ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, November 29, 2016

JAFFO AFUNGUA MAFUNZO YA SHERIA YA MANUNUZI YA UMMA MKOANI DODOMA

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mheshimiwa Selemani Said Jaffo amewataka watumishi wa Umma wanaoshiriki kwenye michakato ya manunuzi kuzingatia udilifu wakati wanapotekeleza majukumu yao ili kuzuia upotevu wa fedha za serikali zinazoelekezwa kwenye manunuzi mbalimbali.
Naibu Waziri Jaffo ametoa kauli hiyo alipokuwa akifungua mafunzo ya Sheria ya Manunuzi ya Umma inayoendeshwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kwa Maafisa Masuhuli, Wenyeviti wa Bodi za Zabuni, Wakuu wa Vitengo vya Usimamizi wa Manunuzi na Idara Nunuzi inayofanyika mjini Dodoma.
Amesema uzoefu unaonesha kuwa baadhi ya watumishi wa Umma ambao wamepewa dhamana ya kusimamia michakato ya manunuzi kwenye taasisi zao wamekuwa hatekelezi wajibu wao ipasavyo na hivyo kusababisha kupatikana kwa wazabuni ambao hawana uwezo wa kutekeleza kazi husika aau kazi kutekelezwa chini ya kiwango.
Akitolea mfano baadhi yao, Naibu Waziri Jaffo amesema “baadhi ya wajumbe wa bodi za zabuni wamekuwa wakishiriki katika vitendo visivyo vya kiuadilifu na mwisho tunapata wazabuni wasio na vigezo na hivyo kusababisha hasara kwa Serikali”.
Alitoa pia wito kwa wakuu wa taasisi za umma kuepuka vitendo vya mgongano wa kimaslahi kwenye michakato ya manunuzi ya umma na kutokubali kuyumbishwa na wasiasa.
“Naomba kuwasihi wakuu wa taasisi msikubali kuyumbishwa na wanasiasa ambao wameingiza kampuni zao kwenye michakato ya manunuzi kwani hali hiyo husababisha kazi nyingi kutekelezwa chini ya kiwango na hivyo kukosa thamani ya fedha kwenye miradi inayotekelezwa kwa fedha za Umma,” alisema Naibu Waziri.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa PPRA, Dkt. Laurent Shirima, alielezea baadhi ya maeneo yenye changamoto kubwa kwenye manunuzi ya umma kuwa ni pamoja na usimamizi wa mikataba ya manunuzi. “Eneo la utekelezaji wa mikataba ndilo linalotumia fedha nyingi kwenye mchakato mzima wa manunuzi ya umma. Hivyo usimamizi mzuri katika eneo hili ni muhimu sana, lakini tumeshuhudia mapungufu mengi kwenye eneo hili kupitia ukaguzi ambao ambao tumeufanya katika mwaka wa fedha 2015/16,” alisema Dkt. Shirima.

Mafunzo hayo yanayoendeshwa na PPRA ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, ya kuitaka Mamlaka hiyo kuwapatia mafunzo kuhusu sheria ya manunuzi wakuu wa taasisi za umma ili wawe na uelewa wa kutosha katika kusimamia shughuli za manunuzi ya umma kwenye taasisi zao.

No comments: