Na Tiganya Vincent
WATU saba wa kijiji cha Mwambondo wilayani Uyui wanashirikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuwashambulia na kuwauunguza kwa moto wanawake waanne wakiwatuhumu kuwa wachawi na wanahusika na kifo cha mume wa mmoja wao.
Kauli hiyo imetolewa jana mjini hapa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati wa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu taarifa alizozipata kutoka kwa Kamanda wa Polisi Mkoa huo Wilbroad Mtafungwa.
Alisema kuwa chanzo cha vitendo hivyo vya kinyama zilianzia baada ya Mtu mmoja alikuwa akiitwa Mafumba Jirawisi kufariki kwa sababu ya maradhi lakini baadhi ya watu walianza kumtuhumu mke wa marehemu anayeitwa Manugwa Lutema kuhusika na kifo cha mume wake na kuamua kumpeleka porini na kuanza kumshambulia huku wakitaka awaeleze watu wanaoshirikiana naye kuwafanya vitendo vya kichawi.
Mwanri alisema kuwa mama huyo baada ya kupiga sana na kuumia aliamua kutaja ovyo majina ya majirani zake na ndipo nao wakaunganishwa naye na kuendelea kupigwa na kuunguzwa katika sehemu za siri.
Kufuatia vitendo hivyo vya kinyama Mkuu huyo wa Mkoa amemwagiza kuwasaka watu waliobaki ambao wamehusika katika kitendo hicho wakiwemo Makamanda wa sungusungu ili hatua kali ziweze kuchukuliwa dhidi yao.
Mmoja wa majeruhi wa tukio hilo la kinyama alisema kuwa alilazimika kutaja majirani zake ili kutaka kunusu roho yake baada ya kuona mashambulizi yanazidi na anasikia maumivu makali.
Kwa upande wa ndugu wa waathiri wameomba wagonjwa wao watibiwe bure kwa sababu tukio hilo limetokea wakati wakiwa hawana kitu na hawajiandaa na kutokuwa na fedha ya kulipia matibabu
Akijibu ombi la ndugu hao Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Gunin Kamba alisema wagonjwa wote walijeruhiwa na kuuguzwa moto watapewa matibabu kwa mkopo katika Hospitali hiyo ya Rufaa ya Mkoa ya Kitete ,malipo yatafanyika baadaye.
Alisema kuwa lengo ni kutaka kwanza kuokoa maisha yao kutokana na unyama waliofanyiwa na kundi hilo la watu.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Kitete Dkt.Nassor Kaponta alisema kuwa wanaendelea kuwapatia huduma katika Hospitali hiyo na hakuna majeruhi ambaye atahamishiwa kwingine kwa sababu wanauwezo wa kuwasaidia wakiwa katika eneo hilo hilo.
Aliwataja waliojeruhiwa ni Maria Sahani , Elizabeth Kashindye, Manugwa Lutema na Raheli Mikomangwa. Kabla ya kufariki marehemu ambaye alikuwa mganga wa kienyeji alikwenda kutoa matibabu kijiji cha jirani na baada ya kurejesha akaanza kuumwa na hatimaye usiku wake alifariki kwa sababu ya ugonjwa.
Vitendo vya kinyama ikiwemo mauaji kwa wanawake Mkoani Tabora vinaanza kuonekana kama vya kawaida ambapo mapema mwezi Agosti mwaka huu wilayani Nzega wakinamama watano walipoteza maisha baada ya kushambuliwa na kisha kuchomwa moto na mwei huo huo wilayani Sikonge mtu mmoja alinusurika kifo baada ya kufungiwa nyumbani kwake na nyuma kuwekwa moto
No comments:
Post a Comment