ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, September 6, 2016

MGODI WA DHAHABU WA BULYANHULU WAKABIDHI MADAWATI KWA MKUU WA MKOA WA SHINYANGA

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi,Zainab Telack akikata utepe kuashiria kupokea madawati yaliyotolewa na kampuni ya Acacia.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ,Bi Zainab Telack (aliye vaa ushungi) akiongozwa na Meneja wa Ustawi na Mahusiano ya Jamii wa Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu Elias Kasitila (kushoto kwake) wakati wakielekea uwanja wa Taifa wa mjini Kahama kwa ajili ya makabidhiano ya Madawati kutoka kampuni ya Acacia. 
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Telack akihutubia wananchi katika uwanja wa Taifa Kahama wakati wa zoezi la Kukabidhiwa madawati kutoka kwa kampuni ya Mgodi wa Dhahabu wa Acacia, Bulyanhulu.
Wafanyakazi wa Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu,kutoka kushoto ni Meneja wa Ustawi na Mahusiano ya Jamii katika Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu, Elias Kasitila, Afisa Miradi Mzee Hamisi, Afisa Mahusiano ya Jamii William Bundala Chungu pamoja na Afisa Mahusiano ya Jamii David Magege, wakiwa katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama kabla ya zoezi la Kukabidhi Madawati.

Madawati yaliyotolewa na kampuni ya Acacia kwa ajili ya shule katika mkoa wa Shinyanga.


Na Dixon Busagaga, Shinyanga.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Telack amekabidhiwa madawati 2,000 yenye thamani ya Shilingi 240,800,000/= na Mgodi wa Dhahabu wa Acacia Bulyanhulu uliopo katika Halmashauri ya Msalala, Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga. Makabidhiano yamefanyika leo mjini Kahama.

Akimkabidhi madawati hayo Meneja wa Ufanisi wa Mgodi wa Acacia Bulyanhulu Bwana Elias Kasitila amesema, “hii ni awamu ya nne kwa mgodi wa Acacia Bulyanhulu kukabidhi madawati ndani ya mwaka huu katika kipindi ambacho taifa linaendelea kutekeleza kampeni ya kitaifa ya dawati kwa kila mwanafunzi iliyoagizwa na Mheshiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr John Pombe Magufuli kwa lengo la kuboresha mazingira ya elimu nchini Tanzania.”

Ameongeza kuwa, “licha ya Mgodi wa Dhahabu wa Acacia Bulyanhulu kuchangia madawati pia inachangia miradi mingine kwenye jamii lakini kwenye sekta ya elimu mgodi unashirikiana na jamii kuitekeleza miradi kama vile ujenzi na ukarabati wa nyumba, ofisi za walimu madarasa, maabara za sayansi na udhamini wa masomo kwa wanafunzi.”

Mkuu wa Mkoa Shinyanga Bi Zainab Telack amesema, “ Tukio hili la kukabidhiwa madawati ni tukio kubwa, nimefurahi sana na ninajua furaha ya watoto watakaotumia madawati haya itakuwa mara mbili yake, kwa hivyo kwa niaba ya Mkoa wa Shinyanga nawashukuru sana Mgodi wa Dhahabu wa Acacia Bulyanhulu kwa kututengenezea madawati elfu mbili, mkoa wa Shinyanga ulikuwa na upungufu wa Dawati elfu 7000 lakini sasa kupitia mchango wa leo kutoka Bulyanhulu na wadau wengine sasa mkoa wetu unamaliza kabisa upungufu wa madawati.”

No comments: