ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, January 26, 2017

MAZAO YATAONGEZWA THAMANI KABLA YA KUUZWA NJE YA NCHI-MAJALIWA

 Waziri Mkuu, Kassim Majliwa akifurahia ngoma ya Limdoya iliyochezwa na wasanii kutoka kijiji cha Kanitelele wilayani njombe wakati alipohutubia mkutano wa hadhata kayika uwanja wa michezo wa Lupembe mkoani Mjombe Januari 25, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama  chai   katika shamba la wananchi wa kijiji  cha Lwangu , Njombe akiwa katika ziara ya mkoa huo Januari 25, 2017.Kulia ni Meneja wa Kampuni a kutoa huduma kwa wakulima wadogo wa Njombe  (NOSC),Bw.Filbert Kavia.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Askofu   Alfred Maruma wa jimbo Katoliki la Njombe,  wakati alipotembelea shamba ya chai ya wakulima wa kijiji cha Lwangu, Njombe Januari 25, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imejipanga katika kuhakikisha inaongeza thamani ya mazao yake kabla ya kuyauza nje ya nchi.

Amesema kwa muda mrefu Serikali ilikuwa inapata hasara kwa kusafirisha malighafi nje nchi lakini kwa sasa inajenga viwanda ili iweze kuuza bidhaa.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumatano, Januari 25, 2017) wakati alikizungumza na wakulima wa chai katika kijiji cha Lwangu wilayani Njombe.

“Miaka mingi Serikali imekuwa ikipata hasara kwa kuuza mazao nje ya nchi, tumeamua kujenga viwanda vitakavyoweza kuyachakata na kuuza bidhaa badala ya malighafi,”.

“Ujenzi wa viwanda ni moja kati ya mikakati dhati ya Serikali ya kuhakikisha mazao  mnayolima yanakuwa na thamani kubwa  hivyo kuwaongezea tija,” alisema.

Kutokana na mkakati huo Waziri Mkuu amewataka wananchi kuongeza juhudi katika kilimo. “Kuna anayetaka hela hapa? Kama mnataka mali mtazipata shambani. Limeni,”.

Waziri Mkuu alisema mazao hayo ndiyo yatakayoweza kuleta tija kwa wakulima, hivyo aliwashauri waendelee kushirikiana katika vikundi ili wapate misaada ya kitaalam kwa urahisi.

Aidha, alimuagiza mkuu wa wilaya hiyo, Ruth Msafiri na Maafisa kilimo kuwatembelea wakulima hao kwa lengo la kuwaelekeza namna bora ya kuendeleza mazao yao.

Waziri Mkuu alisema hatua hiyo itawawezesha wakulima kupata mbinu bora za kilimo na hatimaye kuvuna mazao mengi yenye viwango vya ubora vinavyotakiwa kimataifa.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu aliiagiza halmashauri ya wilaya ya Njombe kuwaunga mkono wakulima hao kwa kuimarisha barabara zinazoingia kwenye mashamba yao.

“Tuwaunge wakulima wetu kwa kuwaimarishia miundombinu ya barabara ili kuwawezesha kupeleka chai yao kiwandani kwa gharama nafuu,” alisema.

Naye Mbunge wa jimbo la Lupembe Mheshimiwa Joram Hongoli alisema kilimo cha chai ndio mkombozi kwa wananchi hao, hivyo aliwaomba waongeze juhudi.

Awali Meneja Mkuu wa Kampuni ya Kutoa Huduma kwa Wakulima Wadogo Njombe (NOSC), Bw. Filber Kavia alisema kampuni inatoa huduma za kitaalam  kwa wakulima.

Alisema wanalenga kuendeleza kilimo cha chai kwa kuongeza kuongeza uzalishaji kwa hao kutoka kilo 500 hadi kilo 2,000 za majani makavu ya chai kwa hekta kwa mwaka.

Meneja huyo alisema kampuni inakusudia kuongeza mashamba mapya ya chai hadi kufikia hekta 3,800 kutoka hekta 614 ifikapo mwaka 2025.

Bw, Kavia alisema huduma nyingine inayotolewa na kampuni hiyo ni utoaji wa mikopo nafuu ya pembejeo bila ya riba na mkulima hulipa muda mrefu kupitia mauzo ya chai.

Pia kampuni hiyo inatoa huduma ya usimamizi wa mashamba makubwa ya chai ya vijiji na watu binafsi kwa mkataba maalumu ili kuongeza uzalishaji na tija.

Awali Waziri Mkuu alikagua eneo litakalojengwa kiwanda cha kisasa cha kuchakata chai cha kampuni ya Unilever.

      
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMIS, JANUARI 26, 2017.

No comments: