ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, October 1, 2017

RC RUKWA AWATAHADHARISHA WANANCHI KUJIANDAA NA MSIMU WA MVUA

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amewatahadharisha wananchi wa Mkoa huo kujihadhari na mvua zilizoanza na upepo ulioezua baadhi ya paa za nyumba na vituo vya kutolea huduma katika baadhi ya maeneo ya mkoa.


Amesema kuwa sasa ni wakati wa wazazi kuwachunga watoto katika msimu huu wa mvua na kuongeza kuwa wenye nyumba hawanabudi kuimarisha majengo yao mapema ili kuepukana na hasara ambayo wangeweza kuipata baada ya madhara kutokea.

“Ni wakati muafaka hivi sasa kila mtu kuchukua tahadhari kuangalia watoto, kukagua majengo yetu kuona kuwa yapo imara na pale ambapo ninatokea basi wajue sehemu salama ya kukimbilia ili kuokoa Maisha,”


Ameyasema hayo aliposhiriki kufanya usafi nyumbani kwake eneo la Mkoani, mjini Sumbawanga. Ambapo alisema kuwa suala la usafi linaanzia nyumbani kwa mtu na kuwa wananchi wafanye usafi kwa faida yao wenyewe na kuendelea kuwasisitiza Wakurugenzi wa Halmashauri kuendelea kusimamia usafi kuanzia ngazi ya Kijiji au mtaa ili kutekeleza agizo lake la kufanya usafi kuanzia katika ngazi hizo.

“Nimewaagiza wakurugenzi na wataalamu wake wakague usafi kwasababu suala la usafi ni faida kwa kila mtu, siyo faida ya rais wa la mkuu wa mkoa pekee, kwasababu tukiingiliwa na magonjwa halitakuwa la rais peke yake,” Alisema


Pamoja na hayo Mh. Zelote aliwaonya wenye tabia ya kuchoma misitu hasa katika kipindi hiki cha kukaribia msimu wa kilimo, hivyo amewasisitiza viongozi kuanzia ngazi ya Kijiji kushirikiana kuhakikisha kuwa jambo hilo halijitokezi.


“Katika kipindi hiki uchomaji hovyo wa mioto unaonekana kushika kasi, ni juu ya serikali ya Kijiji ama kata kuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba mioto haiwashwi ovyo ovyo na atakayefanya hivyo achukuliwe hatua za kisheriakwani mambo haya huaribu mazingira na pia usipodhibitiwa hule madhara,” Alisisitiza.

No comments: