Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema Serikali imeanza kupitia zabuni ili kumpata mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge) kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro, umbali wa kilomita 200.
Amesema treni zitakazopita katika reli hiyo zitatumia mafuta na umeme na mradi huo utasaidia pia kupunguza msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam.
Sambamba na mradi huo, amesema Serikali itajenga barabara ya haraka ya njia sita, (Express Road) kutoka Dar es Salaam hadi Chalinze.
“... Hatua zote zimekamilika na kilichobaki ni mazungumzo na makandarasi kabla ya kuanza kujenga,” alisema Rais Magufuli.
Akizungumza wakati akizindua rasmi mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT), Rais Magufuli alibainisha miradi mbalimbali ya miundombinu itakayorahisisha utoaji wa huduma ya usafiri katika jiji la Dar es Salaam na nchi kwa ujumla.
Makamu wa Rais wa WB (Afrika), Makhtar Diop alisema mradi wa BRT ni muhimu kwa uchumi wa Taifa kwa sababu unachochea maendeleo ya sekta nyingine.
Alisisitiza kuwa WB itaendelea kufadhili miradi mbalimbali ya ujenzi wa miundombinu.
Alisema miaka 25 ijayo, Dar es Salaam itakuwa na watu Zaidi ya milioni 10, hivyo ni muhimu kuandaa mazingira bora ya miundombinu ambayo itaweza kutoa huduma kwa wananchi hao bila usumbufu.
“Huu ndiyo mradi wa mabadiliko, umebadilisha uhalisia wa nchi hii. Tuko tayari kudhamini awamu zitakazofuata za mradi wa BRT na miradi mingine ya ujenzi wa miundombinu kote Tanzania,” alisema Diop.
Mkopo zaidi
Katika hatua nyingine, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema bajeti ya mwaka 2017/2018 inategemea mkopo wa Dola za Marekani 785 milioni sawa na Sh1.7 trilioni kutoka Benki ya Dunia ili kukamilisha utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Aliitaja miradi inayotarajiwa kutekelezwa kupitia fedha hizo kuwa ni awamu ya pili ya mradi wa BRT, upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam, ujenzi wa barabara ya juu katika makutano yaliyopo Ubungo, elimu, menejimenti ya bajeti, maboresho ya mazingira ya biashara na maji.
“Benki ya Dunia imekuwa mdau muhimu wa maendeleo katika nchi yetu, imekuwa ikitukopesha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali, kwa sasa ipo miradi inayotekelezwa na mingine ipo katika hatua ya mazungumzo.
“Kuna mingine tayari wamekubali kutukopesa ukiwamo wa upanuzi wa Bandari. Watatoa Dola za Marekani 305 milioni (Sh671 bilioni) kwa ajili ya awamu ya kwanza,” alisema Dk Mpango.
Alisema awali Serikali iliomba mkopo wa Dola za Marekani 600 milioni sawa na Sh1.2 trilioni kutoka benki hiyo kwa ajili ya utekelezaji wa mradi mzima na imekubali kutoa Sh671 bilioni kwa ajili ya awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo.
Miradi mingine ni awamu ya pili kati ya sita wa mabasi yaendayo haraka ambao utagharimu Dola 403 milioni (Sh886.6 bilioni), elimu Sh220 bilioni, menejimenti ya bajeti na uwazi Sh176 bilioni, maboresho ya mazingira ya biashara Sh176 bilioni na mradi wa maji Dar Sh220 bilioni.
Umeme
Aidha, Dk Mpango alisema anatarajia kuunda kamati ya kushughulikia masuala ya umeme kwa sababu Tanzania ya viwanda haiwezi kujengwa bila nishati ya uhakika na ya bei nafuu.
“Itaundwa kamati ya pamoja ili kushughulikia masuala ya Tanesco ili shirika hilo liweze kujiendesha na kuliepusha na hasara za kila mwaka, ikiwa ni mkakati wa kufanikisha azma ya Tanzania ya viwanda,” alisema Mpango.
1 comment:
KWA UMEME WA MGAO?SERIOUSLY?
Post a Comment