Advertisements

Tuesday, April 5, 2016

UTASHI WA KISIASA UNAHITAJIKA KUDHIBITI SILAHA ZA NYUKILIA-TANZANIA

Silaha kama hizi ( Pichani) na nyinginezo nyingi na ambazo mataifa mbalimbali yanaendelea kujilimbikizia si tu zinataharisha uhai wa sayari dunia lakini pia uhai wa mwanadamu na viumbe hai. Jumuiya ya Kimataifa imekuwa ikikuna vichwa na kujiuliza nini kitatokea endapo silaha hizi ambazo zimeshindwa kudhibitiwa zitangukia mikononi mwa magaidi na makundi mengine ya kiharamia. Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu upunguzaji na udhibiti wa silaha za nyukilia na za maangamizi imeanza mkutano wake wa wiki mbili hapa Umoja wa Mataifa.

Na Mwandishi Maalum,

Wakati Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu upokonyaji wa silaha za maangamizi zikiwamo za nyukilia kushindwa kwa miaka kumi na tano kuwasilisha taaria ya mapendekezo ya kina kuhusu utekelezaji wa jukumu hilo, Tanzania kwa upande wake imeungana na mataifa mengine katika kutoa wito wa kuhakikisha kwamba silaha za maagamizi haziangukii mikononi mwa magaidi na makundi mengine hatari.

Jana Jumatatu, Kamisheni kuhusu ukoponyaji wa silaha, imeanza mkutano wake wa wiki mbili ambapo washiriki wanajadiliana na kubadilishana mawazo kuhusu dhima ya upokonyaji wa silaha za maangamizi na masuala mengine yahusianayo na silaha.

Akichangia majadiliano katika siku ya kwanza ya mkutano , Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, amesema, utashi wa kisiasa unahitajika hasa kutoka kwa nchi ambazo zinamiliki silaha za nyukilia na silaha ninyingine za maangamiii ili kuifanya dunia iendele kuwa mahali salama.

Akabainisha kwamba kutonyesha nia ya kweli ya kudhibiti malimbikizo ya silaha hizo na, kwa Kamisheni kutowasilisha mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ripoti yake kwa kipindi cha miaka kumi na tano sasa ni wazi kwamba kunatoa mwanya wa silaha hizo kuangukia mikononi mwa makundi ya kigaidi na mengineyo.

Ni katika kuliongopa hilo Tanzania kupitia kwa mwakilishi wake, Balozi Manongi imeeleza kwamba hoja ya kwamba kwa nchi kumiliki silaha za maangamizi zikiwamo za nyukilia kunazifanya nchi hizo kuwa na nguvu lakini pia kujenga mazingira ya Amani kuwa haina tija wala matinki yoyote.

“ Suala la upunguzaji wa silaha za nyukilia na silaha nyingine za maangamizi ni jambo linaloitia wasi wasi mkubwa nchi yangu, ni wazi kwamba hatari zitokanazo na nyukilia ziwe kwa bahati mbaya, za kimkakati au kukosewa kwa mahesabu siyo tu kunaitishia dunia lakini pia na wanadamu”. akasema Balozi

Na kuongeza kwamba “ Tanzania inaendelea kuikata ile dhana kwamba kwa namna moja silaha ya nyukilia zinatoa dhamana ya uwepo wa Amani. Kwa upande wetu hatujawahi kujihisi tukiwa na Amani kwa misingi ya kwamba silaha hizo amana zinamilikiwa na rafiki zetu au washirika wao”.

Balozi Manongi ametahadharisha kuwa , katika mazingira ya sasa ambapo pamekuwapo na ongezeko kubwa la makundi yasiyo ya kiserikali yanayotaka kuzipindua serikali halali, hakuna uhakika kwamba makundi hayo hayawezi kugeukia mbinu zozote zile ambazo zinaweza kuingia mikononi mwao.

Kuhusu Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kutowasilisha ripoti yoyote mbele ya Baraza Kuu kwa miaka kumi na tano, Balozi Manongi asema. Kamisheni hiyo haiwezi kukwepa majukumu yake na hasa kama inataka kuendelea kujijenga uhalali.

“Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, limetoa wito wa kuitaka Kamisheni ifanye tathmini na kutoa mapendekezo kuhusu matatizo mbalimbali katika eneo hili la upokonyaji wa silaha, na kutoa maamuzi ya utekelezaji. Mapendekezo ya Kamisheni kwa Baraza Uuu yanatakiwa kutekelezwa na huu ni wajibu wa msingi wa Kamisheni”. akasisitiza Balozi Manongi.

Pamoja na mapungufu kwa upande wa Kamisheni, Tanzania imesema bado na Imani na Kemisheni hiyo na inaitambua kama chombo pekee halali na chenye maamuzi katika Umoja wa Mataifa kuhusu upunguzaji wa silaha za maangamizi..

Awali akizungumza mwanzoni mwa mkutano wa Kamisheni, Mwakilishi Maalum wa Masuala ya upokonyaji wa silaha, Bw. KIM won-soo, pamoja na mambo mengine alikiri kwamba Kamisheni ilikuwa inaingia katika kipindi kingine ambapo kuna mgawanyiko mkubwa miongoni wa jumuiya ya kimataifa kuhusu upokonyaji wa silaha za nyukilia na silaha nyingine za maangamizi.

Akasema kila mjumbe anafahamu kuhusu mgawanyiko huo. Ambao umejidhihirisha wazi kuanzia mkutano wa majereo kuhusu Mkataba wa upunguzaji na usambazaji wa silaha za nyukilia ( NPT) uliofanyika mwaka jana, kushindwa kuanza kwa utekelezaji wa mkataba unaozuia majaribio ya silaha za nyukilia, na kutokuwapo kwa mwendelezo wa majadiliano katika mkutano kuhusu upunguzaji wa silaha.

Hata hivyo na kama ilivyokuwa kwa wajumbe wengine, Bw. KIM won –soo alionyesha matumaini yake kwa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu upunguzaji wa silaha za nyukilia za maangamizi na kwamba wajumbe wake wakifanya kazi kwa pamoja na ushirikiano na bila kutiliana mashaka hapata kuwa na sababu ya kuwenda kutafuta njia mbadala nje ya Umoja wa Mataifa.

No comments: