ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, January 28, 2017

MENEJIMENTI YA TAZAMA WATAKIWA KUWA WABUNIFU

 Waziri wa Nishati wa Zambia, Mabumba David (kulia) akizungumza wakati wa mkutano na wafanyakazi wa Kituo TAZAMA cha Jijini Ndola, Zambia. Kushoto ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa tatu kutoka kulia) na Waziri wa Nishati wa Zambia, Mabumba David (wa tatu kutoka kushoto) na ujumbe wao wakitembelea miundombinu ya Bomba la Kusafirisha Mafuta la TAZAMA.
 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) na Waziri wa Nishati wa Zambia Mabumba David (nyuma) wakisalimiana na wafanyakazi wa Kituo cha Kusukuma Mafuta (pumping station) cha Kalonje kilichopo wilaya ya Mpika, nchini Zambia.
 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akielekeza jambo wakati wa ziara ya kutembelea Vituo vya Kusukuma Mafuta vya Tazama (Pumping stations) nchini Zambia. Kulia ni Waziri wa Nishati wa Zambia Mabumba David na Katikati ni Mkurugenzi Mtendaji wa TAZAMA, Davison Thawethe.
 Baadhi ya wafanyakazi wa TAZAMA Kituo cha Kupokelea Mafuta Ghafi cha Ndola, nchini Zambia wakiwasikiliza Mawaziri wa Nishati wa Tanzania na Zambia (hawapo pichani).
Mita za kupokelea Mafuta Ghafi za Kituo cha Tazama- Ndola, Nchini Zambia.

Menejimenti ya Kampuni ya Kusafirisha Mafuta Ghafi ya TAZAMA imeagizwa kuhakikisha inabadilisha uendeshaji wake na kuwa wa kisasa zaidi ili kuwa na uzalishaji wenye tija kumudu ushindani wa soko na kufikia malengo yanayokusudiwa. 

Wito huo umetolewa jana kwa nyakati tofauti na Mawaziri wa Nishati wa Tanzania na Zambia, Profesa Sospeter Muhongo (Tanzania) na Mabumba David (Zambia) walipokuwa wakizungumza na wafanyakazi wa Vituo vya Kusukuma Mafuta (Pumping Stations) vilivyopo nchini Zambia wakati wa ziara ya kutembelea vituo hivyo.

Waziri Muhongo alisema ili kuwa na uzalishaji wenye tija, ni jukumu la kila mfanyakazi kuhakikisha anaondokana na fikra za kizamani na badala yake awe na ubunifu na mipango mipya ya kuendeleza kampuni.

“Mnapaswa kutumia rasilimali zilizopo kwa umakini; kuweni wabunifu ili kuongeza ufanisi; shughuli zenu ziwe zenye tija ili muweze kushindana kwenye soko,” alisema Waziri Muhongo.

Alisema teknolojia kila siku inabadilika kwani wakati Bomba hilo linaanza kazi Mwaka 1968 na sasa ni tofauti hivyo aliwataka kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia ili kuweza kuongeza uzalishaji na kumudu ushindani wa soko.

Naye Waziri David aliwaeleza wafanyakazi hao kuwa, Serikali zote mbili zimewaamini na ndio maana wamepewa kuendesha kampuni hiyo hivyo aliwaasa kufanya kazi kwa kujiamini na kujituma ili kuleta tija.

David alisema hapo awali ilikuwa ni TAZAMA pekee yenye kuhusika na sekta ya Mafuta nchini Zambia lakini kwa sasa jambo hilo limebadilika tayari kuna ushindani wa soko kwenye sekta hiyo hivyo ni vyema Menejimenti hiyo ikatambua hilo na kubadilisha mtazamo na utendaji wake.

Aliongeza kuwa jitihada za makusudi zinapaswa kuchukuliwa na Menejimenti hiyo ili kuondokana na matumizi yasiyo ya lazima kwa lengo la kupunguza gharama za uendeshaji na kuweza kuuza kwa bei ya soko.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TAZAMA, Davison Thawethe alipongeza jitihada za Serikali hizo za kuhakikisha TAZAMA inabadilika na kuwa ya kisasa zaidi.

Aidha, aliahidi kuhakikisha suala la mabadiliko linapewa kupaumbele ili kwenda na kasi inayotakiwa pamoja na kupunguza matumizi yasio ya lazima. 

No comments: