ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, August 16, 2017

Mbowe aeleza madiwani waliojiuzulu Chadema watakavyoigharimu Serikali

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameeleza jinsi mamilioni ya fedha yatakavyotumika kugharimia uchaguzi mdogo katika kata nane za mikoa ya Arusha na Kilimanjaro kuziba nafasi zilizoachwa wazi na madiwani wa Chadema waliojiuzuru.
Akizungumza katika mikutano tofauti ya hadhara jimboni kwake, Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai, alisema uchaguzi mdogo katika kata moja unatarajia kugharimu Sh250 milioni.
Katika majimbo ya Arusha Mjini na Arumeru Mashariki mkoani Arusha na Hai mkoani Kilimanjaro ambayo yote yako chini ya Chadema, jumla ya madiwani nane walijiuzulu, wakisema wanamuunga mkono Rais John Magufuli.
Endapo makadirio ya Mbowe yatakuwa ni sahihi, kiasi cha Sh2 bilioni kitatumika kufanya uchaguzi mdogo katika kata tatu za jimbo la Hai, nne za jimbo la Arumeru Mashariki na moja ya Arusha.
Alipoulizwa kuhusu gharama hizo, mkurugenzi wa uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC), Kailima Kombwey alisema “huwa sipendi ku-comment wanaposema wanasiasa sababu I’m not a politician (mimi si mwanasiasa)”.
Akizungumza katika mikutano tofauti ya hadhara jimboni kwake kwa siku nane mfululizo, Mbowe alisema matumizi hayo ya mamilioni ya fedha ni mabaya kwa kuwa ni fedha za walipakodi.
Alisema mwaka 2015 wakazi wa Mnadani walimchagua Ernest Kimath kuwa diwani wao, lakini akasema ni jambo la aibu kwamba CCM na viongozi wa serikali wilayani Hai wamerubuni watu.
“Haya ni matumizi mabaya ya fedha za umma kwa sababu gharama za kurudia uchaguzi hapa Kata ya Mnadani pekee ni Sh250 milioni. Hizi zingeweza kwenda kujenga shule na zahanati,” alisema.
“Serikali inaona kuliko kuwe na diwani wa upinzani, bora turudie uchaguzi kwa gharama ya mamilioni. Nataka niwaambie nitalala hapa Shirinjoro tukirudia uchaguzi na haiendi popote,” alisema.
Mbowe alisema sababu zilizotolewa na madiwani hao za kujiuzulu si za kweli, akidai kuwa baadhi ya madiwani hao waliandikiwa barua za kujiuzulu.
Katibu wa Chadema wa Kanda ya Kaskazini, Aman Golugwa amekuwa akisisitiza kuwa madiwani wanaojiuzulu wanafanya hivyo kwa kushawishiwa kifedha na vyeo, madai ambayo wameyakanusha.
Hata hivyo CCM inadai mbinu mpya za kimkakati kulingana na kasi ya dunia na mahitaji ya jamii, ndizo zinazowarudisha katika chama hicho.
Kauli hiyo ilitolewa mwezi uliopita na katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM anayehusika na siasa na uhusiano wa kimataifa, Kanali Ngemela Lubinga wakati akizungumza na wanahabari mjini Moshi.
Kanali Lubinga alisema hata madiwani wa Chadema katika Jimbo la Arumeru waliojiuzulu na kumuunga mkono Rais Magufuli ni kutokana na kuridhishwa na utendaji kazi wa Serikali.
“Hii sasa hivi ni CCM mpya na Tanzania mpya. CCM tulijifanyia tathmini ya miaka 40 na kuona mapungufu na tumeyarekebisha ndani ya CCM na serikalini. Kasi hii inawavutia wengi,” alisema.
“Tumeanzisha mbinu mpya za kimkakati kulingana na hitaji la jamii. Dunia inakwenda spidi na spidi ya dunia inavyokwenda lazima chama tawala kiendane na spidi hiyo na hitaji la jamii,” alisisitiza.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amekaririwa akisema anayo orodha ya viongozi wengi wa upinzani wanaoomba kurudi CCM, lakini aliwataka wasubiri kwanza.
Arusha na Kilimanjaro ni kati ya maeneo ambayo ni ngome kuu ya upinzani, hasa Chadema ambayo imekuwa ikikosa upinzani kutoka vyama vingine.
Mwaka 2015, aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa aliihama CCM na kujiunga na Chadema, akikufuatiwa na madiwani kadhaa kutoka CCM.

Chanzo: Mwananchi

No comments: