ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, September 20, 2017

MRISHO MPOTO KUIWAKILISHA TANZANIA KATIKA TAMASHA LA UTALII DUNIANI NCHINI CHINA

Mamia ya wadau wa sanaa wamejitokeza kwa wingi Jumanne hii jioni katika Uwanja wa ndege wa JK Nyerere jijini Dar es salaam kumuaga msanii wa muziki wa asili nchini, Mrisho Mpoto ambaye ameelekea nchini China kwaajili  ya kuiwakilisha Tanzania katika tamasha la utalii wa sanaa duniani.

Muimbaji huyo ambaye anafanya vizuri na wimbo, Kitendawili alitangaza katika mitandao yake ya kijamii kwamba atasafiri Jumanne hii kuelekea nchini China hali iliyopelekea mashabiki wengi kumimika uwanjani hapo kwaajili ya kumuaga.

Akiongea na waandishi waliojitokeza uwanjani hapo, Mpoto alisema anawashukuru mamia ya watu waliojitokeza uwanjani hapo kwaajili ya kumuaga kwenda kuiwakilisha nchi katika masuala ya kiutalii nchini China.

“Sikutegemea kama watu watakuwa wengi hivi, huu ni upendo wa dhati sana na nawashukuru sana kwa moyo huo na upendo mliouonyesha, nakwenda China kwaajili ya Watanzania, sio Mpoto lakini nakwenda kuuonyesha ulimwengu kwamba Tanzania tuna utajiri wa sanaa, Tanzania tuna makabila zaidi ya mia moja na ishirini hiki ni kitu kikubwa sana, tunaenda kuwatambia usalama tuliokuwa nao,” alisema Mrisho.


Muimbaji huyo amedai haikuwa kazi rahisi kupata kazi hiyo na kuwa muakilishi pekee wa Tanzania kwenye maadhimisho hayo ya utalii duniani ambayo yanawakutanisha mataifa mbalimbali duniani.

Aliongeza, “Mungu bado anaendelea kutuona, kati ya nchi zote za Afrika ni nchi tatu tu ambazo zimepata mualiko huu ikiwemo Tanzania na Kenya. Hii ni ishara nzuri sana duniani na Afrika nzima kwa sababu wadau ambao watatembelea mahadhisho hayo washuhudia vitu vyetu vya asili, ngoma, nyimbo, ala za muziki pamoja na mitindo mbalimbali ya upigaji wa ngoma,”

Alisema safari hiyo imewezeshwa na  Ubalozi wa Tanzania China, Wizara ya Utamaduni, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, TANAPA, TTB, BASATA pamoja na Leopard Tours.

No comments: