Kaimu Mkurugenzi wa Maadili toka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Lambert Chialo (kushoto) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akieleza umuhimu wa watumishi wa Umma kuzingatia maadili kazini, kulia ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini toka Ofisi ya Rais Bi. Mary Mwakapenda. Picha na Eliphace Marwa - Maelezo
Na. Georgina Misama – MAELEZO
Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imewaonya watumishi wa Umma kutoa taarifa za serikali za siri na za kawaida kwa watu ambao sio walengwa wa taarifa hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Maadili kutoka Wizara hiyo Lambert Chialo alisema kwamba kwa mujibu wa sheria ya Usalama wa Taifa Na. 3 ya mwaka 1970 na marekebisho yake, Ibara ya 5(a) na (b), adhabu ya uvujaji wa siri ni kifungo kisichozidi miaka 20.
“Hivi karibuni tumeshuhudia taarifa za serikali za siri zikitumwa katika vyombo vya habari pamoja na mitandao mbalimbali ya kijamii kitu ambacho ni kosa kisheria na ni kinyume cha Kanuni za Maadili ambapo inasisitizwa kuwa na matumizi sahihi ya taarifa”, alisema Chialo.
Chialo aliongeza kwamba lengo la serikali si kuficha taarifa kwa wadau wake, bali taarifa zinazotolewa zinapaswa kutolewa kwa utaratibu maalumu na kupelekwa kwa watu wanaopaswa kupokea taarifa hizo (walengwa). Aidha, taarifa zinazotolewa na taasisi husika lazima zipate idhini kwa Uongozi husika kabla ya kupelekwa kwa wadau.
Akiongelea suala la matumizi mabaya ya Ofisi, Chialo alisema kwamba baadhi ya watumishi wamekuwa wakitumia nafasi walizonazo kwa manufaa yao binafsi na sio ya Umma, kwa kufanya hivyo ni kosa kisheria na watumishi watakaogundulika watawajibishwa kwa mujibu wa Kanuni na taratibu.
Watumishi wa Umma wanapaswa kufahamu kwamba serikali inaendelea kufatilia matendo yote yasiyo ya kimaadili na kuchukua hatua kila inapobidi. Aidha, wananchi wanaombwa kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za ukiukwaji wa maadili katika taasisi za umma kila wanaposhuhudia matukio hayo.
“Tunalo dawati la msaada kwa ajili ya kupokea maoni, malalamiko, ushauri na taarifa mbalimbali katika kuhakikisha utoaji wa huduma za serikali kwa wananchi unaboreshwa” alisema Chialo.
Chialo alitoa rai kwa wananchi wote kwa ujumla, kuzingatia swala la maadili kuanzia ngazi ya familia. Aidha, inasisitizwa viongozi na wasimamizi wa kazi kuendelea kuelimisha watumishi kuhusu suala la maadili na kuhakikisha watumishi wanaishi kwa kuzingatia kanuni na taratibu zilizopo kwa vitendo.
No comments:
Post a Comment