ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, December 14, 2016

RC TABORA AMWAGIZA RPC AMTUMBUA OCD WAKE

Image result for Aggrey Mwanri
Mhe. Mwanri amemwagiza
Na Mwandishi wetu, Tabora

MKUU wa Mkoa wa Tabora ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo Aggrey Mwanri amemwagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa ACP Hamis Issa kumchukulia hatua za kinidhamu OCD wa Igunga na askari aliyekuwa zamu kwa kosa la uzembe.

Ametoa agizo hilo jana alipotembelea familia ya wafiwa wilayani Igunga Mkoani humo akiwa ameambatana na Kamati nzima ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na ile ya wilaya ambapo alikabidhi rambirambi ya sh 256,000/- kwa baba mzazi wa marehemu.

Alisema kifo cha kijana Isahaka Juma (21) aliyekuwa dereva wa bajaj, aliyekodiwa na watu wasiojulikana na kisha kutekwa na kuuawa huku watekaji wakiharibu na kuchomoa vifaa vya bajaj hiyo kimemsikitisha sana, hivyo akamwagiza RPC kuwasaka wahusika wote.

‘Nawapongeza sana kwa mshikamano wenu uliowezesha kupatikana kwa mwili wa marehemu uliotelekezwa kijiji jirani, lakini nimesikitishwa sana na hali iliyojitokeza ya kutopata ushirikiano kutoka kituo cha polisi wilaya mlipoenda kutoa taarifa na kuomba msaada wa gari’, alisema.

Alisema kitendo cha wananchi kupeleka taarifa za tukio la mauaji kituo cha polisi na kuomba msaada wa gari la polisi ili kwenda kuchukua mwili wa marehemu lakini wakanyimwa kwa sababu zisizoeleweka, hakikubaliki na sio cha kiungwana.

‘RPC na Kamati yako ya nidhamu nakuagiza mchukulie hatua za kinidhamu OCD wa wilaya hii (Mayila Pesa) na askari aliyekuwa zamu siku hiyo aliyeletewa taarifa akashindwa kutoa ushirikiano hali iliyopelekea kuchukizwa sana wananchi’, alisema.

Alisema kazi ya Polisi ni kulinda usalama wa raia hivyo wanapaswa kuwa mstari wa mbele kukomesha matukio ya uhalifu na kushirikana na wananchi wakati wote pasipo kuweka masharti yoyote.

Alifafanua kuwa kitendo cha polisi kutotoa ushirikiano kwa wananchi kilichochea hali ya sintofahamu ikiwemo wananchi kuamua kufunga barabara kuu itokayo Dar es salaam, jambo ambalo halikubaliki, hivyo akatoa wito kwa wananchi kuwa watulivu na kujiepusha na mihemuko ya
namna hiyo.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa Hamisi Issa alimhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa atachukua hatua stahiki kwa OCD na askari huyo kwa kutowajibika ipasavyo, na aliahidi kuwasaka usiku na mchana watekaji hao ili watiwe nguvuni, pia aliomba ushirikiao wa wananchi ili
kufanikisha zoezi hilo.

Aidha aliwataka polisi wilayani humo kuhakikisha wanakomesha matukio yote ya utekaji bodaboda na bajaji na kuonya askari yeyote atakayeendekeza uzembe atatumbuliwa mara moja kwa kuwa wapo vijana wengi sana wanaotafuta nafasi ya kujinuga na jeshi hilo.

No comments: