ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, October 5, 2017

BALOZI WA MOROCCO ATEMBELEA TADB

Na mwandishi wetu,

Balozi wa Morocco nchini Tanzania, Mheshimiwa Abdelilah Benryane ametembelea Ofisi za Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili kufuatilia utekelezaji wa Mkataba wa Ushirikiano uliosainiwa kati ya Serikali ya Tanzania na Morocco wakati wa Ziara ya Mfalme wa Morocco Mtukufu Mohammed VI alipotembelea nchini Tanzania mwezi Oktaba mwaka jana.

Mheshimiwa Benryane ambaye alifuatana na uongozi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya Morocco (GCAM), ulioko nchini kwa ajili ya kikao cha pamoja cha ushirikiano na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya kilimo inayotekelezwa kati ya Benki hiyo na TADB.

Akizungumza wakati wa kikao cha pamoja kati ya GCAM na TADB, Mheshimiwa Benryane alisema kuwa utekelezaji wa makubaliano kati ya Mfalme wa Morocco na Rais Dkt. John Pombe Magufuli yanaendelea vizuri na kutolea mfano mashirikiano kati ya benki hizo mbili kwa upande wa miradi ya kilimo.

“Ni chini ya mwaka mmoja tangu viongozi wetu wakubaliane utekelezaji wa mikataba 21 katika nyanja mbalimbali zikiwamo za kilimo, gesi, madini na na usafiri wa anga,” amesema.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga aliishukuru GCAM kuichagua TADB kusimamia miradi ya utekelezaji wa makubaliano hayo kwa upande wa kilimo.

Kwa mujibu wa Bw. Assenga, pamoja na kupanga mikakati hiyo, ujumbe huo ulipata fursa ya kukagua miradi kadhaa ya kilimo na ufugaji ambayo Tanzania inaweza kuianzisha kwa mafanikio.

TADB imeanzishwa kwa malengo makuu ya Kusaidia upatikanaji wa utoshelezi na usalama wa chakula ambao ni endelevu nchini Tanzania; na Kuchagiza na kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.
Balozi wa Morocco nchini Tanzania, Mheshimiwa Abdelilah Benryane (kulia) akisaini kitabu cha wageni wakati alipotembelea Ofisi za Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB). Wanaoshuhudia ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya Morocco (GCAM), Bw. Jamal Eddine el Jamali (katikati).
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga (aliyesimama) akizungumza wakati wa kikao cha pamoja cha ushirikiano kati ya TADB na GCAM.
Balozi wa Morocco nchini Tanzania, Mheshimiwa Abdelilah Benryane (kulia) akizungumzia mafanikio ya utekelezaji wa makubaliano kati ya Mfalme wa Morocco na Rais Dkt. John Pombe Magufuli. Wengine pichani ni Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya Morocco (GCAM), Bw. Jamal Eddine el Jamali (katikati) na Mkurugenzi wa masuala ya kilimo ya GCAM, Bw. Mustapha Chehhar.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga (kushoto) akimsikiliza kwa makini Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Suleiman Saleh (kulia) wakati wa kikao cha pamoja kati ya GCAM na TADB.
Balozi wa Morocco nchini Tanzania, Mheshimiwa Abdelilah Benryane (kushoto) akiangalia zawadi aliyokabidhiwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga (kulia) mara baada yakikao cha pamoja kati ya GCAM na TADB.
Balozi wa Morocco nchini Tanzania, Mheshimiwa Abdelilah Benryane (wapili kushoto) akionesha picha ya mchoro wa tembo aliyokabidhiwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga (wapili kulia) mara baada ya kikao cha pamoja kati ya GCAM na TADB. Wanaoshuhudia ni Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya Morocco (GCAM), Bw. Jamal Eddine el Jamali (kushoto) na Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Suleiman Saleh (kulia).

Picha ya pamoja! Balozi wa Morocco nchini Tanzania, Mheshimiwa Abdelilah Benryane (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na mara baada ya kikao cha pamoja kati ya GCAM na TADB.

No comments: