Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Filip Mpango (katikati) akiwa na viongozi wengine wa Serikali, Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP) Biswalo Mganga (kushoto), Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato nchini TRA Charles Kichere(kulia) Naibu Kamishna Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Brigedia Jenerali John Mbungo wakiangalia Mzigo wa Almasi uliokamatwa katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Filip Mpango akisoma maelezo ya mzigo huo ambayo yalikuwa tofauti kabisa na uhalisia mara baada ya kuhakikiwa na timu ya Wataalamu wa Kitanzania wazalendo. |
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Filip Mpango akipata maelezo ya mzigo huo ambayo yalikuwa tofauti kabisa na uhalisia mara baada ya kuhakikiwa na timu ya Wataalamu wa Kitanzania wazalendo.
Sehemu ya Mzigo huuo wa Almasi uliokamatwa katika uwanja wa Ndege ambao thamani yake ni zaidi ya Tsh. Bilioni 65.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Filip Mpango akizungumza wakati akipokea Ripoti ya Uchunguzi wa Madini hayo ya Almasi jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akiongea na wanahabari baada ya kufanya ziara ya kushtukiza, kufuatilia Almasi iliyokamatwa ikisafirishwa kwenda nje ya nchi huku ikiwa imethaminiwa chini ya kiwango katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam. Kulia kwake ni Naibu Kamishna Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Brigedia Jenerali John Mbungo, Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Charles Kichere na Kushoto kwake ni Kamishna wa Madini Tanzania Mhandisi Benjamini Mchwampaka Msajili wa Hazina Dkt. Oswald Mashindano na kulia kabisa ni Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Bw. John Biswalo.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), ameviagiza vyombo vinavyohusika kuchukua hatua za kisheria dhidi ya kampuni ya Williamson Diamond Ltd na wote waliohusika kuidhinisha usafirishaji wa madini ya almasi kutoka migodi ya kampuni hiyo na kudanganya thamani halisi ya madini hayo kwa lengo la kuisababishia hasara Serikali.
Dkt. Mpango ametoa agizo hilo leo tarehe 09 Septemba, 2017 baada ya kukagua madini ya almasi yaliyokamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam yakisafirishwa kupelekwa nchini Ubelgiji.
Miongoni mwa hatua za kisheria ni pamoja na kutaifisha madini yote ya almasi yaliyokamatwa baada ya kubainika udanganyifu wa thamani yake halisi, kuwakamata na kuwachunguza wote waliohusika katika udanganyifu huo wakiwemo wajumbe wa bodi zilizomaliza muda wake na wafanyakazi waliopo na waliostaafu.
Almasi hiyo ilikamatwa tarehe 31 Agosti, 2017 muda mfupi kabla ya kupakizwa kwenye ndege ili isafirishwe kwenda nchini Ubelgiji, na ilipochunguzwa ilibainika kuwa nyaraka za kampuni ya Williamson Diamond Ltd zimeonesha kuwa almasi hiyo ina thamani ya Dola za Marekani Milioni 14.798 sawa na Shilingi Bilioni 33 za Tanzania wakati thamani yake halisi ni Dola za Marekani Milioni 29.5 sawa na Shilingi Bilioni 65 za Tanzania.
Kabla ya kukagua almasi hiyo Waziri Mpango amepokea taarifa ya timu ya wataalamu iliyofanya tathmini ya thamani halisi ya madini hayo ambapo kiongozi wa timu hiyo Prof. Abdulkarim Mruma amesema pamoja na kubaini upotevu mkubwa wa fedha, kuna dosari nyingine zikiwemo kukosekana kwa vifaa ya kupimia madini hayo, almasi kusafirishwa na kuuzwa sokoni bila uwepo wa mwakilishi wa Serikali na ameshauri hatua za udhibiti huo zifanyike katika madini yote yanayochimbwa hapa nchini.
Pamoja na kuipongeza timu iliyofanya tathmini hiyo na vyombo vya dola vilivyokamata madini hayo Waziri Mpango amesema Serikali itatekeleza ushauri wote uliotolewa na timu ya Prof. Mruma na kwamba kuanzia sasa almasi inayozalishwa hapa nchini itasindikizwa na maafisa wa Serikali hadi sokoni na inataka kuanza kupokea gawio halali kutoka mgodi huo.
Waziri Mpango ametoa maagizo hayo mbele ya viongozi wa vyombo mbalimbli wakiwemo Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Charles Kichere, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Bw. Biswalo Mganga, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Brigedia Jenerali John Julius Mbungo, Kamishna wa Madini Tanzania Mhandisi Benjamin Mchwampaka na Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam SACP - Lazaro Mambosasa.
Imetolewa na Benny Mwaipaja
MKUU WA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO
No comments:
Post a Comment