao wengi hutembea kwa kujikongoja kutokana na hali inayosababishwa na kujifungau kwa upasuaji, waliungana naye kupaza sauti, lakini hakuna aliyewasikiliza na haikusaidia.
Ilipofika alfajiri saa 11:30 hali ya mgonjwa huyo ilizidi kuwa mbaya na alianza kukoroma, muda ambao wauguzi hao walianza kuamka.
Walipoona damu zimejaa kitandani na mgonjwa huyo akikoroma, waliitana na mmoja wao alimchukua mtoto huyo na kumsafisha. Mwingine alikimbia kuchukua mtungi wa hewa ya oksijeni na kumwekea mwanamke huyo wakati tayari imeshafika saa 12:00 asubuhi.
Mzazi atambaa kufuata dawa
Ukiachana na tukio hilo, wauguzi kwenye wodi hiyo wana tabia ya kuwalazimisha wanawake waliojifungua kwa upasuaji kutembea kwenda kuchukua dawa bila ya kutathmini hali yao.
Asubuhi ya siku hiyo, muuguzi mmoja aliketi mezani kwake na kuwatangazia kinamama hao wakachukue dawa, lakini mmoja (jina linahifadhiwa) alimwambia hawezi kutembea kwa kuwa mshono wake umeanza kufumuka.
Na wauguzi walipombishia, aliamua kutambaa kwa kusota kutoka kwenye kitanda alicholazwa kumfuata muuguzi huyo ili ampe dawa ya kupunguza maumivu. Baada ya kuchukua dawa hizo, maumivu yalionekana kumzidia kabla ya kufika kitandani, lakini alipoomba asaidiwe muuguzi huyo alimjibu kwa kebehi akisema: “Usinisumbue”.
Mgonjwa alimuomba muuguzi aende kumwangalia, lakini alijibiwa kuwa angeenda kwa muda ambao angeamua.
“Hapa siyo TMJ au Regency,” alisema akimaanisha hospitali za kulipia za jijini Dar es Salaam.
“Sina muda huo, nina wagonjwa wengi sana wa kuwapa dawa kama hutaki endelea kukaa hapo hapo.”
Mgonjwa huyo alionekana kuishiwa nguvu, ndipo wagonjwa wengine walipoongeza nguvu ya kumuita muuguzi huyo, hadi alipoacha kugawa dawa na kwenda kumuangalia.
Alipofika, alistuka na kuwaita wenzake ambao walimwekea hewa ya oksijeni na baadaye kumpeleka chumba cha upasuaji ambako walirudishia nyuzi zilizofumuka.
Ni jambo la kawaida kwa wauguzi wa wodi hiyo kukaa kwenye kiti na kuita wagonjwa waende kuchukua, tofauti na wodi nyingine ambazo wagonjwa hufuatwa kitandani.
Vitendo hivyo viliwafanya wagonjwa waliolazwa wakati huo kwenye wodi namba 33, kuwabatiza wauguzi jina la “mabandidu’, neno ambalo halimo kwenye kamusi ya Kiswahili.
Wauguzi hao, ambao wanaonekana kuizoea hali ya wagonjwa kulalamika hata wanapoonekana kuwa katika hali mbaya, hudiriki kuwaambia wale wanaolalamika kwa muda mrefu kuwa ni wasumbufu.

Mionzi machoni mwa kichanga
Watoto wa wazazi hao huwekwa chumba chao maalumu, na baadhi huwa na matatizo kama homa ya mapafu, kunywa maji machafu wakati wa kuzaliwa au homa ya manjano.
Mtoto moja mchanga aliyekuwa na homa ya manjano, alikuwa amewekewa mashine ya mionzi ya kutibu ugonjwa huo bila kufunikwa plasta ya kuzuia mionzi kwenda machoni. Mionzi hiyo huweza kusababisha upofu kwa mtoto.
Wazazi waliokwenda kunyonyesha kwenye chumba hicho, waliona hali hiyo na kumwita ofisa muuguzi ambaye aliizima mashine hiyo.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Muhimbili, Aminiel Aligaesha alisema iwapo wagonjwa wanaona hali hiyo watoe taarifa. “Ni vyema akaripotiwa ili hatua za kinidhamu dhidi yake ziweze kuchukuliwa,” alisema.
“Wauguzi wetu wanavaa nembo za majina. Soma jina lake. Tuna mfumo mzuri sana wa kusikiliza malalamiko kwa hiyo tushirikiane kukomesha vitendo hivi. “Mwisho niwakumbushe watoa huduma kufanya kazi kwa mujibu wa kanuni na taratibu na pia kuzingatia maadili ya kazi kwa kila kada.”
Naye kaimu mkurugenzi mkuu wa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru alisema hajawahi kupata malalamiko lakini akaahidi kufanya uchunguzi.
“Ninachofahamu wauguzi si wanyama kiasi hicho,” alisema Profesa Museru.
“Wagonjwa wengi wamekuwa wakihudumiwa na kurudi nyumbani salama kutoka wodi hiyohiyo. Hatuwezi kusema wauguzi wamekuwa wakisababisha kufumuka kwa vidonda ya wagonjwa kwa sababu ya malalamiko ya mgonjwa mmoja, ila namtuma mtu akafanye uchunguzi nitakupa majibu.”
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu hakupatikana kuzungumzia suala hilo, na naibu wake, Dk Hamis Kigwangalla alikataa kuzungumzia akieleza kuwa si msemaji wa wizara.
300-350
Idadi ya akina mama wodi ya wazazi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili

2 comments:

  1. haya sasa waziri wa afya yuko wapi au wakurugenzi wanaohusika maana kila kukicha mko mnafukuza watu makazini mkiita kutumbua majipu....why not go to muhimbili as undercover and see how real mothers suffer. its very depressing to see such abuse.

    ReplyDelete
  2. minashangaa sana hivi kwa nini mtu anaenda kazini kulala... inamaana wanalipwa mishahara ya bure,.. usiku ndipo wagonjwa wanapougua sana wao wanaenda kulala,, hichi kitendo kinaniudhi sana ,, waziri weka video camera kila kona unase hawa manurse wavivu. mimi ni nurse na ninafanya kazi usiku huwezi funga macho hata dak 5 labda kama uko kwenye break. Pliz pliz waziri Magufuli tuma undercover kama mawaziri wako wameshindwa kazi

    ReplyDelete

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake