Katika kuadhimisha siku ya Mama Duniani, mke wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Mama Salma ameelezea maisha yake ya ulezi huku akifafanua nini kilimsukuma kuja na kaulimbiu ya ‘Mtoto wa Mwenzio ni Wako.’
Alisema kaulimbiu hiyo aliyoiibua katika taasisi yake ya Wanawake na Maendeleo (Wama), ni matokeo ya maisha yake halisi aliyoyaishi.
Mama Salma aliyasema hayo jana alipokuwa akihojiwa nyumbani kwake Msoga mkoani Pwani, katika kipindi cha 360 kinachorushwa na Televisheni ya Clouds.
Alisema licha ya kufanikiwa kulea watoto tisa ndani ya familia yake, pia ni mama wa watoto wengi wanaosoma katika shule mbili za sekondari zilizoanzishwa na taasisi hiyo.
“Nilianzisha kaulimbiu ya ‘Mtoto wa Mwenzio ni Wako’ nikiwa nimelenga kuifunza jamii kwamba watoto wote wanapaswa kuonyeshwa upendo, haijalishi siyo wa kumzaa au uliyemkuta barabarani, kwani hawana makosa kuzaliwa pahala fulani, hivyo hawapaswi kuhukumiwa,” alisema mama Salma.
Alisema watoto alionao ndani ya familia yake, amekuwa akiwalea kwa kuwaelekeza, kuwawekea mipaka japokuwa alikuwa akikumbana na changamoto kadhaa za ulezi jambo ambalo alifanikiwa kulidhibiti.
Kuhusu kazi yake
Alisema kwa kuwa yeye ni mama anayefanya kazi, amekuwa akijipangia ratiba ya shughuli zake za ofisini na muda wa malezi ya watoto wake, huku msaada mkubwa akiupata kutoka kwa mumewe.
“Mume wangu amenisaidia kwa mambo mengi sana hasa kwenye malezi ya watoto wangu tisa ambao wa kwanza akiwa Ridhiwan ambaye sasa ameoa na wa mwisho anaitwa Mohamed, hawa wote nimewalea kwa kuwaelekeza katika mambo mbalimbali.
“Nataka niwaeleze wazazi wenzangu, malezi bora siyo lazima utumie fimbo bali unapaswa kuwaeleza watoto wako ukweli kwamba haya ni maziwa na hili ni tui la nazi, watakuelewa zaidi badala ya kutumia nguvu na ukali,” alisema Mama Salma.
Akielezea changamoto ya malezi ya sasa, alisema mambo yanayofanyika kwenye mitandao ya kijamii imekuwa kishawishi kikubwa kwa watoto wengi kujiingiza katika mambo yasiyofaa.
Hata hivyo, alisema siyo jambo jema kwa wazazi kuwatupia lawama watoto wao, bali wazazi wanapaswa kutumia mamlaka waliyopewa na Mungu kutenga muda wa malezi ya watoto wao, kwani wanapopanga ratiba zao vizuri, watafanikiwa kuwalea watoto wao kwa namna wanavyopenda.
“Unakuwa mwanamke hatimaye mama, kuwa mama ni kitu muhimu sana na unapaswa kutumia nafasi hiyo vizuri kwa watoto wako, lakini kumbuka kwamba mumeo pia unapaswa kumwangalia karibu na kumtia moyo kila mara, huo ndiyo umama,” alisema huku akifunguka kwamba anapokuwa nyumbani mbali na kuandika, hupendelea kupika vyakula mbalimbali kwa ajili ya familia yake.
Akiizungumzia taasisi yake ya Wama, Mama Salma ambaye ni mwenyekiti wa taasisi hiyo, alisema alianza kujihusisha na masuala ya kusaidia watoto yatima na wasiojiweza miaka mingi, lakini kutokana na ongezeko la watoto hao, aliamua kujenga shule ili wote wasome sehemu moja kwa lengo la kurahisisha ufuatiliaji wa makuzi yao.
No comments:
Post a Comment