ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, July 21, 2016

BINTI ANAYEANDIKIA ULIMI AOMBA MSAADA

By Colnely Joseph,Mwananchi Cjoseph@mwananchpapers.co.tz

Dar es Salaam. Msichana aliyepooza mwili wake, Wakonta Kapunda ambaye ni miongoni mwa waandishi wa miswada ya filamu waliochaguliwa katika tamasha la Maisha Film Lab lililofanyika siku chache zilizopita visiwani Zanzibar anaomba msaada ili kukamilisha ndoto zake za kuwa ‘daraja’ kati ya jamii na Serikali.

Wakonta alipooza baada ya kugongwa na gari akiwa katika maandalizi ya mahafali ya kidato cha sita ya Shule ya Sekondari ya Wasichana Korogwe mkoani Tanga.

Wakonta alisema jana kuwa anashindwa kumudu gharama za uchunguzi wa maendeleo ya afya yake na matibabu kwa kukosa fedha.

“Watu wanaopata matatizo kama yangu huwa katika wakati mgumu kutokana na kuchelewa kupona, nahitaji uangalizi wa karibu wa daktari na changamoto inayonikabili ni fedha,” alisema.

Pia, alisema anahitaji kuishi jijini Dar es Salaam ambako itakuwa rahisi kupata msaada wa tiba na fedha.

“Jijini hapa nimepata wadau wengi na wakongwe katika kuandaa ‘script’, hivyo nitajifunza zaidi na kuwa mahiri jambo litakalonisaidia kutimiza ndoto zangu.

“Nilikuwa mtu wa kukaa tu nyumbani (baada ya kupata ajali) na kuanza kutumia muda wangu mwingi kutazama picha, ndipo nilipopata wazo la kuanza kujifunza kuandika na nikaituma katika mashindano hayo na kuchaguliwa.

“Nilianza kwa tabu kuandika kwa ulimi, lakini kwa sasa nimezoea na siumii kama zamani,” alisema.

Baba yake, Bazilio Kapunda alisema changamoto zinazoikabili familia hiyo ni za kiuchumi kutokana na malezi ya Wakonta.

“Amepata fursa hii ya filamu, lakini bado anahitaji wadau wengi kumuunga mkono,” alisema.

No comments: