Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na viongozi, watalaam,wafugaji na wadau mbalimbali wa uhifadhi katika kikao maalum cha kujadili suala la kuondoa mifugo katika Pori la akiba la Maswa, Ranchi ya MWIBA na Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Makao wilayani Meatu.
Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Dkt. Joseph Chilongani akizungumza na viongozi, watalaam,wafugaji na wadau mbalimbali wa uhifadhi katika kikao maalum cha kujadili suala la kuondoa mifugo katika Pori la akiba la Maswa, Ranchi ya MWIBA na Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Makao wilayani humo.
Baadhi ya viongozi na watalaam wa Mkoa wa Simiyu na Wilaya ya Meatu,wafugaji na wadau mbalimbali wa uhifadhi wakifuatilia hoja mbalimbali zilizokuwa zikijadiliwa katika kikao maalum cha kujadili suala la kuondoa mifugo katika Pori la akiba la Maswa, Ranchi ya MWIBA na Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Makao wilayani Meatu.
Meneja wa Pori la Akiba la Maswa, Lusato Masinde akiwasilisha taarifa yake kwa viongozi na watalaam wa Mkoa wa Simiyu na Wilaya ya Meatu,wafugaji na wadau mbalimbali wa uhifadhi katika kikao maalum cha kujadili suala la kuondoa mifugo katika Pori la akiba la Maswa, Ranchi ya MWIBA na Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Makao wilayani Meatu.
Na Stella Kalinga, Simiyu
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka ameitaka Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Meatu mkoani humo, ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo,Dkt. Joseph Chilongani kutekeleza kwa weledi, uadilifu na haki zoezi la kuondoa mifugo kwenye maeneo ya hifadhi litakaloanza September 04, 2017.
Mtaka ametoa kauli hiyo mara baada ya viongozi wa Serikali na Chama Mkoa na Wilaya, Wataalam, wafugaji na wadau wa uhifadhi na Utalii kukutana na kujadili suala la uondoaji mifugo katika Maeneo ya Hifadhi, yakiwemo ya Pori la Akiba la Maswa, Ranchi ya MWIBA na Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) Makao wilayani Meatu.
“Mkafanye zoezi hili kwa weledi mkubwa na haki, lisije likawa zoezi la kuwaonea watu, kufanya utapeli kwa kujifanya mnachukua ng’ombe kwa ajili ya kutaifisha halafu mkagawana; viongozi na wote mtakaohusika mkalisimamie kwa makini sana suala hili” alisisitiza Mtaka
Mkuu wa Wilaya ya Meatu Mhe.Joseph Chilongani amesema baada ya makubaliano yaliyofikiwa kati ya viongozi, wafugaji na wadau wa uhifadhi na utalii ametoa muda wa siku nne na kufikia Septemba 04 mwaka huu, wafugaji wawe wametoa mifugo katika maeneo ya hifadhi kwa hiari.
Dkt.Chilongani amebainisha kuwa Viongozi wa Wilaya ya Meatu walikutana na wafugaji katika maeneo yao na kuwatahadhalisha juu ya uingizwaji wa mifugo kwenye maeneo ya hifadhi, ili kuwasaidia waepuke adhabu ya kifungo na mifugo yao kutaifishwa kwa kuwa kuingiza mifugo hifadhini ni makosa kwa mujibu wa sheria.
“Maandalizi yote yako tayari, timu za kutekeleza zoezi hili zote zipo, nitoe muda wa siku hizi zilizobaki ili kufikia Jumatatu ya tarehe 04 zoezi la kuondoa mifugo kwenye Pori la Akiba la Maswa, Ranchi ya MWIBA na WMA ya Makao lianze, tulishawapa wafugaji muda wa kutosha tulipokuwa tukipita kwenye vijiji kuzungumza nao juu ya madhara ya kuingiza mifugo hifadhini” amesema.
Kwa upande wake Meneja wa Pori la Akiba la Maswa Lasato Masinde amezitaja baadhi ya changamoto za kuingiza mifugo katika maeneo ya Hifadhi kuwa ni ushindani wa malisho na maji kati ya wanyamapori na wafugwao,ongezeko la ujangili, kuuwawa kwa wanyamapori hasa walao nyama, magonjwa na mmonyoko wa udongo kutokana na wafugaji kukata miti.
Aidha, Masinde amefafanua kuwa suala la uingizwaji wa mifugo katika hifadhi linachangiwa pia na baadhi ya viongozi wa vijiji wasiokuwa waadilifu ambao hupokea fedha kwa wafugaji na kuwaruhusu kuingiza mifugo yao, jambo ambalo Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Meatu kuwachukulia hatua stahiki wale wote watakaobainika kujihusisha na uhalifu huo.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ametoa wito kwa wafugaji kupima maeneo yao wanayomiliki na kuyawekea miundombinu ya mifugo kama vile visima vya maji na mabwawa, majosho na mashamba ya malisho ili waweze kufuga kisasa na kuondokana na adha ya kuhangaika kutafuta maji na malisho.
Katika kikao hicho wafugaji kwa pamoja wamekubali kutoa mifugo katika maeneo ya hifadhi na kukubaliana na ushauri wa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu wa kupima maeneo yao na kuweka miundombinu, hivyo wameomba watalaam wa Ardhi na Mifugo waweze kuwasaidia namna wanavyoweza kutumia maeneo yao kufuga kisasa.
No comments:
Post a Comment