ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, June 17, 2017

TRUMP AKIRI KWAMBA ANACHUNGUZWA MAREKANI

Donald Trump
Rais wa Marekani Trump amethibitisha kwamba anachunguzwa yeye binafsi kutokana na hatua yake ya kumfuta kazi mkuu wa Shirika la Uchunguzi wa Jinai la Marekani FBI James Comey.

Kupitia Twitter, Bw Trump amekariri kwamba uchunguzi unaoongozwa na mwendesha mashtaka maalum kuhusu tuhuma kwamba maafisa wa Urusi waliingilia uchaguzi wa mwaka 2016 ili kumfaa Trump hauna msingi.

Ni mara ya kwanza kwa Bw Trump kuzungumzia taarifa kwenye magazeti kwamba anachunguzwa kwa tuhuma za kuhujumu mifumo ya haki kwa kumfuta kazi Bw Comey.

Awali, taarifa kwenye vyombo vya habari Marekani vilikuwa vimeripoti kwamba wasaidizi wake pamoja na watu waliojitolea kusaidia katika kundi lake la mpito wameamrishwa kuhifadhi nyaraka zote kuhusiana na uchunguzi huo wa madai kuhusu Urusi.

Taarifa zinasema mawakili wa maafisa hao wa Trump wametakiwa kuhifadhi nyaraka zote zinazohusiana na Urusi, Ukraine na washauri wengine kadha wa kampeni.

Kuna makundi kadha yanayofanya uchunguzi, kundi moja likiongozwa na mkurugenzi wa zamani wa FBI Robert Mueller, ambayo yanachunguza iwapo maafisa wa Trump walishirikiana na maafisa wa Urusi wakati wa kampeni.

Bw Trump amekana tuhuma hizo.

BBC

No comments: