ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, July 6, 2017

POLISI WAWASHAMBULIA NA KUWAUA WAHALIFU WAWILI IKWIRIRI.


 Mkuu wa Oparesheni Maalumu za Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Liberatus Sabas (Kushoto) na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Rufiji, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Onesmo Lyanga wakionyesha kwa Waandishi wa habari silaha mbili zilizopatikana baada ya mapambano katika msitu wa Ngomboroni Tarafa ya Ikwiriri  ambapo katika tukio hilo waliuwawa wahalifu wawili wanaojihusisha na mauaji katika wilaya  ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji. (Picha na Frank Geofray-Jeshi la Polisi)

Mkuu wa Oparesheni Maalumu za Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Liberatus Sabas akionyesha kwa Waandishi wa habari silaha mbili aina ya SMG na Shot Gun zilizopatikana baada ya mapambano katika msitu wa Ngomboroni Tarafa ya Ikwiriri  ambapo katika tukio hilo waliuwawa wahalifu wawili wanaojihusisha na mauaji katika wilaya  ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji. Kulia kwake ni Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Rufiji, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Onesmo Lyanga.



Na. Frank Geofray -Jeshi la Polisi.
Jeshi la Polisi nchini limefanikiwa kuwaua wahalifu wawili  ambao ni miongoni mwa wahalifu wanaoendesha mauaji katika  Kanda maalumu ya Polisi Rufiji  kufuatia operesheni kali inayoendelea  katika  Wilaya ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji  mkoani Pwani.

Akielezea tukio hilo,   Mkuu wa Operesheni Maalum  za Jeshi la Polisi,  Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Liberatus Sabas alisema tukio hilo lilitokea siku ya Jumatano Julai 5 majira ya saa nne usiku  katika msitu wa Ngomboroni kata ya Ikwiriri, Wilaya ya Ikwiriri Kanda maalumu ya Rufiji  ambapo askari wa operesheni maalum wakiwa katika doria  za ufuatiliaji wahalifu sugu wanaojihusisha na mauaji yanayoendelea katika Kanda hiyo ya kipolisi.

 Sabas alisema  Askari wakiwa na mtuhumiwa mmoja muhimu anayeshiriki katika mauaji hayo  ambaye alikuwa amekamatwa na baada ya mahojiano alikubali kwenda kuwaonesha Polisi mahali  ambapo ni maficho ya wenzake.

Sabas alieleza kuwa, baada ya kufika  eneo la msitu wa Ngomboroni  kikundi cha watu wanaokadiriwa kufikia watano walikurupuka  kutoka kwenye kichaka na kuanza kukimbia ndipo askari Polisi kwa tahadhari kubwa walianzisha mashambulizi na kufanikiwa kumjeruhi mhalifu mmoja kwa risasi, katika  mashambulizi hayo  mtuhumiwa aliyekuwa mkononi mwa polisi  naye alijaribu kutoroka  na hivyo kupelekea kumjeruhi kwa risasi hivyo idadi yao kufikia wawili.
Majeruhi hao wawili  walifariki dunia njiani wakati wakipelekwa hospitali  kwa matibabu kutokana na kuvuja damu nyingi iliyosababishwa na majeraha ya risasi waliyoyapata. Miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti  Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“Katika tukio hilo tumefanikiwa kupata silaha mbili  aina ya SMG  na shot gun moja pamoja na  risasi tisa za SMG zilizokuwa kwenye Magazine.”  Alisema Sabas.
Aidha,  mkuu huyo  wa Operesheni maalum za Jeshi la Polisi Naibu kamishina Sabas  ameendelea  kuwasisitiza  wananchi kutoa taarifa zitakazowezesha kupatikana kwa wahalifu wengine waliosalia  na kwamba zawadi nono bado ipo pale pale  na itatolewa kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa sahihi kuhusiana na wahalifu  wanaojihusisha na mauaji katika kanda maalumu ya Rufiji.

No comments: