Sunday, September 10, 2017

Mjane aomba kuishi jengo la shule Kiluvya

By Jackline Masinde na Hidaya Nyanga mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Farida Mikashikashi (50), mjane anayeishi Gogoni “B” Kiluvya ameomba kuishi katika majengo ya Shule ya Msingi ya Kiluvya, endapo nyumba yake itabomolewa kupisha upanuzi wa Barabara ya Morogoro.

Nyumba zilizo ndani ya mita 121 kutoka katikati ya barabara hiyo, zinabomolewa na Wakala wa Barabara (Tanroads) kwa ajili ya kupanua eneo la kuanzia Ubungo hadi Kiluvya.

Uamuzi wa kubomoa nyumba hizo umewakuta wakazi wengi wa eneo hilo wakiwa hawajajiandaa, na kulazimisha baadhi kuishi kwenye mapagala ya nyumba zao baada ya kubomolewa. Na Farida, ambaye anadai mumewe alifariki Septemba tatu kutokana na mshtuko, anategemea hali kama hiyo.

“Sina pa kwenda,” alisema Farida akiongea na Mwananchi.

“Endapo watakuja kubomoa, nitaomba shule inipe walau hata chumba kimoja ili niishi kwa muda mpaka nitakapopata mahali pa kuishi.”

Mama huyo alisema bado yupo katika kipindi cha eda cha siku 40 kuomboleza kifo cha mumewe, kwa mujibu wa utaratibu wa dini ya Kiislamu.

“Kwa kawaida mke ukifiwa na mume utaratibu wa dini unatakiwa kukaa ndani siku 40 bila kutoka nje. Hofu yangu ni kwamba naweza nisimalize eda maana nasikia watakuja siku yoyote na leo nina siku ya tano tangu nianze,” alisema.

Alisema Jumatano iliyopita, Tanroads walibomoa nyumba za jirani zake na kitendo hicho kimemfanya aingiwe na hofu kiasi cha kutoa vitu nje.

Alisema watoto wake wanataka kumtafuta mkuu wa shule ili wamfikishie maombi yao ya kuishi eneo hilo.

“Tulitoa nje kila kitu, ikabidi sasa tufanye utaratibu wa kuanza kumtafuta mkuu wa shule atusaidie darasa moja,” alisema.

“Bahati nzuri Tanroads waliacha kubomoa nyumba za jirani na wakaondoka, nikapumua.

“Nafikiri shuleni ndipo kutakuwa na msaada pekee mwanangu (mwandishi). Sina mahali ambako nitaweza kupata msaada zaidi ya shule. Ikishindikana basi nyumba hii ndiyo itakuwa jeneza langu. Nitalala humuhumu, wabomoe nikiwa ndani.”

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, mkuu wa shule hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Ishengoma, hakutaka kulizungumzia.

“Samahani siwezi kuzungumza chochote mpaka nipate kibali kutoka kwa mkurugenzi. Najua ni majibu mepesi lakini siwezi,” alisema.

Hata hivyo, mwenyekiti wa mtaa huo, Julius Mgini aliiambia Mwananchi kuwa ni vigumu kumtimizia mwanamke huyo maombi yake.

“Hatuwezi kumpangisha mtu katika madarasa ya shule kwa sababu shule yenyewe ina vyumba vichache. Suala hilo haliwezekani kabisa, nasema mimi kama kiongozi wa shule,” alisema.

“Mjane huyo kwao ni Morogoro. Kama anaona atakosa pa kuishi, arudi kwao lakini kwa suala hilo haitawezekana.”

Kuhusu kurudi Morogoro, Farida alisema: “Sikatai, ni kweli nina ndugu (Morogoro), lakini kwa usawa huu kwenda kuishi kwa mtu nani atakubali?”

Wakati mjane huyo akiomba malazi ya muda, juzi Mwananchi ilikuta ubomoaji ukiendelea eneo la Mbezi kwa Yusuph saa 11:00 jioni. Katika eneo hilo kulikuwa na umati mkubwa wa watu wakiwa wamezingira nyumba moja iliyojengwa kwa mabati na nje alikuwepo kikongwe anayeonekana kuwa na umri wa miaka tisini anayeitwa Athuman Said.

“Kuna mgonjwa hawezi kutembea wala kuongea na ni mzee ambaye nyumba yake inatakiwa kubomolewa muda wowote kuanzia sasa,” alisema mmoja wa watu waliokuwepo eneo hilo baada ya kuulizwa na Mwananchi.

Wakati mzee huyo akiwa nje, Mwajuma Hussen (70) ambaye alijitambulisha kuwa ni mke wake, alikuwa akitoa vitu ndani kujiandaa kwa ubomoaji ambao ulikuwa unaendelea katika nyumba ya jirani.

“Hapa tunaishi wawili tu, hatukubahatika kuwa na watoto,” alisema mama huyo.

“Eneo hili tumeishi miaka mingi sana, wabomoaji wamekuja hapa wakatuambia wanataka kubomoa nikawaambia jamani mimi nina mgonjwa ndani.”

Mama huyo, ambaye alikuwa akibubujikwa na machozi na kutetemeka mikono wakati akifanya kazi hiyo, alisema baada ya kuwaambia kuwa ana mgonjwa, walimtaka aanze kutoa vitu vya ndani na kuondoa mabati taratibu.

“Unaniona hapa natoa vitu nje na mgonjwa wangu ndiyo huyo yuko hapo nje hawezi kutembea, haoni wala hasikii,” alisema.

“Sasa sijui hata nifanyeje, nimechanganyikiwa. Najiuliza nitakwenda wapi na huyu mgonjwa? Bora hata tungekuwa na mtoto angetusaidia, hatuna hata wa dawa mjukuu wangu.”

Baadhi ya watu waliokuwa eneo hilo walikuwa wakihangaika kumtafutia makazi mgonjwa huyo.

“Jamani muondoeni huyu mgonjwa hapa nje mpelekeni hata kwa majirani ambao nyumba hazibomolewi, anaumia,” alisikika mmoja wa watu hao.

Kutokana na hali ya baridi, vumbi na kelele, mgonjwa huyo alibebwa na kurudishwa ndani ya nyumba yake baada ya kukosa sehemu ya kuhifadhiwa.

“Wakija kubomoa, atatolewa maana anaumia,” alisema mkazi mwingine.

Hata hivyo, maofisa Tanroads hawakuigusa nyumba hiyo, badala yake wakamtaka aendelee kubomoa taratibu kabla ya wao kwenda kuimalizia.

No comments: