ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, July 26, 2017

CUF Maalim yajiandaa kujibu mapigo ya Prof Lipumba


By Waandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. CUF upande wa Maalim Seif Sharif Hamad umesema utaitisha Baraza Kuu la uongozi la Taifa ili kujibu mapigo ya Profesa Ibrahim Lipumba.

Pia, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amesema suala hilo litapata majibu baada ya kujadiliwa.

Juzi, Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Lipumba aliwafukuza uanachama wabunge wanane na madiwani wawili wa chama hicho kwa madai ya kukihujumu chama hicho.

Wabunge waliofukuzwa uanachama ni Riziki Ngwali, Severina Mwijage, Raisa Abdallah, Saumu Sakala, Salma Mwasa, Miza Bakari, Halima Mohamed, Khadija El Khasim na madiwani ni Leila Hussein na Elizabeth Magwaja ambao wote wamevuliwa uanachama kuanzia Julai 23.

Naibu Katibu wa CUF- Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alisema wamepata taarifa za uamuzi wa baraza kuu hilo na kwamba wataitisha la kwao ili kujibu mapigo.

Mazrui alisema kabla ya kuitisha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, kikao cha kamati ya Utendaji kitakutana kwa ajili ya kujadili suala hilo kwa kina na kuwataka wanachama wa CUF kuwa wavumilivu.

“Tutaitisha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa halali kujadili haya yaliyofanywa na upande Profesa Lipumba. Hapa ninavyoongea na wewe ninaongoza kikao cha maandalizi kuhusiana na kamati ya utendaji na baraza kuu.

“Baraza Kuu la Uongozi la Taifa halali, litatoa uamuzi nini way forwad (mwelekeo) wa uamuzi uliofanywa na hawa watu ambao wengine tuliwasimamisha uanachama,” alisema Mazrui ambaye ni mmoja kati ya viongozi watakaoitwa kwa ajili ya mahojiano kwa tuhumu za kukihujumu chama hicho kwa mujibu wa Profesa Lipumba.

Akizungumzia mgogoro huo mpya, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi alisema utatolewa maelezo mara baada ya kujadiliwa na ofisi yake.

Kuhusu hatua hiyo, mmoja wa wabunge waliofukuzwa uanachama, Khadija Salum alisema anasubiri maelekezo kutoka kwa kiongozi wa chama chake, Maalim Seif ambaye ni katibu mkuu wa CUF kwa sababu katiba haimtambui Profesa Lipumba.

“Inakuwaje mtu ambaye hata si mwanachama anajitokeza na kukufuta uanachama? Haikubaliki, mimi nitaendelea kufanya wajibu wangu,” alisema.

Mbunge mwingine, Salma Mohamed alisema hautambui uongozi wa Profesa Lipumba.

“Si halali kwa kundi la watu au mtu mmoja kutoa maamuzi wakati kesi ipo mahakamani,” alisema.

Spika atoa neno

Lakini wakati wabunge hao wakisema hawatambui hatua hiyo, Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema amepokea barua ya Profesa Lipumba kuhusu kufukuzwa kwao uanachama.

Katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari jana, Spika amesema suala la kuwaondoa wanachama ni la utashi wa vyama vyenyewe na kila chama kina utaratibu wake.

“Hivyo bado naendelea kuitafakari barua hiyo; na taarifa rasmi kuhusu maamuzi yangu kwa wabunge waliofukuzwa nitaitoa hapo baadaye,” amesema.

Juzi, Profesa Lipumba aliwaeleza wanahabari kwamba uamuzi wa kuwavua uanachama wabunge hao umetokana na maazimio ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, lililokutana juzi kwa lengo la kupokea na kujadili taarifa kutoka kamati ya nidhamu na maadili ya chama hicho.

Profesa Lipumba alidai kwamba wabunge hao wamekuwa wakifanya vitendo mbalimbali kinyume cha Katiba ya CUF ikiwamo kushirikiana na Chadema kukihujumu chama hicho.

Imeandikwa na Bakari Kiango, Fortune Francis na John Namkwahe.

No comments: