Wednesday, January 25, 2017

Trump kuwazuia wahamiaji kuingia Marekani

Donald Trump
Rais wa Marekani Donald Trump anatarajiwa kutia saini amri kuu kuweka masharti kuhusu wahamiaji wanaoingia nchini humo.

Taarifa kutoka Marekani zinasema ataanza kwa hatua ya kuimarisha usalama katika mpaka wa nchi hiyo na Mexico atakapozuru makao makuu ya wizara ya usalama wa ndani baadaye Jumatano.

Aidha, anatarajiwa pia kutoa tangazo la kuidhinisha sheria kali zaidi za kupata visa kwa wageni kutoka eneo la Mashariki ya Kati na Afrika ambayo yana Waislamu wengi.

Miongoni mwa nchi zitakazoathiriwa na agizo la Trump ni Syria, Yemen, na Iraq.

Bw Trump ameandika kwenye Twitter kwamba leo itakuwa siku muhimu sana kwa usalama wa taifa la Marekani.

Mwandishi wa BBC David Willis kutoka Washington anasema hatua hiyo huenda ikayaudhi mashirika ya kibinadamu na yale ya kutoa misaada ikizingatiwa mzozo unaoendelea kwa sasa kuhusu hali ya wakimbizi wa Syria.
Watakaoumia na watakaofaidi chini ya Trump Marekani
Melania Trump kuchelewa kuingia White House


Wakati wa kampeni yake ya urais, Donald Trump aliahidi kufanyia mageuzi suala la uhamiaji Marekani.

Aligusia ujenzi wa ukuta kati ya Mexico na Marekani kuzuia wahamiaji haramu na kuwapiga marufuku Waislamu kuingia katika taifa hilo kama sehemu ya vita dhidi ya ugaidi. Baadaye alibadili msimamo kidogo na kufafanua kwamba watakachofanyiwa Waislamu ni kufanyiwa ukaguzi mkali kabla ya kuruhusiwa kuingia Marekani.Haki miliki ya pichaTWITTER

Anatarajiwa kufika katika wizara ya usalama wa ndani baadaye leo na anatarajiwa kusaini maagizo hayo ya kuimarisha usalama katika mpaka wa Mexico na taifa lake na baadaye wiki hiii taarifa zinaashiria atawajibikia ahadi yake ya kupunguza idadi ya wakimbizi wanaoingia Marekani.

Na hiyo ni hadi pale ukaguzi mkali utakapoanzishwa na kuzuia raia wa mataifa saba ya Afrika na kutoka eneo la Mashariki ya Kati yote yalio na idadi kubwa ya waumini wa Kiislamu.

Ubaguzi wa kidini unapigwa marufuku kwa mujibu wa katiba ya Marekani lakini inadhaniwa utawala wa Trump utaidhinisha marufuku hiyo kwa misingi kwamba ni hatua za dharura kukabiliana na tishio lililopo la ugaidi.
Trump ayabana mashirika ya utoaji mimba
Trump: Mexico watalipia ukuta '100%'


Awali, Bw Trump aliandika kwenye Twitter kueleza kusikitishwa kwake na kiwango cha juu cha ghasia na mauaji katika jiji la Chicago.

Vyombo vya habari wiki hii viliripoti kwamba tayari watu 228 wamepigwa risasi na wengine zaidi ya 40 kuuawa mwaka huu.

Bw Trump ameandika kwamba iwapo watawala wa Chicago hawatatua tatizo hilo la mauaji, basi atawatuma 'Feds' akimaanisha maafisa wa FBI.

BBC

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake