ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, May 1, 2016

DIWANI AMSHAMBULIA MWENZAKE KWA CHUPA

Diwani wa Kata ya Maparoni, Haji Ngachoka (CUF) ameshambuliwa kwa kupigwa na chupa ya maji na diwani wa Viti Maalumu, Amina Mapande (CCM) katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichokuwa kikiendelea wilayani hapa leo.
Tukio hilo lilitokea wakati Ngachoka alipokuwa akitoa hoja ya kupinga mgawanyo wa mipaka ya wilaya mpya ya Kibiti kuwa ipakane ndani ya Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, wakati kijiografia ipo ndani ya Jimbo la Rufiji.
Akizungumzia tukio hilo, Ngachoka alidai alikuwa akitoa hoja, ndipo aliposhtuka akipigwa chupa ya maji usoni na diwani huyo bila kujua sababu za kupigwa kwake.
“Nilikuwa nikitoa hoja ya kupinga mipaka ya Wilaya mpya ya Kibiti ipakane na Wilaya ya Kilwa, ghafla nilishtukia nimepigwa na chupa ya maji usoni na Amina, baada ya tukio hilo alikuwa akijiandaa kunipiga tena na chupa ya soda ikadakwa,” alidai.
Ngachoka alisema mipaka ya majimbo ya Kibiti na Rufijiilipogawanywa haikuzingatia jiografia ilivyo.
Alisema maeneo ya delta ya kusini kufanywa yawe wilayani Kibiti yataleta usumbufu kwa wananchi, bali yanapaswa yawe Wilaya ya Rufiji.
Diwani huyo alidai kuwa Amina ana tabia ya kupinga hoja zake kila mara akizitoa barazani.
Akijibu tuhuma hiyo, Amina alisema alifanya kitendo hicho baada ya kuchoshwa na hoja za mara kwa mara za Ngachoka kulazimisha Tarafa ya Mbwera iliyopo kwenye delta ya kusini inakopakana na wilaya ya Kilwa ihamishiwe Wilaya ya Rufiji.
“Nilichoshwa na hoja zake za kulazimisha mipaka ya delta ya kusini ambayo ipo Jimbo la Kibiti lililopewa wilaya mpya yahamishwe na kupelekwa Rufiji ,” alisema.
Hata hivyo, alidai hata yeye hushambuliwa kwa maneno makali na Ngachoka kutokana na kukataa maoni yake.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji, Khatibu Chaurembo alisema kitendo hicho ni cha utovu wa nidhamu hatua dhidi ya diwani huyo zitachukuliwa.

No comments: