ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, July 22, 2017

SH. BILIONI 1.669 KUTEKELEZA MIRADI YA MAJI ILEJE-MAJALIWA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imetenga sh. bilioni 1.669 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji katika wilaya ya Ileje mkoani Songwe.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Julai 22, 2017) wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Ileje katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Itumba.


Waziri Mkuu amesema kati ya fedha hizo sh. bilioni moja zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji katika miji miwili ya Isongole na Itumba wilayani Ileje.


“Kiasi kingine cha sh. milioni 669 kimetengwa kwa ajili ya maji katika vijiji mbalimbali vya wilaya ya Ileje katika mwaka wa fedha wa 2017/2018.


Hata hivyo, amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa Kampeni ya Rais Dkt. Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani kwa kusogeza huduma ya maji kwa urahisi.


Waziri Mkuu amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi katika maeneo yote nchini wanapata huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400.


Wakati huo huo Waziri Mkuu ameiagiza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Songwe kuhakikisha inaimarisha ulinzi katika maeneo ya mipaka.



Amesema kamati hiyo inatakiwa kuimarisha ulinzi katika maeneo yote ya mipaka ili kuizua wageni kuingia bila ya kufuata taratibu zilizowekwa kisheria.


Awali Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Bw. Joseph Mkude alisema katika kipindi cha Julai 2016 hadi Juni 2017 jumla ya wahamiaji haramu 38 walikamatwa kwenye wilaya hiyo.


Alisema kati ya wahamiaji hao haramu 36 ni raia wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na wawili walikua raia wa Malawi na wote walirudishwa makwao.

No comments: