Sunday, April 24, 2016

WABUNGE TISA PAC WAPEWA SIKU 30 KUICHUNGUZA LUGUMI

Ukweli kuhusu mkataba tata wa kampuni ya Lugumi Enterprises inayodaiwa kulitapeli Jeshi la Polisi huenda ukajulikana baada ya siku 30, baada ya jana Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuunda kamati ndogo ya watu tisa kuchunguza kwa kina suala hilo.
Makamu Mwenyekiti wa PAC, Aeshi Hilally alisema kamati hiyo ndogo itafanya uchunguzi kwa muda wa siku 30 sambamba na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Uchunguzi huo utafanywa kwa mtindo wa kikachero na ule wa kushtukiza, ili kukwepa hali ya kuandaliwa kwa mazingira ya kuficha ukweli.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Dodoma baada ya kumalizika kwa kikao cha kamati hiyo, Aeshi alisema wameunda kamati hiyo kutokana na kutoridhishwa na yaliyomo katika “Maelezo ya kina kwa maandishi kuhusu utekelezaji wa mradi huo” pamoja na majibu ya Jeshi ya Polisi lililoitwa mbele ya kamati hiyo Jumatano iliyopita.
“Spika wa Bunge (Job Ndugai) ndiye aliyetuelekeza kuunda kamati hii ndogo ambayo itafanya uchunguzi na kuiletea kamati ya PAC mambo yote iliyobaini. Kamati (PAC) itaanda ripoti na kuipeleka kwa Spika kwa ajili ya kuwasilishwa bungeni,” alisema Aeshi.
Kampuni ya Lugumi ilibainika kutotimiza matakwa ya mkataba wake wa kufunga mashine za Utambuzi wa Vidole (AFIS) katika vituo vya polisi 108 nchini kwa gharama ya Sh37 bilioni na badala yake ilifunga katika vituo 14, licha ya kulipwa zaidi ya asilimia 90 ya fedha kwa mujibu wa mkataba.
Ripoti ya CAG ya mwaka 2013/14 ndiyo iliyofichua udhaifu huo, huku taarifa za ndani kutoka PAC zikieleza kuwa mashine mbili kati ya 14 ndizo zinazofanya kazi.
Wajumbe tisa wa kamati hiyo ndogo ni; Japhet Hasunga (Vwawa-CCM), wengine wa CCM ni Livingstone Lusinde (Mtera), Stanslaus Mabula (Nyamagana), Haji Mponda (Malinyi) na Hafidh Ali Tahir (Dimani). Wabunge wa upinzani waliopo katika kamati hiyo ni Nahenjwa Kaboyoka (Same Mashariki-Chadema) Musa Mbaruk (Tanga Mjini-CUF), Tuza Malapo (Viti Maalum-Chadema) na Khadija Nassor Ali (Viti Maalum-CUF).
Akifafanua zaidi kuhusu uchunguzi wa sakata hilo, Aeshi alisema Jeshi la Polisi liliwasilisha utekelezaji wa mkataba huo Aprili 18, mwaka huu na tangu wakati huo kamati ya PAC imekuwa ikiupitia na kubaini kasoro kadhaa.
“Kamati hii itaendesha mambo yake kwa siri na mwisho wa siku italeta majibu. Naamini wajumbe wake watafanya kazi kwa uadilifu mkubwa kwa sababu tunaamini sisi wote ni wazalendo,” alisema.
Alisema kamati hiyo itafanya kazi kwa wiki nne na kuanzia Jumatatu ijayo itakutana kujadili mipango yao, ikiwa ni pamoja na kupanda itakavyoanza na kumaliza kazi zake.
“Siwezi kusema mambo tuliyoyabaini katika maelezo yao maana nitakuwa nimeweka kila jambo litakalofanywa na kamati ndogo,” alisema Aeshi huku akishikwa kigugumizi kusema kama kamati hiyo imeupata mkataba ambao Lugumi iliingia na Jeshi la Polisi.
Alisema kamati hiyo itakagua mashine moja moja, kulingana na majibu ya Jeshi la Polisi lililoeleza siku lilipokutana na kamati hiyo kuwa mashine hizo zimefungwa katika vituo vyote 108.
Baadaye Aeshi alimweleza mwandishi wetu kuwa kamati hiyo itafanya kazi kwa mtindo wa kuvamia maeneo ambayo polisi wanadai wamezifunga, ili kuepuka maofisa wa jeshi hilo kuhamisha mashine kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
“Ripoti ya utekelezaji ya Polisi inaeleza kuwa mashine hizo zipo na zimefungwa katika maeneo husika. Kutokana na majibu hayo kamati ndogo itakwenda kila kituo ili kujiridhisha,” alisema.
Habari kutoka ndani ya kamati hiyo zinaeleza kuwa zabuni ilitangazwa Septemba 22, 2011 na mkataba ukasainiwa Septemba 23 ya mwaka huohuo, ndani ya siku moja mkataba huo ukasainiwa bila kujiridhisha kama mashine husika zinafanya kazi sawasawa.
Kadhalika taarifa hizo zinaeleza kuwa kuna Sh500 milioni hazijulikani zilipo katika mkataba huo, kutokana na taarifa za Jeshi la Polisi kupishana na za CAG.
Mkataba unaeleza kuwa polisi walitoa Sh37.1 bilioni wakati taarifa ya CAG inaonyesha zilitolewa Sh37.7 bilioni jambo ambalo lilishindwa kutolewa ufafanuzi na watendaji wa wizara ya Mambo ya Ndani wakiongozwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenarali Projest Rwegasira walipoitwa na kamati hiyo.
Jambo jingine lililobainika ni zabuni hiyo kutolewa bila ushindani na hivyo kuwa na gharama zaidi.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake