ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, May 29, 2016

UREKEBISHAJI MIASHAHARA UMMA KUKAMILIKA FEBRUARI MWAKANI

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Angela Kairuki
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Angela Kairuki

SERIKALI imesema wamelipa madai ya watumishi mbalimbali 24,675 yenye thamani ya Sh bilioni 22 huku ikieleza tathmini ya urekebishaji mishahara kwa watumishi wa umma itakamilika mwezi Februari mwakani.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais , Utumishi na Utawala Bora Angela Kairuki aliliambia bunge juzi jioni wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge kuhusu makadirio ya bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi,Teknolojia na Ufundi.

Alisema kati ya madai hayo walimu 14,366 waliokuwa wakidai takribani Sh bilioni 10.7 wameshalipwa madai yao na sasa wameshapokea madai mbalimbali na wanaendelea kuhakiki madai yenye thamani ya Sh bilioni 11.5 na yakithibitika ni halisi yatalipwa bila shaka.

Kairuki alisema lengo la serikali siyo kuwalipa posho zaidi watumishi wake bali kuboresha mishahara na wameanza zoezi la tathmini ya kazi na upangaji wa madaraja. Alisema kama alivyosema kwenye bajeti yao siyo kwa walimu pekee bali watumishi wote wa umma kwa kuainisha mishahara na posho mbalimbali au marupurupu na aina ya kazi si kwa walimu tu kwani kuna watumishi wenye sifa sawa lakini wanapishana mshahara mara tano au kumi.

“Zoezi litakamilika Februari mwaka kesho na siyo kwa walimu pekee ila serikali nzima kwa watumishi wa umma kwa kuainisha mishahara na posho mbalimbali huku wakiangalia aina ya kazi,” alisema.

Akizungumzia malimbikizo ya mishahara kwa watumishi, alisema tangu walipoanza taarifa za kiutumishi za mishahara Mei 2012 wamekuwa wakitekeleza ulipwaji wa madai mbalimbali.

“Lakini tumekuwa na changamoto ya madai hayo kukokotolewa ‘automaticaly’ kupitia mfumo huku walimu wengine wakipeleka madai yale yale ‘manual’ hivyo wakati mwingine kutofautiana na ya ‘automatic’, ”alisema.

Kairuki alisema hali hiyo imekuwa ikiwapa tabu na kujikuta wanapokea madai mara mbili kwa hiyo ilikuwa lazima kufanya uhakiki na aliwaomba walimu na watumishi wengine kuwa na subira lakini wajitahidi kuhakikisha wanapeleka madai ambayo ni sahihi na kuwaasa waajiri kuwa hawatapokea madai ‘manual’.

HABARI LEO




No comments: