Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama hicho, Edward Lowassa na viongozi wengine waandamizi wameitwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwenda kuripoti kesho Septemba Mosi.
Hatua hiyo inatokana na viongozi hao kukamatwa juzi, baada ya kufanya mkutano maalumu wa ndani wa Kamati Kuu, na walipelekwa Kituo Kikuu cha Polisi cha Kanda hiyo na kuhojiwa kabla ya kuachiwa.
Mbali na Mbowe na Lowassa, viongozi wengine wa Chadema waliokamatwa na kutakiwa kwenda Polisi kesho ni Katibu Mkuu, Vincent Mashinji, Naibu wake, John Mnyika na Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho, Said Issa Mohammed.
“Wameitwa Polisi waende Septemba mosi kuripoti baada ya jana kukamatwa na kuhojiwa wakituhumiwa kukiuka maagizo ya Polisi,” alisema Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene na kufafanua:
“Lakini wanaweza kwenda au wakaanzia kwenye maandamano kisha wakaenda Polisi kuripoti.”
Alisema maandamano hayo yatakuwapo kama yalivyopangwa kwani maandalizi yake yamekamilika.
Habari zaidi zilieleza, kwamba jana mchana viongozi hao walikuwa wakifanya kikao Makao Makuu ya chama hicho Kinondoni Dar es Salaam, ambapo pia walikutana na wabunge wote wa chama hicho kwa makundi tofauti.
Kwa mujibu wa mtoa habari ndani ya Chadema makao makuu katika kikao hicho walijadili mambo mengi ikiwa ni pamoja na suala la utekelezaji wa Ukuta kesho.
Mmoja wa wabunge wa Chadema alisemai kwamba walikuwa wakiwekana sawa kuhusu maandamano yao.
Alibainisha kwamba katika mkutano huo ambao Mbowe hakuwepo pia walijadili maombi ya viongozi wa dini kuwataka kusitisha maandamano hayo Septemba mosi.
“Viongozi wa dini wamekuwa wakituomba tusitishe maandamano ya Ukuta Septemba mosi, tusubiri hadi baada ya mkutano wa vyama vya siasa Septemba tatu,” alisema Mbunge huyo wa Kanda ya Ziwa.
Aliongeza: Katika mkutano huo, Lowassa na viongozi wengine walijadili hayo na ikikubalika kwa heshima ya viongozi wa dini maandamano ya Ukuta yafanyike baada ya Septemba tatu.”
Hata hivyo, mwandishi alishuhudia wabunge wengi wa chama hicho wakitoka katika mkutano huo kimya kimya bila kutaka kuzungumza na kabla muda uliopangwa kwisha, huku taarifa zikieleza kwamba mkutano huo uliahirishwa baada ya kuwepo taarifa za kutaka kuvamiwa na Polisi.
“Tumeambiwa tusambaratike, tutajulishwa wapi tutakutana tena, kama hapa au wapi,” alidokeza mmoja wa wabunge hao.
Baada ya mkutano huo kuahirishwa, Lowassa alitoka eneo hilo huku taarifa zikieleza alikuwa akielekea kwenye moja ya hoteli jijini humo kuungana na Mbowe ambapo walikuwa na mazungumzo na baadhi ya viongozi wa dini.
No comments:
Post a Comment