ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, December 15, 2016

UNICEF yaadhiminisha miaka 70 tangu kuanzishwa, Serikali yaipongeza kwa kusaidia watoto

Mwakilisha wa Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) nchini, Bi. Maniza Zaman akielezea kazi ambazo UNICEF imekuwa ikizifanya kwa miaka 70 tangu kuanzishwa na mafanikio ambayo wameyapata.

Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) limeadhimisha miaka 70 tangu kuanzishwa (1946-2016) likiwa na kauli mbiu ya Kwa Kila Mtoto, Tumaini. Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Bi. Maniza Zaman alisema shirila lao kwa kipindi cha miaka 70 limekuwa likifanya kazi za kuwasaidia watoto ambapo malengo yao ni kuhakikisha watoto wanaishi maisha bora na kuwawezesha kufikia malengo ambayo wanatamani kuyafikia. 


"Hii ni siku muhimu kwetu kufikisha miaka 70, ni muhimu kwa sababu ya malengo ambayo yamewekwa ya kujenga dunia ambayo kila mtoto atapata haki zake za kimsingi bila kumuacha hata mmoja nyuma ni muhimu sababu ya uwepo wenu kujadili umuhimu wa watoto ambao utatoa matumaini mapya kwa kila mtoto Tanzania, "Kwa miaka 70 UNICEF imekuwa ikiwatetea watoto, kwa pamoja tukishirikiana na wadau wetu kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha tunaboresha maisha ya kila mtoto duniani kote.

 Mpango wetu upo wazi kuwa kuhakikisha kila mtoto anapata nafasi ya kufikia malengo yake," alisema Zaman. Nae Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema UNICEF ni washirika wazuri wa serikali kutokana na programu ambazo wamekuwa wakitoa kwa watoto na kuwaomba kuendelea kushirikiana na serikali ili kuboresha maisha ya watoto nchini. 
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akizungumza faida ambazo Tanzania imepata kutokana na uwepo wa UNICEF nchini pamoja na kumshukuru Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi kwa kusaini mkataba ambao uliwaruhusu UNICEF kuingia nchini kwa ajili ya kuwasaidia watoto.

"Serikali ya Tanzania itaendelea kulinda na kutetea haki za watoto na katika utekelezaji wa hili tunawashukuru sana UNICEF kwa programu ambazo wamekuwa wakizifanya, watoto wa Tanzania wamefaidika sana na programu ambazo UNICEF mnazitoa na serikali itaendelea kushirikiana na UNICEF kuwasaidia watoto nchini," alisema Mwalimu. Kwa upande wa Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN), Alvaro Rodriguez alisema UNICEF imesaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha maisha ya watoto duniani kote tangu ilipoanzishwa na kupitia mpango wa SDGs ni matumaini ya UN kuwa serikali ya Tanzania kwa kushirikiana nanyi zitaendelea kushirikiana ili kuwasaidia watoto. 
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN), Alvaro Rodriguez akielezea jinsi UNICEF ambavyo natekeleza mipango ya Umoja wa mataifa kwa kuanza na mpango wa kwanza wa Millenium Development Goals (MDGs) ambao ulimalizika mwaka 2015 na mpango wa sasa wa maendeleo endelevu (Sustainable Development Goals - SDGs).

"Mchango wa shirika hili la watoto ni mkubwa, muhimu na wenye thamani kubwa sana katika dunia ya leo na kesho, kwa miaka 15 iliyopita tulikuwa na mpango wa MSDs ambao ulishughulikia changamoto ambazo zinawakabili watoto na sasa kuna mpango wa SDGs ambao tumekusudia ufanye mageuzi makubwa kwa maendeleo ya baadae ya binadamu wakiwepo watoto, na Tanzania kama mwanachama wa UN ina wajibu wa kuhakikisha inafanikisha hilo," alisema Rodriguez. 
Rais wa pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi akitoa pongezi kwa UNICEF kwa kazi ambazo wanafanya za kuwasaidia watoto ili waishi katika mazingira bora.

Nae mgeni wa heshima katika maadhimisho hayo, Rais wa pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi aliipongeza UNICEF kwa kufikisha miaka 70 na kusema kuwa "Nilihusika kukubali UNICEF kufanya kazi nchini na leo sijuitii hilo kwa kazi ambayo mnaifanya, niwatie moyo muendelee na kufanya kazi kwa kuwasaidia watoto." 
Baadhi ya watu waliohudhuria sherehe za maadhimisho ya miaka 70 ya kuanzishwa shirika la UNICEF.

No comments: