ANGALIA LIVE NEWS

Monday, December 19, 2016

DALILI ZA UGONJWA WA ZIKA NA JINSI YA KUJIKINGA UNAVYOAMBUKIZA

Ugonjwa wa zika unasababishwa na virusi vinavyoitwa zika ambavyo huenezwa na mbu wajulikanao kama Aedes.
Kwa mara ya kwanza ugonjwa huu uligundulika kwa nyani nchini Uganda mwaka 1947, wakati wa kutafiti ugonjwa wa homa ya njano.
Si jambo la kushangaza kwa ugonjwa huu kugundulika hapa nchini kwani baada ya kugundulika kuwapata nyani, baadaye mwaka 1952 ugonjwa huu uligundulika kuwapata binadamu nchini Tanzania na Uganda.
Mwaka jana ugonjwa huu ulianza kuwa gumzo tena, baada ya taarifa za kitabibu kuonyesha kuwa kuna wagonjwa wenye maambukizi nchini Brazil.
Mara nyingi mbu anayeeneza virusi wa zika huwa na kawaida kuwauma wanadamu nyakati za asubuhi, mwishoni mwa mchana na jioni. Kama ilivyo kwa magonjwa ya malaria, njano, dengue na chikungunya yanayoenezwa na mbu, wadudu hawa humwachia mwanadamu virusi wakati anapomuuma na kufyonza damu.
Dalili za ugonjwa huu zinafanana na za homa ya dengue na chikungunya, magonjwa ambayo pia yanaenezwa na mbu ambazo ni homa, kutokwa vipele, macho kuwa mekundu yenye machozi, uchovu, kichwa kuuma, maumivu ya misuli na maungio.
Bado kitaalamu haijulikani muda wa kupata maambukizi mpaka kuibuka kwa dalili. Kwa kawaida dalili na viashiria huweza kudumu kwa siku 2-7.
Ugonjwa huu si mkali unapompata mtu, mwili wenyewe unaweza kukabiliana nao kwa kutumia mfumo wa kinga ya mwili.
Ugonjwa huu umekuwa ukijadiliwa maeneo mbalimbali duniani na kila kukicha wanasayansi wanaendelea kuufanyia utafiti.
Taarifa mpya zinaeleza kuwa ugonjwa huu unahusishwa na kuzaliwa kwa watoto wenye hitilafu au maumbile yasiyo timilifu.
Hitililafu ya kuzaliwa inayojulikana ni ile ya mtoto kuzaliwa akiwa na kichwa kidogo, kitabibu hujulikana kama “microcephally”.
Vilevile maambukizi ya zika yanahusishwa katika kuchochea kutokea kwa ugonjwa unaoathiri mfumo wa fahamu ambao husababisha udhaifu na kupooza kwa viungo vya mwili (miguuni), tatizo hili hujulikana kitabibu kama “Guillain-Barre syndrome”.
Ugonjwa huu unaweza kuambukizwa pia kwa njia ya kujamiana, kwa kuongezewa damu bado tafiti zinaendelea kuthibitishwa.
Utambuzi wa ugonjwa huu hujikita zaidi kwa kuangalia dalili na viashiria vya ugonjwa pamoja na historia ya kusafiri au kutembelea maeneo yenye mlipuko wa ugonjwa wa zika.
Uwepo wa maambukizi wa ugonjwa huu unaweza kuthibitishwa kwa kutumia vipimo vya maabara kwa kupima sampuli ya damu au majimaji mengine ya mwilini ikiwamo mkojo, mate na majimaji ya sehemu za siri.
Kama nilivyoeleza hapo awali, maambukizi ya zika hayasababishi kuumwa sana bali huwa ni kawaida na hakuna matibabu maalumu ya kuangamiza virusi hivyo.
Mgonjwa hushauriwa kupumzika sana, kunywa maji mengi au vyakula vyenye majimaji ikiwamo juisi za matunda. Dawa za matibabu zinazotolewa ni zile za kuondoa maumivu ya mwili na homa tu.
Inapotokea dalili zimekuwa mbaya zaidi mgonjwa apelekwe haraka katika huduma za afya kwa uangalizi wa kitabibu. Mpaka dakika hii hakuna chanjo ya zika ingawa tafiti zinaendelea kusaka chanjo.

Mbinu za kujikinga
Mbinu za kujikinga na ugonjwa huu ni kama zile za kuzuia maambukizi ya homa ya malaria.
Njia hizi ni pamoja na kuvaa mavazi yanayokinga mwili kuumwa na mbu, kuishi katika nyumba yenye madirisha yenye wavu wa kuzuia mbu kupenya na kufunga madirisha na milango ya nyumba. Watu walale ndani ya chandarua kilichowekwa dawa maalumu ya kufukuza mbu yenye kiambata dawa kijulikanacho DEET, IR 3535 au Icaridin. Wazazi au walezi watoe msaada wa kuwakinga watoto na wazee au wagonjwa ambao hawawezi kujikinga wenyewe. Tahadhari za mapema zichukuliwe kwa wasafiri au watalii wanaotembelea maeneo yenye mlipuko wa zika.
Vilevile ni muhimu sana kuangamiza maeneo yanayochangia mazalia ya mbu ikiwamo kuondoa maji yanayotuama na vitu vinavyobeba maji kutuama ikiwamo vipande vya vyombo, vifuu na matairi.
Jamii inatakiwa kushirikiana na serikali za mtaani katika juhudi za kupunguza mbu katika maeneo yao kwa kuweka mazingira yao wanayoishi ikiwamo kupulizia dawa za kuuwa mbu na kukata nyasi zinazozunguka maeneo wanayoishi. Ikumbukwe kuwa pale unapokabiliana na ugonjwa wa zika vilevile inakusaidia pia kukabiliana na magonjwa mengine ikiwamo homa ya dengue, chikungunya na njano pamoja na malaria

2 comments:

Anonymous said...

Hizi report ..magonjwa yote yameanza Africa ....

Anonymous said...

Africa ni jaa la watu wa Magharibi kusukumia kila baya na balaa linalomkabili binaadamu. Tunaambiwa ukwimwi umeanzia Africa wakati kuna ushahidi tosha kabisa yakwamba umeanzia New York city marekani kwa wanaume waliokuwa wakijihusisha na ngono ya jinsia moja. Na zika nayo tunaambiwa imeanzia Africa wakati kuna taarifa za kutosha yakwamba mbu waliozalishwa kwa majariribio nchini Brazil na wataalam wa wakimarekani ili kwenda kupambana na mbu wengine wanaosababisha maradhi kwa wanaadamu kama vile maleria na dengu wamekuwa ndio chanzo cha zika. Mambo mengi ya hovyo Africa inasukumiwa na hakuna wa kukanusha.