Kauli ya Rais John Magufuli kuwa ataendelea kuteua wapinzani wenye akili na kuacha vilaza imewachanganya wapinzani, kutojua Rais anafanya siasa ya aina gani.
Rais Magufuli amezungumzia kuendelea kuwateua wapinzani akiwa anahutubia wananchi wa Mkoa wa Tabora katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi baada ya kuzindua miradi ya barabara yenye thamani ya Sh 457.256.
Kauli hiyo inachukuliwa kama mwendelezo wa uteuzi unaofanywa na Rais Magufuli ambapo tayari amemteua muasisi na mshauri wa chama cha ACT Wazalendo, Profesa Kitila Mkumbo kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji na aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Anna Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Akizungumzia kauli ya Rais na uteuzi anaofanya kwa wapinzani Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui amesema kinachofanyika ni kukubali alichokikataa hadharani.
Amesema Rais Magufuli aliwahi kufanya mkutano Pemba na kusema kuwa hawezi kamwe katika Serikali yake kuteua wapinzani, “Inaonyesha wazi aliowateua siyo wapinzani kama ambavyo alisema hawezi kuwateua.”
Mwenyekiti wa NCCR – Mageuzi, James Mbatia amesema hayo yote yanatokana na baadhi ya wapinzani kusahau misingi na mifumo ya uwapo wa vyama vyao.
“Hizi zote ni kelele, hakutakuwa na upinzani wa kweli, siasa za kweli kama hakutakuwa na meza ya majadiliano ili kupata muafaka.
“Atawateua, watafanya wanachoelekezwa na hiyo haitasaidia kwa sababu haitaleta msukumo wa kusonga mbele, hakuna hekima bila ufahamu, ufahamu unatokana na kupata mawazo kinzani badala ya kuyapinga,” amesema kwa kifupi Mbatia.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wakizungumzia kauli ya Rais Magufuli wameeleza kuwateua wapinzani ni kubadili dhana nzima ya vyama hivyo.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), Richard Mbunda amesema uteuzi umebadili dhana nzima ya upinzani kama ulivyowaziba mdomo wabunge wa CCM.
Amesema wabunge wa CCM hawawezi kuikosoa Serikali kwa kuamini kuwa hawatapata nafasi za uteuzi kama uwaziri na unaibu, wapinzani pia wameingia kwenye mkumbo huo na matokeo yake watapotea.
“Nafasi za uteuzi wa kisiasa dunia nzima unachukuliwa kama ajira, hivyo ni ngumu kumkemea aliyekuajiri, wapinzani kupenda, kukubali kuteuliwa wanajiua bila kufahamu,”amesema Mbunda.
No comments:
Post a Comment