ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, June 17, 2017

DK. KAFUMU ASHAURIWA AJIUZULU

Na ABDALLAH AMIRI,

SUALA la usafirishaji mchanga wa madini (makanikia) limeshika kasi baada ya wananchi wa Igunga kumshauri Mbunge wa Jimbo lao, Dk. Peter Kafumu kujiuzulu.

Wamedai alishindwa kutumia madaraka yake vizuri wakati akiwa Kamishna wa Madini.

Baadhi ya wananchi wa jimbo hilo walisema baada ya kusikiliza taarifa zote mbili zikiwasilisha kwa Rais John Magufuli, wameona ni vema kumshauri mbunge huyo kuachia ngazi ili kuonyesha uwajibikaji.

Oscar Thomas alisema akiwa mmoja wa wapiga kura, ameona ni vema mbunge wao akajiuzulu kwa kuwa yeye ni miongoni mwa viongozi wanaotuhumiwa kuilingizia taifa hasara kwa kushiriki kutengeneza mikataba mibovu ya madini.

Thomas alisema kazi anayofanya Rais Magufuli ya kufuatilia rasilimali za nchini anapaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania mwenye uchungu na taifa hili.

Mwenyekiti wa Wazee wa Wilaya Igunga, Kassim Ally, alimuomba Rais Magufuli kutokatishwa tamaa na baadhi ya viongozi wasiokuwa waaminifu.

Alisema wazee wako nyuma yake kwa kumpa ushirikiano huku akimtaka mbunge wake kujitafakari zaidi.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Igunga, Costa Ollomi na Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Mwanamvua Killo wamesema kazi anayoifanya Rais Magufuli imeleta heshima ndani ya chama na serikali.

Kuhusu wananchi kumtaka mbunge wao kujiuzulu ubunge alisema yeye hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa tayari Rais alikwisha kutoa maelekezo.

HABARI LEO

No comments: