Akizungumza na Nipashe Jumapili jana, Mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Mussa Ali, alisema watamhoji kiongozi wa upinzani na Katibu Mkuu huyo wa Chama cha Wananchi (CUF), ili kusaidia uchunguzi dhidi ya madai yake.
Alisema wanataka awasaidie taarifa za vigogo hao wanaomiliki fedha chafu nje ya nchi ili wachukuliwe hatua za kisheria.
“Tumeunda timu maalum ya kuchunguza tuhuma kama hizo kwa madhumuni ya kuchukua hatua za kisheria pale tunapopata ushahidi wa kutosha hivyo tutamhoji Maalim Seif,” alisema Mussa.
Akizungumza na waandishi wa habari Shangani mjini Zanzibar wiki iliyopita, Maalim Seif alisema kuna viongozi wengi wa SMZ ambao wameficha fedha chafu nje ya nchi.
Alizitaka Jumuiya za Kimataifa kufuatilia akaunti za viongozi hao nje na kuwachukulia hatua za kisheria.
Madai ya Maalim Seif yalikuja katika kipindi ambacho dunia imegubikwa na kashfa ya 'Nyaraka za Panama' ambapo viongozi mbalimbali mashuhuri duniani, akiwemo Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameroon wamegundulika kuficha fedha kwenye nchi hiyo ya Panama.
Waziri Mkuu wa Iceland, Sigmundur Gunnlaugsson alijiuzulu nafasi hiyo Aprili 5 kutokana na maandamano ya kumtaka awajibike baada ya jina lake kuwa mmoja wa watu waluioficha fedha Panama.
Wengine mashuhuri waliotajwa kwenye kashfa hiyo ni pamoja na wasaidizi wa karibu wa Rais wa Russia, Vladmir Putin.
Maalim hakutaja majina ya viongozi hao lakini alisema suala la kuwepo vigogo walioficha fedha nje ya Zanzibar halitaji tochi kwa sababu wengine wanamiliki nyumba za kifahari Dubai kwa fedha walizopata kinyume na sheria.
Wakati huo huo, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imemtaka Maalim Seif kutaja majina ya vigogo anaodai wameficha fedha chafu nje ya nchi.
Akizungumza jana mjini hapa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Mohamed Aboud Mohamed alisema serikali ya Rais Dk. Ali Mohamed Shein itawachukulia hatua za kisheria endapo atawataja.
Maalim Seif alikuwa Makamu wa kwanza wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), lakini CUF ilisusia Uchaguzi Mkuu wa marudio wa Machi 20 na huivyo Katibu Mkuu huyo kupoteza nafasi yake.
CUF ilisusia Uchaguzi Mkuu wa marudio ikidai ilipokwa ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana na mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jecha Salum Jecha ambaye alitangaza kuufuta licha ya waangalizi wa ndani na kimataifa kudai ulikuwa huru na wa haki.
ABoud alisema serikali imedhamiria kupambana na vitendo vya rushwa, ufisadi na kuimarisha misingi ya uwajibikaji kwa viongozi na watumishi wa umma.
Alisema serikali imekusudia kuendelea kuimarisha dhana ya utawala bora na hatua ya kuwataja majina viongozi walioficha fedha nje ya nchi itasadia sheria kufuata mkondo wake.
“Maalim Seif kama ana ushahidi awataje majina viongozi anaodai wameficha fedha nje ya nchi, akifanya hivyo atakua amesadia serikali na vyombo vyake vya sheria,” alisema Waziri Aboud.
NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment