ANGALIA LIVE NEWS

Monday, November 6, 2017

WATU 26 WAUAWA KWA KUPIGWA RISASI KANISANI

Watu 26 wameuawa kwa kupigwa risasi na mtu mwenye silaha aliyewafyatulia risasi waumini katika kanisa moja lililopo jimbo la Texas nchini Marekani wakati wa ibada iliyofanyika jumapili.

Shambulio hilo lilitekelezwa katika kanisa la First Baptist Church katika mji wa Sutherland Springs, mji mdogo katika wilaya ya Wilson, Texas.

Mshambuliaji, ambaye anadaiwa kuuawa baada ya kutekeleza mauaji hayo, aliingia kanisani na kuanza kuwafyatulia risasi watu mwendo wa saa tano unusu asubuhi (17:30 GMT).
Gavana Greg Abbott amethibitisha idadi ya waliofariki na kusema ndicho kisa kibaya zaidi cha mauaji ya kutekelezwa kwa kutumia bunduki katika historia ya texas.

“Ni majonzi makubwa kwa wafiwa hili ni tukio ambalo halivumiliki ambalo limetokea, nawapa pole sana kwa wafiwa na huu ni msiba wa taifa, hivyo tunaungana kwa pamoja katika majonzi haya,”amesema Gavana Greg
Mkuu wa idara ya usalama wa Texas Freeman Martin amesema waathiriwa walikuwa na umri wa kati ya miaka 5 na 72.

Maafisa wamesema watu zaidi ya 20 pia walijeruhiwa na wamelazwa hospitalini.
Bw Martin amesema mshukiwa ni mwanamume mzungu wa umri wa miaka 20 ambaye alikuwa amevalia mavazi meusi na fulana ya kujikinga dhidi ya risasi pamoja na kuwa na bunduki yenye uwezo mkubwa.

Alianza kufyatua risasi nje ya kanisa kabla ya kuingia ndani na kuendelea kufyatulia watu risasi.
Raia mmoja  alitwaa bunduki yake na kuanza kumfyatulia  risasi mshukiwa kabla ya mshukiwa huyo kutoroka akitumia gari.

Raia huyo alimwandama mshukiwa huyo ambaye aliendesha gari lake na kisha kuliangusha katika barabara wilaya ya Guadalupe.
Polisi waelimpata mshukiwa akiwa amefariki ndani ya gari lake.Haijabainika iwapo alifariki kutokana na majeraha ya risasi aliyojisababishia mwenyewe au kutokana na mejaraha kutoka kwa raia huyo

Mshukiwa ametajwa kuwa Devin P Kelley, 26, kwa mujibu wa vyombo vya jhabari Marekani, lakini Polisi bado hawajathibitisha jina lake.
Mhubiri wa kanisa hilo la First Baptist Frank Pomeroy, ameiambia ABC News kwamba binti yake wa miaka 14 kwa jina Annabelle ni miongoni mwa waliouawa.

Sutherland Springs ni mtaa mdogo wenye wakazi wasiozidi elfu moja ambao hupatikana kilomita 50 hivi kusini mashariki mwa mji wa San Antonio mjini Texas.

Maafisa wa FBI kutoka San Antonio wametumwa kufanya uchunguzi lakini kufikia sasa lengo la mshambuliaji halijabainika.

FBI pia wamesema mshambuliaji alikuwa mmoja pekee, lakini bado wanachunguza uwezekano wa iwapo kuna mtu mwingine aliyehusika.

Rais Donald Trump, ambaye yumo ziarani Asia, ameshutumu kisa hicho na kusema ni “kitendo cha uovu” na kusema kwamba Wamarekani watajikwamua na kusalia na umoja.

“Na kupitia kwa machozi na kupitia huzuni hii, tunasalia imara, imara zaidi,” ameandika  Rais Trump

No comments: