ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, September 10, 2016

HOFU YATANDA FAO LA KUJITOA KWA WANACHAMA WA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII

Na Mwandishi Wetu
HATUA ya Serikali kuwa katika maandalizi ya kuliondoa fao la kujitoa imezua taharuki miongoni mwa wafanyakazi ambao wengi wao ni wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii.
Hali hiyo imekuja baada ya Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), kuandaa muswada wa mabadiliko ya Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambao kwa sasa upo katika hatua za mwisho, huku ikielezwa kuondolewa kwa fao la kujitoa na badala yake kuletwa fao la kutokuwa na ajira.
Taarifa za kuondolewa kwa fao hilo zimesambaa kwenye mitandao ya kijamii, hivyo kuzua mjadala mkubwa kwa wafanyakazi wa sekta mbalimbali nchini.
Katika mapendekezo hayo inaelezwa kuwa mfanyakazi ambaye amechangia zaidi ya miezi 18, atalipwa asilimia 30 ya mshahara wake wa mwisho baada ya kupoteza ajira.
Mbali na hilo, pia atalipwa kwa miezi sita mfululizo, kisha malipo hayo yatasitishwa. Anayestahili malipo hayo ni yule ambaye hakuacha kazi kwa hiari yake (resignation).
Inaelezwa katika mapendekezo hayo ya awali kuwa baada ya miaka mitatu tangu kusitishwa kwa fao la kujitoa, mfanyakazi atakayekuwa hajapata ajira ataruhusiwa kuhamisha michango yake kutoka kwenye mfuko wa lazima (Compulsory Scheme), kwenda mfuko wa hiari (Supplementary Scheme).
Kutokana na mabadiliko hayo, mfanyakazi atakuwa na hiari kuchukua fedha zake kulingana na mfuko wa hiari aliojiunga nao na pia atakuwa na haki ya kuendelea kuchangia.

“Na kwa mfanyakazi aliyeachishwa kazi akiwa amechangia chini ya miezi 18, atakuwa na haki ya kuchukua asilimia 50 ya michango yake mara baada ya ajira kukoma,” ilieleza sehemu hiyo ya mapendekezo ya sheria hiyo.
Kutokana na taharuki hiyo ya kuondolewa kwa fao la kujitoa, MTANZANIA ilimtafuta Mkurugenzi wa SSRA, Irene Isaka ambaye alikiri kuwapo kwa muswada huo ambao bado upo katika hatua za awali.
Alisema hatua ya kufanyika kwa marekebisho hayo inatokana na mifuko ya hifadhi ya jamii kutokuwa na sheria ya fao la kujitoa.
“Sheria za mifuko ya hifadhi ya jamii hazina fao la kujitoa, ila kwa sasa suala hilo lipo katika ngazi ya mapendekezo, ikiwamo upande wa Serikali. Na baada ya kukamilika yatachukuliwa na kwenda kwa wadau na kujadiliwa kabla halijaridhiwa.
“Na linafanyika hili kwa lengo la kuwasaidia wananchi kuweza ku-access (kupata). Hivyo ni vema tusubiri kwanza Serikali iliridhie ndiyo tunaweza kusema.
“SSRA tunawaomba Watanzania wasubiri maelekezo ya Serikali kwanza, na hawana haja ya kuhamaki kwa suala hilo,” alisema Irene.


KAULI YA SERIKALI
MTANZANIA ilipomtafuta Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu, Bunge Kazi, Ajira, Vijana, Wazee na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama kuzungumzia suala hilo, alisema kwa sasa bado wanaendelea na kazi ya kushauriana na wadau na ikikamilika atatoa taarifa kwa umma.
“Kwa sasa bado tunaendelea na kuzungumza na wadau ili kuweza kupata maoni yao, na tukikamilisha kazi hii tutatoa taarifa kwa umma,” alisema Jenista.


WAZIRI KIVULI
Akizungumzia muswada huo, Waziri Kivuli wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu, Bunge Kazi, Ajira, Vijana, Wazee na Wenye Ulemavu, Esther Bulaya (Chadema), alisema muswada huo hauna dhamira njema na badala yake unataka kuwafunga watu kwa hiari.
“Muswada huu hauna dhamira njema kwa wafanyakazi na ndiyo maana unataka kupelekwa bungeni kwa njia za panya… Utakumbuka huko nyuma wadau walioukataa. Sasa inakuwaje maoni ya wadau yafanywe siri katika suala linalohusu haki za wafanyakazi?
“Tunajua namna Serikali inavyokopa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kwa ajili ya miradi ya maendeleo, leo kutaka kuondoa fao hili ni sawa na kuwafunga kwa hiari.
“Huku nyuma mtu aliweza kufanya kazi na kama aliacha aliamua kuchukua fedha zake ili zimsaidie kwenye miradi, sasa kuja na utaratibu wa muswada huu haikubaliki,” alisema Bulaya ambaye bado anatumikia adhabu yake ya kutohudhuria vikao vya Bunge.

TUCTA WAPINGA
Akizungumzia muswada huo, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Nicholaus Mgaya, aliitaka Serikali kuliacha fao la kujitoa kwa sababu linaweza kuwasaidia wafanyakazi kujiunga na mfuko wanaoutaka ili waweze kupata faida.
Akizungumza na MTANZANIA jana kwa simu, alisema kuwa miongoni mwa mambo ambayo shirikisho hilo lilikuwa likiyapigia kelele ni pamoja na kuanzishwa kwa fao hilo ambalo linaweza kuwasaidia wafanyakazi.
“TUCTA tuliwasilisha mapendekezo ya kuitaka Serikali kuanzisha fao la kujitoa ili kutoa fursa kwa wafanyakazi kujiunga na mfuko wanaotaka, ambao wanaona wanaweza kupata faida zaidi, jambo ambalo limesaidia hata baadhi ya wabunge kutuunga mkono,” alisema Mgaya.
Alisema TUCTA inapinga uamuzi wa Serikali kutaka kuwalipa wafanyakazi ndani ya miezi sita halafu wanawaacha, kwa sababu wanaweza kuwasababisha waendelee kuwa masikini.
Mmoja wa wadau alihoji ni namna gani mfanyakazi anayelipwa mshahara wa Sh 180,000 ataweza kumudu gharama za maisha baada ya kupoteza ajira kwa kulipwa asilimia 30 ya mshahara wake.
“Mfanyakazi anayelipwa mshahara wa Sh 180,000 kama akilipwa asilimia 30 ya mshahara wake ni sawa na Sh 54,000 kwa mwezi baada ya kupoteza ajira yake, huyu ni vipi ataweza kumudu gharama za maisha?” alisema.
Aprili 13, mwaka 2012 Bunge lilifanya marekebisho na kuondoa fao la kujitoa (withdrawal benefits) – mafao ambayo yalikuwa yakitolewa pindi mwanachama alipokuwa anaacha kazi na kulazimu kupata mafao pale atakapofikisha umri wa kustaafu kwa hiari (miaka 55), kwa lazima (miaka 60) au pale anapopata ulemavu wa kudumu.
Kutokana na marekebisho hayo, Mbunge wa Kisarawe, Selemani Jafo (CCM) – kwa wakati huo, aliwasilisha muswada binafsi bungeni wa kutaka sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii ya mwaka 2012, hususan kipengele kinachomtaka mfanyakazi kupata mafao yake baada ya kufikisha umri wa kustaafu kwa hiari miaka 55 au 60 kirekebishwe.
Jafo ambaye kwa sasa ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais (TAMISEMI), alifikia uamuzi huo baada ya kuona kukiwa hakuna dalili kwa Serikali kuwasilisha bungeni muswada wa marekebisho ya sheria kama ilivyoahidi.
Hatua hiyo ya Jafo, aliichukua baada ya aliyekuwa Mbunge wa Ubungo – sasa Kibamba, John Mnyika (Chadema), kuwasilisha kwa Katibu wa Bunge kusudio la kuwasilisha muswada binafsi wa sheria hiyo kwa hati ya dharura.

No comments: