PRESS RELEASE
VIKUNDI VITATU VYA MUZIKI WA REGGAE KUTUMBUIZA TAMASHA LA 14 LA SAUTI ZA BUSARA
Ushiriki wa wasanii watatu wa muziki aina ya Reggae na bendi zao kwenye tamasha la 14 la Sauti za Busara lenye kauli mbiu #AfricaUnited unaashiria kuwa ni wakati muafaka kwa wadau wa muziki Tanzania kuutazama muziki wa Reggae kwa jicho la pili.
Kupitia jukwaa la Sauti za Busara muziki wa Reggae umepewa uzito mkubwa kwa kuwa hubeba ujumbe mzito wa umoja, amani, upendo pamoja na kuibua mabaya yote yanayoendelea kwa jamii husika.
Kupitia nafasi hizo tatu zilizotolewa na uongozi wa Sauti za Busara ni changamoto kwa wanamuziki chipukizi na mameneja wa muziki kuwekeza kwenye muziki wa Reggae Tanzania kama ilivyo kwa aina nyingine ya muziki.Vikundi hivi ni miongoni mwa vikundi 40 vya muziki vitakavyotumbuiza ni pamoja na Rocky Dawuni kutoka Ghana, Sami Dan na Zewd band kutoka Ethiopia na Bob Magharib kutoka Morocco.
Mkurugenzi wa tamasha Yusuf Mahmoud amesema, “wasanii hawa watatu wa Reggae wanawakilisha vema muziki wa Reggae kwa bara la Afrika. Tuna hakika kuwa Watanzania wengi wanapenda Reggae si kwa midundo yake tu bali ni pamoja na ujumbe wa matumaini kwa wote wanaopigania haki na uhuru,”.
Bob Maghrib ni kundi lililozinduliwa mwaka 2011 lenye muunganiko wa wanamuziki wanaowakilisha tasnia ya muziki Morocco. Kundi hili pia linamuenzi mwanamuziki maarufu wa Reggae Bob Marley.
Sami Dan ana taaluma ya uhandisi mwenye shauku na muziki. Harakati zake za kimuziki zilianza kwa kuandika nyimbo na kufanya kazi kwenye bendi akiwa kidato cha tano na sita.
Mwaka 2014, Sami Dan aliunda bendi ya Zewd nyimbo zake kama ‘Fikir Selam’ au ‘Love, Peace’ huburudisha mashabiki wake kwa ujumbe wa amani na umoja.
Tamasha la Sauti za Busara lilitajwa na CNN kuwa ni kati ya matamasha 7 ya muziki Afrika ya kutazamwa litafanyika tarehe 9-12 February Ngome Kongwe Zanzibar.
Kwa mawasiliano zaidi: busaramusic.org
No comments:
Post a Comment