ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, May 7, 2016

MVUTANO WAIBUKA UHALALI WA KAZI ZA MAWAZIRI WA MAGUFULI

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju

Hatua ya mawaziri kuanza kutekeleza majukumu yao Desemba 28, 2015 bila kuwapo kwa sheria ya mwongozo wa muundo wa majukumu hayo, imechukua sura mpya baada ya wanasheria nchini kusema ni kinyume na mfumo wa utawala wa kisheria.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana wanasheria hao wamesema upo uwezekano kuwa iwapo watendaji waliotumbuliwa na mawaziri hao watakwenda mahakamani kupinga kuna uwezekano maamuzi hayo yakatenguliwa kwa sababu walikuwa wanafanya kazi bila kujua majukumu yao ambayo yalipaswa kutolewa Rais John Magufuli.
Wanasheria hao walikuwa wakitoa maoni yao kufuatia sakata lililoibuliwa na Aprili 22 mwaka huu na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe ambaye alisema Serikali ya Awamu ya Tano ilikiuka kifungu cha 5 (1) cha Katiba kinachoweka masharti kwa Rais kutengeneza mwongozo wa muundo na utekelezaji wa majukumu ya serikali yake kwani hadi siku ile haukuwapo mwongozo.
Mbowe ambaye aliwaongoza wapinzani kususia kuwasilisha na kujadili hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu alisema Serikali ya Awamu ya Tano haikuwa na mwongozo uliosainiwa na Rais, ilikuwa ikitumia uliosainiwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Desemba mwaka 2010.
“Mheshimiwa Spika, mpaka sasa mwongozo wa utendaji wa Serikali kwa kila Wizara unaotumika ni ule uliochapishwa kwenye gazeti la Serikali namba 494A la tarehe 17/12/2010,” alisema.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju walimjibu Mbowe kwamba Rais halazimishwi kutoa mwongozo huo, lakini waliibuka baadaye na kutoa mwongozo huo na kuutangaza katika gazeti la Serikali (GN), ikiwa imepita miezi minne tangu mawaziri waanze kazi.
Wanasheria hao wamesema nchi lazima iongozwe kwa sheria na taratibu na si kila Rais kuchukua uamuzi wake na kwamba hata kama Serikali itatoa mwongozo leo, utaeleza majukumu ya wizara kuanzia siku ulipotolewa na si kuanzia siku ambayo mawaziri waliapishwa.

Wanasheria
Wakili na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Jesse James alisema, “Wapinzani wako sahihi. Tunapozungumzia mfumo wa utawala wa sheria maana yake kila jambo linalofanywa na Serikali lazima litanguliwe na sheria. Sheria ndiyo inayoongoza maamuzi yote ya Serikali na taasisi zake.”
Alisema kabla ya mawaziri kuapishwa lazima mwongozo huo uwe umeandaliwa ili wajue mipaka na majukumu yao ya kazi na wakifanya kazi bila kuwepo kwa jambo hilo inaweza kutafsiriwa kuwa majukumu yao hayapo kwa mujibu wa sheria.
“Bahati mbaya Rais Magufuli alibadilisha wizara. Mfano, Tamisemi aliitoa ofisi ya waziri mkuu na kuipeleka ofisi ya rais. Hapa lazima utoe mwongozo kueleza majukumu mapya ya wizara. Kama angeacha wizara kama zilivyokuwa tungeweza kusema anatumia mwongozo wa Serikali iliyopita,” alisema Jesse.
“Kisheria kama mawaziri wametekeleza maamuzi bila kufuata sheria wakati sheria ilitakiwa itangulie kabla ya maamuzi, maana yake ni kwamba maamuzi waliyoyafanya yanaweza yakatenguliwa na mahakama.”
Jesse alikifananisha kitendo hicho na kumtoza mtu kodi kisha unakwenda bungeni kutunga sheria ya kodi. “Ukifanya hivyo lazima uwarejeshee watu fedha walizowatozwa,” alisema
Alipoulizwa kama waliotumbuliwa wakienda mahakamani wanaweza kushinda kesi, Jesse alitoa kauli iliyofanana na ya mwanasheria wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Hamisi Mkindi kwamba jambo hilo linategemea na tafsiri ya mahakama.
Katika ufafanuzi wake Mkindi alisema, “Ili mwongozo huo uweze kufahamika na umma unatakiwa utolewe kwenye gazeti la Serikali. Sasa bila hivyo nani atajua majukumu yake, mbona hatujaona GN?”
Alisema kama suala hilo halijatangazwa katika gazeti la Serikali maana yake ni kwamba halipo na umma haujui chochote. “Kama huna mwongozo wa utendaji wako wa kazi unafanyaje kazi? Wapo wanaosema kuwa Rais huamua jambo hilo lakini ifahamike kuwa unapoongoza nchi lazima ufuate sheria, kanuni na desturi za nchi za Jumuiya za Madola,” alisema.
“Kama ni kweli sheria inasema hivyo, je ule utamaduni tunaoufuata uko wapi na kama umeunda wizara kwanini usiwape mawaziri mwongozo? Tusifike mahali tukasema kila anachokifanya rais ni halali.”
Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Charles Rwechungula alisema, “Kama kuna sheria inayosema mawaziri hawawezi kuanza kazi bila mwongozo itakuwa ni makosa ya kisheria na kikatiba.”
“Bila kusema kuwa ni kauli ya wapinzani au vipi, kama sheria inasema hivyo na haijafuatwa hakuna shaka kwamba Serikali imekwenda kinyume na matakwa ya sheria na katiba, hili si jambo jema kwa taifa.”

Kauli ya Dk Mwakyembe
Akijibu suala hilo ambalo pia liliibuliwa na Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani bungeni, Tundu Lissu juzi wakati akiwasilisha maoni ya upinzani ya Wizara ya Katiba na Sheria, Dk Mwakyembe alisema Rais anapoteua mawaziri kwa kupitia ibara ya 55 ya Katiba, sharti muhimu ili waziri aanze kutekeleza majukumu yake ni kuapa mbele ya Rais.
“Siyo kwamba lazima uwepo mwongozo. Na ibara ya 56 inasema Waziri au Naibu Waziri hatashika madaraka yake ila mpaka awe ameapa kiapo cha uaminifu kwa Rais au kiapo kingine,”alisema.
“Hakuna mwongozo (instrument) hapa ili uje uwe Waziri. Rais anaweza akakaa hata miaka mitatu bila kuwa na mwongozo na Serikali ikaenda,” alisema Waziri Mwakyembe bungeni mjini Dodoma.

1 comment:

Anonymous said...

Upuuzi mtupu. Watu wanappokosa lakusema siku zote watazua mambo ya ajabu kwani unaofanya kazi ni muongozo au mawaziri? Ukiangalia wanasiasa wa upizani Tanzania utakugundua ni watu wa hovyo kupita kiasi. Wanajaribu kutumia nguvu kubwa kumrejesha nyuma Magufuli katika jitihada na harakati zake za kuikomboa Tanzania kutoka katika dimbwi la uzembe na ubadhirifu wa rasilimali zetu ulioipelekea nchi kuwa masikini wakati ikiwa imejaa rasimali. Watanzania hawatki muongozo kwani muongozo ulikuwepo wakati wa Mwinyi,Mkapa,Kikwete lakini Tanzania na watanzania bado wamebakia wakiteseka hata kula yao ya shida. Watanzania wanahitaji maendeleo kitu ambacho kwa kipindi kifupi cha utawala wa muheshimiwa Maghufuli ameonesha yakuwa inawezekana. Maghufuli amewaletea watanzania matumaini mapya lakini kwa upande wa upizani ni dhahiri kitu hicho kinawakera. Muongozo gani Mbowe anaoudai katika serikali ya Magufuli kama vile kujifanya yeye Mbowe ni mtu wa kufuata sheria wakati alihongwa na lowasa na kumpitisha kidikteta kugombea kiti cha uraisi kupitia tiketi ya chadema na ukawa leo hii ati yeye Mbowe kawa ni mtu wakufuata sheria kama si unafiki kitu gani? Tunaomba wale wote wanayoitakia mema Tanzania na watanzania wawe kutoka wapinzani au ndani ya CCM au taasisi za nje au za ndani wamuache Magufuli afanye kazi yake. Ile nchi ilishaoza sifikirii kama kulikuwa na muongozo au miongozo inaiongoza. Watanzania iwe wanasiasa au raia wa kawaida kujifanya tunajua katika midomo yetu ni vitu vya kwawaida lakini tukija katika suala la utekelezaji siku zote tunashindwa lakini Magufuli amethibitisha kwa vitendo yale yote aliokuwa akiyasema wakati wa campaign kwa hivyo jitihada zozote zile zikiwa za ndani au za nje za kutaka kumzuia Magufuli kuwaletea watanzania maendeleo ni ufisadi uliopitiliza mipaka.