Viongozi wa Kitaifa wakijumuika pamoja na Waumini wa Dini ya Kiislamu kwenye Mlango wa Nne wa Barzanji wenye kisimamo cha kumtukuza Mtume Muhammad {SAW}.
Baadhi ya Waumini wa Dini ya Kiislamu wakiendelea na hafla ya Maulidi ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad {saw} hapo Temeke Jijini Dar es salaam
Waislamu wakiwa makini kusikiliza mawaidha na nasaha zilizokuwa zikitolewa na Viongozi wa Dini ya Kiislamu katika Hafla ya Maulidi ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad {SAW} hapo Temeke Jijini Dar es salaam.
Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir Ali akitoa darsa kwa Maelfu ya Waumini wa Dini ya Kiislamu waliohudhuria Maulidi ya Uzawa wa Mtume Muhammad {SAW} hapo Temeke Jijini Dar es salaam.
Makamu wa Rais Mstaafu wa Tanzania Dr. Moh’d Gharib Bilal akitoa salamu kwenye Maulidi ya Mtume Muhammad { SAW }yaliyoffanyika kwenye Msikiti wa Ijumaa wa Majmuati Islamia Temeke Mjini Dar es salaam.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza katika hafla ya Maulidi ya uzawa wa Mtume Muhammad {SAW } yaliyoandaliwa na Uongozi wa Msikiti wa Ijumaa wa Majmuati Islamia Temeke Mjini Dar es salaam. Picha na – OMPR – ZNZ.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema misikiti endapo itatumika kwa mujibu wa maelekezo ya Kiongozi wa Dini ya Kiislamu Duniani Mtume Muhammad { SAW } itaendelea kuwa kimbilio la waumini wote wa Dini hiyo.
Alisema tabia ya baadhi ya Waumini wa Dini hiyo kuifanya Misikiti kuwa majukwaa ya Kisiasa ndio sababu inayopelekea mifarakano katika Jamii makiwemo matatizo ya kugombea Uongozi wa Misikiti.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo katika hafla ya Maulidi ya uzawa wa Mtume Muhammad { SAW } yaliyoandaliwa na Uongozi wa Msikiti wa Ijumaa wa Majmuati Islamia Temeke Mjini Dar es salaam. Balozi Seif alisema Waumini na Wananchi wanapaswa kujitahidi kuitumia Misikiti mbali ya kusali lakini pia inaweza kufanywa mwahala mwa mipango ya maisha, sehemu ya kutoa Tiba, sadaka pamoja na michezo
inayokubalika Kidini.
Alisema Jamii inaendelea kushuhudia ufinyu mdogo wa matumizi yasiyo sahihi kama matumizi ya dawa za kulevya, udhalilishaji wa watoto wadogo, Wanawake pamoja na ujambazi.
Balozi Seif alifahamisha kwamba kuporomoka kwa maadili hasa kwa Vijana kwa kiasi kikubwa kunatokana na kukosa fursa za kujifunza kupitia Misikiti ndani ya muongozo wa Kiongozi wa Dini ya Kiislamu Mtume Muhammad { SAW }.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameushukuru na kuupongeza Uongozi wa Msikiti wa Ijumaa wa Majmuat Islamia pamoja ya Bodi ya wadhamini ya Msikiti huo kwa kazi kubwa inayoshuhudiwa na Jamii ya muendelezo wa ujenzi wa Majengo ya Skuli ya Temeke Islamia inayolenga kuwafinyanga watoto katika msingi wa maadili.
Balozi Seif alisema huo ni mfano mzuri ulioonyeshwa na Uongozi wa Msikiti wa Majumuat Islamia ambao unastahiki kujigwa na masikiti mengine hapa nchini Mijini na Vijijini.
Mapema Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir Ali alisema hafla za maulidi ya Uzawa wa Mtume Muhammad {SAW} ni fursa ya dhahabu kwa waumini wa Dini hiyo kumtukuza Kiongozi huyo.
Sheikh Zubeir alisema inasikitisha kuona fursa kama hiyo ikiwa miongoni mwa mwingi zilizopo kwa ajili ya kutekelezwa na Waumini hao lakini wapo baadhi ya watu wanaopiga vita hafla hizo.
Alisema maendeleo yoyote ikiwemo yale ya Kiibada yanapatikana pale penye ushirikiano na Umoja na mfarakano ni ugonjwa unaostahiki kuepukwa na Waislamu kwa vile unasababisha kuhasibiana na kubughudhiana.
Alitahadharisha kwamba Waumini wa Dini ya Kiislamu iwapo hawatakubali kubadilika Uislamu utaendelea kubakia Vijiweni.
Akigusia suala la Elimu Mufti Mkuu wa Tanzania alieleza kwamba Uislamu na Elimu na mambo pacha yanayomuwezesha Mwanaadamu kupiga hatua kubwa ya Maendeleo.
Sheikh Zubeir alimtolea Mfano Mwanafalsafa wa Kiislamu Firdas aliyefanya kazi kubwa ya kufanya utafiti uliopelekea wataalamu wa Dunia kuitumia anga kwa harakati za usafiri wa Anga.
Akitoa salamu katika Hafla hiyo ya Maulidi ya Uzawa wa Mytume Muhammad {SAW} Makamu wa Rais Mstaafu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.
Moh’d Gharib Bilal alisema mikusanyiko ya Waumini ni Drsa
linalowasaidia washiriki husika kuwa na upeo zaidi wa ufahamu wa Dini
yao. Dr. Bilal aliupongeza Uongozi wa Msikiti Majmuati Islamia chini ya Imamu Mkuu wake Sheikh Alhad Mussa Salum ambae pia ni Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Da es salaam kwa fikra zao za kuandaa mkusanyiko huo wa kheir
unaoongeza upendo, mahaba na kujuana miongoni mwa Waislamu mbali mbali.
Maulidi ya Uzawa wa Mtume Muhammad {SAW} yaliyoandaliwa na Uongozi wa Msikiti wa Ijumaa wa Majmuati Islamia yameshirikisha Waumini wa
Madhehebu tofauti wa Tanzania, Kenya na Wawakilishi wa Balozi na Taasisi za Kimataifa zilizopo Nchini Tanzania.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
28/1/2017.
No comments:
Post a Comment