Mahakama ya Juu nchini Kenya imefuta matokeo ya urais yaliyompa ushindi Rais Uhuru Kenyatta kuwa madarakani kwa muhula wa pili.
Mgombea wa Muungano wa Nasa, Raila Odinga alifungua kesi mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika Agosti 8, akisema ulitawaliwa na udanganyifu ikiwemo kuchezewa mitambo ya kujumlishia matokeo.
Katika uamuzi wake, Mahakama imesema uchaguzi huo ulikuwa na dosari nyingi, hivyo kukiuka misingi ya uchaguzi huru na wa haki kama ilivyoelekezwa katika Katiba ya nchi hiyo.
Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Taifa hilo kwa Mahakama ya Juu kufuta matokeo ya uchaguzi na inaweka rekodi mpya katika historia ya uchaguzi barani Afrika ndani ya mfumo wa vyama vingi.
Katika uchaguzi wa Agosti 8, Kenyatta alitangazwa mshindi kwa kupata kura 8,203,290 sawa na asilimia 54.27, huku mpinzani wake Odinga akipata kura 6,762,224 sawa na asilimia 44.74.
Katika uchaguzi uliopita, Odinga alienda mahakamani kupinga matokeo lakini Mahakama hiyo ilitupilia mbali hoja zake na kuridhia matokeo yaliyompa ushindi Rais Kenyatta.
Kwa uamuzi uliotolewa na mahakama, uchaguzi mwingine unapaswa kufanyika katika kipindi cha siku 60. Iwapo ushindi wa Kenyatta ungeidhinishwa angepaswa kuapishwa Septemba 12.
Kumekuwa na shamrashamra katika mitaa mbalimbali ya Nairobi na Mombasa kushangilia uamuzi huo, huku Odinga akiwa na wanasiasa wenzake wamepongeza wakisema watatoa taarifa zaidi baadaye.
No comments:
Post a Comment