Wakati maandalizi hayo yakiendelea, Kiongozi wa Muungano upinzani (NASA) nchini Kenya, Raila Odinga amewashauri wafuasi wake, kususia kazi leo ikiwa ni njia ya kupinga matokeo ya uchaguzi yanayomtaja Kenyatta kuwa ndiyo rais mteule. Kamati ya maandalizi ya sherehe hizo inayoongozwa na Katibu Kiongozi Joseph Kinyua imebainisha kuwa imeandaa orodha ya majina ya viongozi wa kimataifa kwa ajili ya kushuhudia tukio hilo la uapisho wa Kenyatta endapo ushindi Kenyatta hautopingwa mahakamani.
Kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo, sherehe za uapisho hufanyika siku 14, baada ya mshindi wa uchaguzi kutangazwa ili kutoa fursa kwa chama chochote kinachotaka kupinga matokeo kufanya hivyo. Viongozi wengine wanaotarajiwa kualikwa katika sherehe hizo wakiwemo wakuu wa nchi ni pamoja na Rais wa Rwanda Paul Kagame, Rais wa Uganda Yoweri Museveni, Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma na Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari. Wengine ni Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May.
Aidha, katika orodha hiyo pia yupo Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, mfanyabiashara tajiri namba moja Afrika Aliko Dangote, Kiongozi wa Jumuiya ya Ismailia, Aga Khan, Waziri Mkuu mstaafu wa Italia, Matteo Renzi na Rais Xi Jinping wa China. “Tupo kwenye maandalizi ya sherehe za uapisho wa Rais wakati tukisubiria hatua za kikatiba kukamilika. Orodha hii ni ya marafiki wa Kenyatta, viongozi wa Afrika na viongozi wengine wa kimataifa, tunaotarajia kuwaalika,” alisema mmoja wa wanakamati hiyo ya maandalizi.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi Kenya, Wafula Chebukati mwishoni mwa wiki alimtangaza rasmi Rais Kenyatta na Naibu wake, William Ruto kuwa washindi katika uchaguzi uliofanyika wiki iliyopita nchini humo. Kwa upande mwingine, wakati akihutubia wafuasi wake katika mtaa wa Kibera, jijini Nairobi kwa mara ya kwanza kabisa tangu kutangazwa matokeo, Odinga alidai kuwa serikali ilipanga kuwaua wafuasi wa upinzani kabla ya kutangazwa matokeo.
Alisema vurugu na mauaji yanayoendelea nchini humo, ni matokeo ya serikali ambayo ilitakiwa ishughulikie tatizo la matokeo feki na si kupambana na wananchi. “Tulionya tangu mapema kuwa watachezea na kuiba kura na hiki ndiyo kilichotokea. Bado hatujalimaliza hili na hatutokata tamaa, subiri muone hatua tutakazochukua na nitawatangazia keshokutwa… lakini kwa sasa nawaomba msiende kazini kesho,” alisisitiza Odinga.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment