Advertisements

Wednesday, July 26, 2017

Wadau watoa angalizo, Acacia kudaiwa kodi ya Sh424 trilioni

By Julius Mnganga na Ephrahim Bahemu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Taarifa za makadirio ya kodiyaliyofanywa na Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa kampuni ya Acacia zisipothibitishwa, zinaweza kuleta mtikisiko kwa wawekezaji wanaotarajia kuja nchini, wadau wamesema.

Licha ya nia njema ya Serikali kutaka Taifa linufaike na rasilimali zake, wadau na wachambuzi wa uchumi, sheria na biashara ya kimataifa wameonyesha hofu kwamba taarifa zaidi zinahitajika ili kutowatisha wawekezaji wengine wanaotamani kuja nchini.

Meneja wa Taasisi ya Usimamizi wa Rasilimali (Natural Resources Governance Institute), Kusini na Mashariki mwa Afrika, Silas Olan’g akizungumzia kodi inayodaiwa Acacia alisema tangu sakata la uchunguzi wa sekta ya madini lianze, jamii haijapata taarifa kamili hivyo kila mmoja kuwa na mtazamo wake.

“Makadirio yaliyotolewa na TRA bila shaka yametokana na uchunguzi wao hivyo Acacia nao wanapaswa kutoa taarifa zao. Hilo likifanyika, kila mdau ataweza kufahamu kama kuna mwenye makosa ama la,” alisema Olan’g.

Alisema hilo lisipofanyika na Serikali ikiendelea kukaa kimya: “Italeta mtikisiko kwa wawekezaji walio nje. Taarifa hizi ni muhimu ili kuwa na mtazamo wa pamoja na kuwaondoa woga. Watakaoridhika kwamba Acacia imekiuka mkataba hawatoogopa kuja kuwekeza.”

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Godfrey Simbeye alisema huenda uamuzi huo umefanywa makusudi ili kuharakisha majadiliano kati ya Serikali na wawekezaji hao.

Alisema TRA imetimiza wajibu wake na ripoti mbili za kamati za uchunguzi zimesaidia kurahisisha tathmini ya kiwango cha kodi ya Acacia ambayo ilitaka kuundwe tume huru, lakini haijafanyika hivyo. “Kiwango cha kodi kilichokadiriwa ni kikubwa sana na huenda siyo halisi. Hakuna kampuni yenye uwezo wa kulipa fedha hizo labda (tajiri wa kwanza wa dunia) Bill Gates,” alisema Simbeye.

Alisema Acacia wanapaswa kuharakisha mazungumzo ambayo huenda yakapunguza kiasi hicho. “Ubaya ni kwamba hata namna ya kukata rufaa kwa Acacia ni ngumu kwa kuwa watatakiwa kulipa sehemu ya kodi hiyo. Uwezo huo pia hawana,” aliongeza.

Alikumbusha kwamba sakata hilo linatafsiriwa vibaya na wawekezaji wa nje kutokana na sifa mbaya zinazoenezwa na kuifanya Tanzania ionekane ina hatari kubwa kisiasa.

Wakati TRA ikiitaka Acacia kulipa kiasi hicho, taarifa za kampuni hiyo zinasema tangu ianze uzalishaji nchini, imeingiza jumla ya Dola bilioni sita ambazo ni sawa na Sh13.2 trilioni kutokana na mauzo ya dhahabu ya Bulyanhulu na Buzwagi, “Si rahisi kwetu kukwepa kodi kubwa kiasi hicho.”

Licha ya mapato hayo, thamani ya kampuni hiyo ni Dola 1.2 bilioni ambazo ni zaidi ya mara 30 ya kodi inayodaiwa (Dola40 bilioni) na zaidi ya mara 150 ya makadirio yote yanayojumuisha kodi, riba na faini (Dola 190 bilioni).

Kuhusu hilo, Profesa wa masuala ya uhasibu na fedha wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Ernest Kitindi alisema mustakabali wa sakata hili utategemea mazungumzo yatakayofanyika baina ya Serikali na Acacia. Juu ya thamani ya kampuni hiyo kuwa ndogo kuliko deni lake, alisema hiyo si hoja ya kuzingatiwa sana kwa kuwa hilo linawezekana kama uongozi wa kampuni unataka kuficha ukweli huo.

“Tunachokifahamu ni hesabu za kampuni hiyo, lakini hatujui kwa muda wote huo, wanahisa wake wamelipwa kiasi gani. Inawezekana fedha iliyokuwa inaingia ilikuwa inaelekezwa kwenye gawio badala ya uwekezaji,” alisema Profesa Kitindi.

Wakati baadhi ya wadau wakiwa na shaka juu ya uwezo wa Acacia kulipa deni hilo, Serikali imepongeza hatua zilizochukuliwa na TRA.

“Utaratibu uliotumiwa na TRA ni sahihi. Kama wanaona kiwango ni kikubwa na hawawezi kulipa, taratibu za kukata rufaa kwa kamishna wa kodi zinaeleweka, wazifuate,” alisema Benny Mwaipaja, ofisa habari wa Wizara ya Fedha.

Hata hivyo, Acacia inalikataa deni hilo kwa maelezo kwamba haijapewa ripoti ya kamati zote mbili ambazo uchunguzi wake umetumika kufanya makadirio hayo. Licha ya kutaka usuluhishi wa kimataifa, bado inaamini majadiliano kati yake na Serikali yanaweza kuleta matokeo mazuri zaidi. Suala linalowapa shaka baadhi ya wachambuzi ni uwezo wa kampuni hiyo yenye thamani ya Dola 1.2 bilioni kulipa deni la Dola 190 bilioni hivyo kusema kuna umuhimu wa kufanyika kwa mazungumzo ili kulipunguza.

Kutokana na umuhimu wake kwa uchumi wa Taifa, Mbunge Vunjo (NCCR Mageuzi), James Mbatia alisema suala hilo linahitaji utulivu kulishughulikia.

“Vita ya uchumi ni kubwa na hii ya kwetu ni kubwa kwelikweli. Silaha pekee tuliyonayo ili kuishinda ni mshikamano na umoja wa kitaifa,” alisema Mbatia. Alifafanua kwamba Serikali inapaswa kuruhusu mawazo mbadala. “Mbatia akiwa na mtazamo tofauti isionekane kama ananunuliwa na upande wa pili, bali iliruhusiwe tafakari makini,” alisisitiza.

Waziri Kivuli wa Fedha na Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee alikumbusha juu ya ahadi ya kufanyika mazungumzo kati ya kampuni ya Barrick Gold; kampuni mama ya Acacia na Serikali ambayo hayana dalili ya kufanyika.

“Ni dhahiri kuna mzozo kati yao. Kila mmoja hakubaliani na mwenzake. Huenda kodi hii imekadiriwa kisiasa. Lakini Serikali na Acacia zinategemeana hivyo mazungumzo hayaepukiki,” alisema.

No comments: