FREDERICK Sumaye, Waziri Mkuu Mstaafu ameeleza kushangazwa na Serikali ya Rais John Magufuli kupenda kusifiwa zaidi na kuchukia kukosolewa
Sumaye bila kumtaja jina Rais Magufuli ameleza kushangazwa na hatua ya serikali kuminya uhuru wa habari na kwamba, kufanya hivyo kunalenga kuficha madudu yanayofanywa na watendaji wake.
“Wapowatawala ambao hawapendi kusemwa lakini wanapenda sana kusifiwa. Kiongozi mwenye tabia ya udikteta hataki kusikia kingine zaidi ya sifa zake tu.
“Huyo ni mtu hatari na katika nchi ya namna hiyo hakuna uhuru wa habari wala uhuru wa kutoa maoni kwa woga wa kupotezwa kusikojulikana,” amesema Sumaye.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari yaliyoratibiwa na Chama cha Waandishi wa Habri za Siasa (TAPOREA), Sumaye amesema, serikali inakiuka Katiba ya nchi.
Amesema, serikali yoyote inayopambana na vyombo vya habari na kuminya uhuru wa kufanya kazi zao huwa ina tatizo kwa upande wa wanaotawala.
Akitolea mfano wa hatua ya serikali kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya bunge Sumaye amesema, kwa kufanya hivyo serikali imevunja Katiba.
“Unapoondoa matangazo ya moja kwa moja ya vipindi vya Bunge, kwanza ni kuvunja katiba. Ibara ya 18 (d) ya Katiba inasema, kila mtu ana haki ya kupewa taarifa wakati wote.
“Kwa kuzuia Bunge kuoneshwa ‘live’ (moja kwa moja) wewe serikali unataka kutoa taarifa ya Bunge kwa wakati unaoutaka na kwa taarifa unayoitaka wewe,” ameeleza Sumaye.
Kuhusu sababu iliyotolewa kwamba, matangazo hayo yanatumia gharama ya Sh. 4 bilioni amesema haina mashiko.
Sumaye amesema, hata kama matangazo hayo yatarushwa na ofisi za bunge bado, gharama zitaongezeka zaidi kwa sababu Bunge litahitaji kununua mitambo pamoja na kuajiri wafanyakazi wake.
Sumaye amesema, serikali yenye demokrasia ya kweli lazima ikubali wananchi wake kutoa maoni.
“Serikali yoyote yenye utawala bora, ingependa mambo yake inayoyafanya kwa ajili ya wananchi wake mambo hayo yajulikane kwa wananchi hao.
“Ukiona serikali inaficha mambo yake lazima kuna mambo wanayoyafanya ambayo hayafai na wasingependa jamii ijue,” amesema Sumaye.
George Maziku, Mkurugenzi Mtendaji wa TAPOREA amezungumzia ripoti ya hali ya uhuru wa waandishi wa habari na uhuru wa vyombo vya habari kimataifa, iliyotolewa na Shirika la Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka lenye Makao Makuu yake nchini Ufaransa haipendezi.
Amesema, ripoti hiyo inaonesha kuwa, katika miaka 10 iliyopita zaidi ya waandishi wa habari 800 kutoka mataifa mabalimbali duniani wameuawa wakiwa wanatekeleza kazi zao.
“Kitisho kingine kwa uhuru wa vyombo vya habari nchini ni utamaduni mpya ulioasisiwa na kuimarishwa na watawala wa sasa na kuvishinikiza vyombo vya habari kutomkosoa Rais John Magufuli na serikali yake.
“Matokeo yake, vyombo vingi vya habari nchini vimelazimika kuandika habari za kumfurahisha Rais Magufuli,” amesema Maziku.
4 comments:
Sumaye na wale wote wanaolilia kutoonyeshwa kwa matangazo ya bunge ya moja kwa moja ya tv kuwa ni kunyimwa kwa uhuru wa habari ni upuuzi mtupu. Wakati mwengine unajiuliza kama wapinzani na wale wote wenye bifu la kukosa uongozi wamekosa la kukosoa katika serikali ya Magufuli. Tulitegemea kuona wapinzani wakidai vitu vya maana kama vile kuanzishwa kwa tv tegemezi itakayojihusisha na shughuli za bunge baada ya kulilia television ya uma kuwalazimisha watu wote kuangalia upuuzi wa watu wazima wakikashifiana kwa kisingizio cha siasa. Siamini yakwamba watanzania wote ni waendawazimu wa siasa na ndio maana kwa wenzetu waliotutagulia kimaendeleo kuna tv stations kwa kila shughuli kama vile sports,politics,music na nakadhalika.
Very true ��������
Well said, TV ya taifa haiwezi kutumia siku nzima kwaajili ya kuonyesha malumbano ya wanasiasa. Kuna mambo ya kuelimisha jamii ambayo watu wengine wangependa kutazama. Ukawa wanaweza kuanziaha tv yao ambayo ita cover bunge siku nzima. Msilizamishe watu wote kuangalia upuuzi unaofanywa na wabunge wanao tafuta sifa kwenye tv badala ya kufanya kazi. Kujenga hoja na kuleta maendeleo si lazima uonekane live kwenye tv. Anzisheni hata redio basi. Wengi tumekulia kwenye kile kipindi cha kusikiliza kila kitu rdeioni. Bishanieni mambo ya muhimu acheni kupoteza muda kudai kuonekana kwenye tv.
VERY SAD INDEED!!! Anonymous May 4, 2016 at 9:09 AM, LET US STICK ON THE ISSUE; Please STOP ATTACKING PEOPLE WITHOUT SUFFICIENT DATA
Post a Comment