ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, August 30, 2017

SERIKALI YATUMIA BILIONI 85 KUPELEKA MAWASILIANO VIJIJINI

 Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akifafanua jambo katika kikao na Kamati ya Bunge ya Miundombinu kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) mjini Dodoma. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Moshi Kakoso na kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Mawasiliano wa Wizara hiyo Eng. Angelina Madete.
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Eng. Angelina Madete akifafanua jambo kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu kuhusu miradi ya maendeleo ya mawasiliano vijijini katika kikao kilichofanyika mjini Dodoma.
 Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Moshi Kasoso, akisisitiza jambo kwa wajumbe wa Kamati hiyo katika kikao kilichowakutanisha na uongozi wa Wizara ya  Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano  na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) mjini Dodoma. Kulia kwake ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo Eng. Edwin Ngonyani.
Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Dua Nkurua, akitoa maoni  kuhusu ufikishaji wa mawasiliano vijijini kwa viongozi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (hawapo pichani) katika kikao na Kamati hiyo mjini Dodoma. Kushoto kwake ni Mjumbe wa Kamati hiyo Mhe. Bhagwanji Meisuria na kulia ni Katibu wa Kamati hiyo Bw. Richard Masuke.

Serikali imesema kuwa imetumia shilingi Bilioni 85 kupeleka mawasiliano vijijini kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa kuzipatia ruzuku kampuni za simu za mkononi ili kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata huduma za mawasiliano.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwenye Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu mjini Dodoma.
“Mfuko huu unaendelea kuhakikisha kuwa mawasiliano bora yanafika katika maeneo mengi nchini hususan vijijini na kwenye maeneo ambayo hayana mvuto wa kibiashara ambapo Takwimu zinabainisha kuwa, tayari mawasiliano   yamefikishwa kwenye kata 443, vijiji 1,939  kuanzia mwezi Machi 2013 hadi Julai mwaka huu”, amefafanua Naibu Waziri Ngonyani.
Ameongeza kuwa tayari Mfuko umetiliana saini mkataba na kampuni za simu za mkononi mwezi Agosti mwaka huu kuhakikisha kuwa zinapeleka mawasiliano kwenye kata nyingine 75 na vijiji 154.
Aidha, ametanabaisha kuwa hadi hivi sasa asilimia 94 ya wananchi wanapata huduma ya mawasiliano nchini na kuongeza kuwa, Serikali kupitia mkataba wake na Kampuni ya Simu ya Halotel imefikisha mawasiliano kwenye jumla ya vijiji 3,069 kati ya vijiji 4,000 tangu walipoanza utekelezaji wa jukumu hilo mwezi Novemba, 2015 na wanatarajia kukamilisha kazi hiyo ifikapo mwezi Novemba mwaka huu.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu Mhe. Moshi Kakoso, amezitaka kampuni za simu za mkononi zinazopeleka mawasiliano vijijini na maeneo yasiyokuwa na mvuto wa kibiashara ambazo zinapatiwa ruzuku na Serikali kuhakikisha kuwa zinatoa taarifa sahihi kwa Mfuko huo ikiwemo hatua zilizofikiwa za ujenzi na usimikaji wa minara na uwepo wa mawasiliano kwenye vijiji husika.
 Amewataka UCSAF kujitangaza na kuweka mabango yao kwenye minara yote nchini iliyojengwa kupitia ruzuku ya Serikali ili kuwawezesha wananchi kutambua uwajibikaji wa Serikali katika kufikisha mawasiliano kwa wananchi wake.
Naye, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Eng. Angelina Madete, amesema kuwa Wizara kupitia UCSAF itahakikisha kuwa kila mwananchi anafikiwa na mawasiliano kuendana na jukumu la msingi la Mfuko huo la kufikisha mawasiliano kwa wote.
Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo Eng. Peter Ulanga, amewahakakikishia wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu kuwa Taasisi yake itashirikiana na wataalam kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kuhakiki kazi zilizofanywa na kampuni za simu za mkononi za ujenzi na usimikaji wa minara na uwepo wa mawasiliano kwenye vijiji mbalimbali nchini.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

No comments: