ANGALIA LIVE NEWS

Friday, June 16, 2017

UWT Zanzibar yawataka wanawake kuchangamkia fursa za Uongozi

 Kaimu  Naibu  Mkuu wa UWT Zanzibar, Bi. Tunu Juma Kondo akizungumza na viongozi wa Matawi ya Jimbo Kijini Wilaya ya Kaskazini “A” kichama Unguja.
  Katibu Msaidizi wa  Idara ya  Organazesheni  UWT Zanzibar, Bi. Mgeni  Ottow akitoa nasaha kwa viongozi wa Matawi ya Jimbo Kijini Wilaya ya Kaskazini “A” kichama Unguja.
Baadhi ya viongozi wa UWT  wa Matawi jimbo la kijini Wilaya ya Kaskazini “A”  kichama Unguja wakisikiliza kwa makini nasaha zinazotolewa na viongozi wa UWT Zanzibar  uko Tawi la CCM Muange.

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
UMOJA wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi  Tanzania (UWT)  umewataka wanawake kuchangamkia fursa za Uongozi wa ngazi mbali mbali  kupitia uchaguzi unaondelea hivi sasa ndani ya Chama na jumuiya zake.

Wito huo umetolewa Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja huo Zanzibar  Bi.Tunu Juma Kondo    katika mwendelezo wa ziara ya  UWT  ya kuzungumza na Viongozi wapya wa ngazi za matawi wa umoja huo uko Jimbo la Kijini  Wilaya ya Kaskazini "A"  kichama Unguja.

Awambia  Akina Mama hao kuwa Uchaguzi  wa ngazi mbali mbali unaoendelea  katika taasisi hiyo ndio fursa moja wapo ya wanawake  kupata nafasi za uongozi ili waweze kufikia malengo ya kupata uwakilishi wa viongozi wenye idadi sawa na wanaume ndani ya Chama hicho.

Alifafanua kuwa wanawake wanatakiwa kuondokana na dhana ya kuendelea  kuongozwa kwa kila nafasi za uongozi ndani ya CCM bali wanatakiwa kujiongeza kwa kuwania wenyewe uongozi ndani ya chama hicho ili kuleta maendeleo endelevu ndani ya chama na jumuiya zake.

Pia alisisitiza viongozi hao kuwa pamoja na majukumu ya kiuongozi waliyonayo ni lazima wawahamasishe  kwa wingi wanawake  kuwania nafasi za uongozi ili kupata viongozi makini na wenye  uwezo  wa kwenda na kasi  za kiutendaji za chama hicho.

"Wanawake wenzangu tutumieni fursa ya Uchaguzi wa Chama kuwania nafasi mbali mbali za uongozi , tusisubiri nafasi za uteuzi  bali tusimame wenyewe  kupambana kwa kuhakikisha nasi tunakuwa na nyadhifa za uongozi kama walivyo wanaume kwani tunaweza wenyewe bila ya kuwezeshwa’’,. Alisema Bi.Tunu.

Akizungumza katika ziara hiyo Katibu Msaidizi Idara ya Organazesheni UWT Zanzibar, Bi. Mgeni Ottow Alisema CCM atadumu madarakani endapo viongozi mbali mbali wanaopatikana kupitia uchaguzi wa chama hicho watakuwa na uzalendo wa kweli katika kulinda maslahi ya taasisi hiyo kwa vitendo.

Bi. Mgeni aliwasihi  Akina Mama wa Umoja huo kuhakikisha wanachagua viongozi waadilifu na wenye uwezo wa kubuni fursa mbali mbali za maendeleo zitakazowanufaisha wanawake wenzao na chama kwa ujumla.

“ Wanawake ndio tegemeo la Chama chetu na jumuiya kwa ujumla hivyo lazima tuwe wa kwanza kujitokeza kwa kila tukio linalohusu uimarishaji wa chama chetu hasa michakato ya uchaguzi na tukiwa wengi katika nafasi za uongozi ndipo tutakapopata nguvu za pamoja kutetea haki zetu na kupinga kisheria udhalilishaji wa Wanawake”,. Aliseleza Bi. Mgeni.

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Kaskazini Unguja, Bi. Miza Ali Kombo amesema zoezi la Uchaguzi kwa ngazi ya Wadi linaendelea vizuri kwani wagombea tayari wamejaza fomu na kinachosubiriwa kwa sasa ni upigaji wa kura ili kupata viongozi watakaoongoza ngazi hiyo kwa miaka mitano.



Naye Katibu wa UWT Tawi la Muange, Bi. Waja Mnadhani Ali  alieleza maratajio yake baada ya kupata nafasi hiyo atafanya kazi za jumuiya na chama kwa umakini na uadilifu ili kuwawakilisha vyema wanawake waliomuamini na kumpa ridhaa ya uongozi huo.

No comments: