ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, May 12, 2016

MAKALA YA MABASI YAENDAYO HARAKA

3
Hussein Makame-MAELEZO
UIMARISHWAJI wa miundombinu na uboreshaji wa sekta ya usafiri ni baadhi ya mihimili inayopewa umuhimu nchini katika kuleta maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla hasa pale usafirishaji unapowezesha abiria na mizigo kufika sehemu kwa wakati na kwa gharama nafuu.
Juhudi za Serikali ikiwemo Serikali kuu, Serikali za mitaa, taasisi za ndani na nje ya nchi, mjenzi, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa pamoja zimekuwa zikishirikiana kuimarisha mtandao wa barabara ya kutosha kwa nia ya kuwafikia wananchi wote na katika viwango bora.
Wachumi, wanaeleza kuwa ili taifa lolote liweze kujikwamua kiuchumi ni lazima pamoja na mambo mengine liboreshe sekta ya usafiri kuanzia ndani na nje ya miji ili kurahisisha usafirishaji na kuchangia maendeleo.
Tanzania inatajwa kuwa ni nchi inayoongoza kwa msongamano mkubwa wa magari katika nchi za Jangwa la Sahara huku jiji la Dar es Salaam likiongoza kwa msongamano mkubwa kutokana na kasi ya kuongezeka kwa wahamiaji mijini huku miundombinu yake ya barabara ikibakia ile ile.

Hali hiyo imekuwa ikiathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla mbali na athari za kiafya na kijamii zinazochangiwa na moshi wa magari na kukaa sana kwenye gari wakati wa asubuhi na jioni, hasa kwa wale wanaokaa mbali na sehemu zao za kazi.
Kukamilika kwa barabara katika mfumo wa kisasa wa Usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) katika jiji la Dar es Salaam kumewezesha kupatikana kwa kilomita 20.9 za barabara.
Kilomita hizo ni za barabara kutoka Kimara hadi Kivukoni Ferry, Morocco hadi Magomeni na Fire hadi Kariakoo na miundombinu yake ikiwemo karakana na vituo vikuu vya mabasi hayo.
Ujenzi huu wa barabara ni kielelezo chanya kuelekea mafanikio ya kuleta mabadiliko ya miundombinu ya usafiri jijini Dar es salaam katika muda mfupi ujao.
BRT ni mfumo unaoinukia kwa kasi duniani kwa kusafirisha haraka abiria wengi mijini kwa gharama ndogo kwa kulinganisha na ule wa garimosho za mjini.
Utafiti uliofanywa na Wakala wa Mradi wa Usafiri wa Haraka (DART) hivi karibuni unaonesha kuwa foleni za magari barabarani hupoteza Shilingi Bilioni 655 kwa mwaka nchini na kusababisha changamoto nyingi.
Changamoto hizo ni kupata magonjwa ya akili na maradhi ya mfumo wa hewa inayochangiwa na kukaa sana kwenye magari na kuvuta moshi wa magari kwa muda mrefu njiani kutokana na foleni.
Tafiti mbalimbali zilizofanywa kuhusu usafiri wa jiji hilo zimebainisha maeneo 56 yanayokabiliwa na changamoto za usafiri ikiwemo kuwepo kwa mfumo wa barabara ambao haukidhi mahitaji na hivyo kukosa uwezo wa kuhimili usafiri wa umma.
Mbali na msongamano wa magari, pia inaelezwa kuwa jiji hilo linakabiliwa na kuwepo kwa vyombo vya usafiri vibovu, visivyokidhi mahitaji ya jamii ya wakazi, na upande mwingine taa za kuongozea magari ambazo mara kwa mara zinakuwa mbovu na zilizopitwa na wakati.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Utafiti wa Mradi wa Usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) ya mwaka 2003, msongamano wa magari husababishwa na wingi wa daladala, ongezeko kubwa la magari ya watu binafsi, uendeshaji usiozingatia kanuni na utendaji mbovu kwa baadhi ya askari waongoza magari.
Ripoti hiyo pia inaonesha kuwa jiji la Dar es Salaam lilikuwa na kilomita 450 tu za lami ambazo ni asilimia 39.5 ya kilomita 1,140 za barabara, wakati kilomita 265 tu ndizo zilizokuwa zinatumika katika usafiri wa mabasi jijini humo.
Kwa upande wa vyombo vya usafiri wa umma, ripoti hiyo inaonesha kuwa asilimia 90 ya magari hayo yana umri unaozidi miaka 10 na mengi ni chakavu na hutumia muda mwingi barabarani na kwenye karakana kwa ajili ya matengenezo.
Ripoti hiyo inabainisha changamoto nyingine kuwa,ni ongezeko la kasi la magari, zikiwemo daladala kwa zaidi ya miaka 16 iliyopita huku kukiwa na usimamizi duni wa magari usiokuwa na mabadiliko wala mkakati mpya mbali na kuwepo na mabadiliko hayo katika jiji.
Baada ya kubaini changamoto hizo, wataalamu wa kizalendo wa jiji la Dar es Salaam walianza kuweka mikakati ya kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo na hivyo kuiunda DART chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI wakati huo.
Lengo la kuanzishwa kwa wakala hiyo lilikuwa ni kutaka kutoa huduma bora ya usafiri kwa gharama nafuu katika jiji la Dar es salaam, ambalo ni ni kitovu kikuu cha biashara nchini.
Katika kutekeleza azma hiyo DART ilipanga mkakati wa kuwa na miundombinu bora, inayokubalika kimataifa, yenye manejimenti ya oporesheni ya usafirishaji.
Suala la miundombinu ya barabara ilikabidhiwa TANROADS na kuanzisha kitengo cha BRT ili kujenga mfumo huo unaoelezwa kuwa bora kiufanisi zaidi duniani ulioanzia katika miji ya Curitiba (Brazili), Quito (Equador) na Bogota (Colombia), na baadaye kuingia nchi za ulaya kama Ufaransa.
KWA NINI USAFIRI WA MABASI YA HARAKA (BRT)
“BRT ni aina ya usafiri wa mijini ambao ni nafuu na endelevu kuliko aina nyingine yoyote ya usafiri katika ulimwengu wa leo”
Haya ni maneno ya utangulizi kwenye kitabu cha Ripoti hiyo ya mwaka 2003 yaliyoandikwa na aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam Dkt. Didas Masaburi.
Mbali na kuwa nafuu na endelevu, BRT inaelezwa kwamba ni mfumo wa usafiri unaohudumia watu wengi kwa haraka na hutumia njia maalum na mabasi makubwa yenye uwezo wa kusafirisha abiria wengi hadi 48,000 kwa saa kwa mwendo wa zaidi ya kilomita 22 kwa saa.
Mfumo wa BRT unazingatia mahitaji ya watumiaji wengine wa barabara waenda kwa baiskeli, watembea kwa miguu na huduma maalum kwa walemavu na miundombinu yake hutumika kupunguza muda wa safari.
Moja ya malengo makuu ya mradi huo ni kubadilisha sura ya jiji kwa kuboresha matumizi ya maeneo ya kandokando ya njia kuu ya mradi na kurahisisha maendeleo ya kiuchumi kwa jiji zima.
Kuanzishwa kwa mradi wa BRT kumetokana na kukosekana kwa mradi wa mabasi madhubuti unaokidhi mahitaji yote ya usafiri.
HALI YA USAFIRI WA JIJI LA DAR ES SALAAM
Ongezeko la watu katika jiji la Dar es Salaam linachangia changamoto za sekta ya usafiri na takwimu zinaonesha kwa miaka 20 ijayo, jiji hilo linatazamiwa kuwa na watu 7,614, 459 watakaohitaji huduma ya usafiri.
Inaelezwa pia wakazi wengi wa jiji hilo hupendelea kutumia usafiri wa umma kutokana na sababu za kiuchumi.Hivyo kuanzishwa kwa BRT kutasaidia wananchi wengi wenye kipato duni.
Pia imebainika kwamba abiria wengi na magari mengi yanatumia barabara kuu huku msongamano mkubwa ukiwa katika barabara ya Morogoro ikifuatiwa na Barabara ya Kawawa na Uhuru.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Barabara ya Uhuru miaka 10 iliyopita ilikuwa na abiria wengi kwa kuwa na abiria 15,000 na magari 770 kwa saa, ikifuatiwa na barabara ya Morogoro yenye abiria 9,000 na magari 715.
Barabara ya Kilwa ilikuwa na 6,200 kwa 549, Kawawa 10,000 kwa 383 kwa saa, Barabara ya Nyerere 8,600 na magari 399 kwa saa na Barabara ya Ali Hassan Mwinyi abiria5100 na maagari 281 kwa saa.
Inaonesha pia abiria wengi wanaoelekea katikati ya jiji asilimia 43 hutumia usafiri wa umma, na asilimia 6 hutumia magari binafsi.
Daladala hubeba takrbani abiria mil 1.4 kwa siku huku abiria wengi wakielekea Kariakoo, katikati ya mji (Posta) na hospitali ya Muhimbili na mengine ni Ubungo, Mwenge na Kimara.
UTEKELEZAJI WA MAMBO YA MRADI WA BRT
Utekelezaji wa mradi wa BRT utafanywa kwa awamu sita ambapo awamu ya kwanza imeshakamilika na huduma imeanza kutolewa baada ya kufikia makubaliano juu ya maslahi ya wananchi na Umma kwa ujumla.
Awamu hii ya kwanza inaanzia na Barabara ya Morogoro na Kawawa, ikifuatiwa na Barabara ya Uhuru na Nyerere, na Kilwa na ifikapo mwaka 2035 inategemewa asilimia 91 ya wakazi wa jiji wataweza kupata huduma ya mradi huo.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Utafiti wa Mradi wa BRT, awamu ya kwanza inahusisha njia kuu na lishi zenye mtandao wa barabara wa kilomita 20.85, vituo vya kawaida 29,vituo vikuu 5 na karakana 2 za Ubungo na Jangwani.
Mpango wa muda mrefu wa BRT ni kuwa na kilomita 137 za njia maalum ya mabasi na vituo 18 na vituo vya kawaida 228.
Tayari vituo vikuu viwili vimejengwa vya Kivukoni karibu na kituo cha Kivuko cha Kigamboni na Soko la Samaki na cha Ubungo karibu na Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo Mikoani (UBT).
Vituo vingine vilivyokwishajengwa ni Ubungo, Kimara (Kimara mwisho), Kariakoo (mtaa wa Msimbazi na njia ya Reli) na Morocco ambapo kila kituo kitahudumia mabasi 65 kwa saa kwa kila mwelekeo.
Mabasi ya njia kuu yatakuwa aina ya kumbakumba yenye uwezo wa kubabe abiria 140 na kila basi litakuwa na safari ya kilomita 14 kila siku.
NJIA KUU ZA MRADI WA MABASI AWAMU YA KWANZA
Lengo la BRT ni kusafirisha abiria wengi kwa muda mfupi, kufupisha muda wa kusimama vituoni kwa kuimarisha usafiri wakati wa asubuhi na jioni ambapo maahitaji ya awali yalionesha huduma ya mabasi 40 kwa saa na katika vipindi vya kawaida mabasi 10 kwa saa (kila baada ya dakika 5)
Ilielezwa kuwa usafiri wa BRT utakuwa na safari 7 kupitia njia saba katika barabara kuu, safari za haraka 2 na safari 5 za kawaida na muda wa kazi ni kuanzia saa 11 alfajiri mpaka saa 5 usiku kila siku.Hata hivyo huwenda muda huo ukafanyiwa mabadiliko kulingana na mahitaji.
Kwa mujibu wa DART kila njia kuu itakuwa na vituo vya kusimama kwenye vituo maalum kama inavyoonesha hapo chini.
DR001-UBUKOO, ni njia inayohusu mabasi yanayotoa huduma kati ya Kituo Kikuu cha Ubungo na Kituo Kikuu cha Kariakoo na yatasimama katika vituo vyote 15 na kuhudumia abiria 3,329 asubuhi na jioni 1,880 kwa mzunguko wa dakika 47.
DR002-KIMKOO, inahusu mabasi yanayotoa huduma kati ya Kituo Kikuu cha Kimara na Kituo Kikuu cha Kariakoo na yatasimama katika vituo vyote 14 vya Kimara terminal, Resort, Thomas, Baruti, Corner, Kibo, Ubungo, Tanesco, Kituo Kikuu cha Ubungo, Bakhressa, Baptist Church, Fire, Uhuru Street na Kituo kikuu cha Kariakoo).
Abiria wa asubuhi wanakadiriwa kufikia 6,801 na jioni abiria 3,505 na mabasi hayo yatatumika kwa mzunguko wa dakika 67 na itatoa huduma ya haraka yaani service index katika kiwango cha asilimia 43
Njia ya DR003-KIMKIV, ni ya mabasi yanayotoa huduma kati ya Kituo Kikuu cha Kimara na Kituo Kikuu cha Kivukoni na yatasimama katika vituo vyote 26 ikiwemo vya Kimara terminal, Korogwe, Bucha, Resort, Thomas, Baruti, Corner, Kibo, Ubungo Tanesco, Kituo Kikuu cha Ubungo, Shekilango, Urafiki, Manzese Tipo Top, Bakhressa, Manzese Agentina, Kagera, Mwembechai, Usalama, Baptist Church, Jngawani, Fire, DIT, Kisutu, Nyerere Square, Posta ya Zamani, Kivukoni na Magogono Ferry.
Abiria wanaotegemewa kusafiri ni 7,215 wakati wa asubuhi na jioni ni abiria 3,048 na watatumia dakika 82 kwa mzunguko.
DR004-MORKOO, ni njia inahusisha mabasi yanayotoa huduma kati ya Kituo Kikuu cha Morocco na Kituo Kikuu cha Kariakoo na yatasimama katika vituo vyote 12 (Morocco, Kinondoni B, Mwanamboka, Mkwajuni, Kanisani, Magomeni Hospitali, Baptist Church, Jangwani, Fire, Uhuru Street na Kituo kikuu cha Kariakoo) na mzunguko wa safari ni dakika 38.
DR005-MORUBU, ni njia ya abiria wanaosafiri kati ya Kituo Kikuu cha Morocco na Kituo Kikuu cha Ubungo ambapo mabasi yatasimama katika vituo vyote 16.Asubuhi inategemea kusafirisha abiria 6,189, jioni abiria 3,419 na itatumia mzunguko wa dakika 24.
DR006-MORKIV, inahusisha mabasi yanayotoa huduma kati ya Kituo Kikuu cha Morocco na Kituo Kikuu cha Kivukoni na yatasimama katika vituo vyote 25.Asubuhi inategemea kusafirisha niabiria 2,935 na jioni abiria 1,928.Njia hii itakuwa na mzunguko wa dakika 46.
DR007-, UBUKIV.Hii ni njia ya mwisho itakayosarisha abiria kati ya Kituo Kikuu cha Ubungo na Kituo Kikuu cha Kivukoni na yatasimama katika vituo vyote 12 vya Ubungo terminal, Shekilango,Urafiki, Mahakama, Bakhressa, Magomeni Kagera, Fire, Bibititi, Libya, City Council, Posta ya Zamani, na Kivukoni terminal).
Inategemea kuwa na abiria 2,726 asubuhi na jioni abiria 1,766. Nji hii itachukua mzunguko wa safari wa dakika 25 na inategemewa kutoa kiwango cha huduma ya haraka kwa asilimia 38.
Vituo hivi saba vitatoa huduma ya urefu wa kilomita 145.8.Hata hivyo ili kuendana na viwango vinavyohitajika na huduma kuwa endelevu, basi moja linatakiwa kusafirisha abiria 2,000 kwa siku.
Safari zote zitachukua jumla ya mabasi makubwa 116 ikiwemo mabasi 6 ya akiba na mabasi lishi 237 na inakadiriwa kuwa abiria 350,000 watasafirishwa kila siku.
Kuhusu nauli, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya UDA Rapid Transit (UDART), David Mgwasa anasema nauli za mabasi zitakuwa shilingi 200 kwa mwanafunzi, shilingi 650 kwa njia maalum na kwa njia lishi nauli ni shilingi 400 na wanaounganisha njia zote za lishi na maalum watalipa shilingi 800.
Abiria watanunua tiketi zao kwa keshia nayepatikana kwenye kila kituo cha mabasi hayo au watanunua kadi ambayo ataipangusa (tap) kwenye mashine iliyopo kituoni na kupewa tiketi.
Anasema UDART kwa sasa iko kwenye mchakato wa kuhakikisha abiria anaweza kulipia nauli kwa kutumia simu ya mkononi au kupitia benki.

No comments: